Maskini Kikwete, serikali yake haina umoja tena!


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 22 February 2012

Printer-friendly version

NIKIRI kwamba kuna wakati namuonea huruma Rais Jakaya Kikwete. Ninamuonea huruma hasa pale ambapo naona mambo fulani yanamuelemea na inaonekana hana jibu la mambo hayo.

Katika historia yetu kama taifa hatujawahi kuwa na serikali ambayo haina umoja yenyewe kuliko wakati mwingine wowote ule na kama iliwahi kuwepo basi iliweza kuficha tofauti zake humo humo ndani.

Leo hii tunashuhudia vituko vya ajabu kabisa katika serikali hii na hapa nazungumzia tofauti kubwa inayotokea kati ya mawaziri. Mawaziri ndio washauri wakuu wa rais na ndio wasimamiaji wa sera ya chama chake katika serikali.

Ni hawa ambao wanatakiwa kuwa wanajua mambo yanayoendelea nchini na kwa kweli kabisa kama ingekuwa jeshini basi hawa ndio makamanda wa juu kabisa wanaopanga vita.

Vikao vya Baraza la mawaziri ni kama vikao vya mikakati ya kijeshi ambapo makamanda wa juu hukaa chini na kuangalia hali ya usalama inakwendaje, maendeleo ya mapambano yanakwendaje na kupanga mikakati ya kujipa nguvu zaidi au kusahihisha mahali ambapo pana matatizo.

Majemedari hao wanapokaa na kujipanga wanatakiwa kuleta mawazo yao tofauti mezani, wanazungumza wote, wanapingana kwa hoja lakini inapofikiwa uamuzi basi unakuwa ni uamuzi wa pamoja.

Katika serikali dhana ambayo inasimamia baraza la mawaziri ni ile inayojulikana kama uwajibikaji wa pamoja (Collective Responsibility).

Mawaziri wanapokula kiapo wanakula viapo kwa kawaida vitatu; wanakula kiapo cha kulinda katiba, kiapo cha kazi yake na vile vile kiapo cha kulinda siri za baraza la mawaziri.

Lengo la viapo hivyo ni kuhakikisha kuwa mawaziri wanamshauri rais kwa ukweli kabisa na kwa uwazi na kwa pamoja wanawajibika pamoja.

Hii ndio sababu wakati mwingine ndani ya bunge unaweza ukaona kuwa swali la mbunge limeulizwa kuhusu wizara moja, lakini waziri wa wizara nyingine akaamua kulijibia au kutoa nyongeza zaidi kwani serikali ni moja.

Ni kwa mantiki hiyo basi serikali nzima inatakiwa ionekane iko pamoja siyo sirini tu bali hata hadharani. Serikali inayopingana hadharani haiwezi kuwa na umoja sirini; na serikali inayopingana sirini bila kupatana, itajionesha hivyo hata hadharani!

Kama kuna jambo ambalo kwa kweli kabisa limefichua zaidi udhaifu wa serikali mbele ya wananchi ni jinsi serikali ya Rais Jakaya Kikwete ilivyoparaganyika katika suala la ugonjwa wa Dk. Harrison Mwakyembe, mbunge wa Kyera na naibu waziri wa ujenzi.

Tangu alipojitokeza karibu mwaka mmoja uliopita na kudai kuwa kuna watu wanataka kumdhuru mwitikio wa serikali umekuwa wa kusikitisha. Hawakutoa uzito wa kutosha na hata baadaye alipoanza kuugua ugonjwa huu wa ajabu mwitikio wa serikali ulikuwa ni ule ule wa “anatafuta kuungwa mkono na wananchi.”

Lakini tumeona hili zaidi baada ya mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai (DCI), Robert  Manumba akija na maelezo marefu ambayo yangeweza kushawishi akili za wale wanaoamini serikali bila kuuliza.

Kwa ufupi alichokisema kuhusu na madai ya Dk. Mwakyembe kuwekewa sumu kinaonesha tu jinsi gani serikali hiyo imekosa umakini.

Lakini kabla hatujatulia taarifa kuwa wizara ya Afya imeshangazwa na taarifa ya Manumba zinashangaza. Sasa kama Manumba hakupata taarifa zake wizarani atakuwa amepata wapi na kwanini alienda kuzungumza kwa uhakika tu kuwa “Mwakyembe hakulishwa sumu”?

Manumba hadi kuja hadharani na kuwashawishi watu kuwa habari hizi si za kweli bila japo kuelezea msingi wa hitimisho hilo ni nini?

Kinachoudhi wengi ni kuwa hakuna waandishi waliomuuliza maswali ya msingi ya kiakili ili japo tuweze kuona aweza kuwa kweli? Je, ulizungumza na Dk. Mwakyembe kabla ya kutoa ripoti yake kwa umma?

Je, alizungumza na daktari aliyemtibia? Alizungumza na hospitali ya Apollo? Uchunguzi wa vielelezo vya ugonjwa wa Mwakyembe vimefanywa wapi na jeshi la polisi? Polisi walichukua sampo yoyote kutoka kwa Mwakyembe na kuifanyia utafiti?

Maswali haya yote yalitakiwa yawe msingi wa majibu ya Manumba lakini akasimama na kusema tu kuwa “hakulishwa sumu.”

Bado tukiwa tunashangaza na tamko la wizara ya afya wakishangazwa na Manumba, rafiki wa Dk. Mwakyembe, Samwel Sitta naye anaendelea kutoa taarifa nzito zaidi akisisitiza kuwa madai yake kuwa Mwakyembe amepewa sumu ni ya kweli na hana shaka na hilo.

Haya yote yanatuachia maswali: Rais Kikwete yuko wapi? Tuliliona hili kwenye suala la katiba, tumeona katika suala la afya (mgomo wa madaktari) na tunaendelea kuliona kwenye suala la Mwakyembe?

Au ni kweli kama wanavyodai wapinzani wake kuwa Kikwete ni kiongozi dhaifu? Ni kweli kwamba hawezi kuchukua maamuzi ya kuonesha uongozi na kutokuvumilia mgongano wa wa wazi kati ya mawaziri wake wanne - waziri wa Afya, waziri wa mambo ya ndani, naibu waziri – ujenzi na waziri wa afrika ya mashariki?

Yawezekana Kikwete sasa ameamua kuacha mambo yawe kama yalivyo tu alimradi tunakwenda?

Kuna watu ambao wanategemea kuwa Rais Kikwete ataamua kuvunja baraza la mawaziri kukabiliana na udhaifu kama huu wa serikali aliyoiunda yeye mwenyewe.

Kwa baadhi yetu akifanya hivyo atathibitiha kile ambacho kiko mbele ya wengi – kwamba ameshindwa kusimamia serikali yake na sasa njia pekee ni ya kuivunja na kuanza upya.

Tatizo ni kuwa hata akivunja serikali mara saba au kila wiki watu atakaowaingiza ni watu kutoka chama kile kile, bunge lile lile na bado yeye atakuwa mkuu wao!

Hivi ni kweli watu wanafikiria baraza jingine likiundwa litakuwa tofauti na hili la sasa? Litakuwa na umoja wa maono na uongozi? Kutoka shamba lilelile, mavuno ni yale yale!

mwanakijiji@jamiiforums.com
0
Your rating: None Average: 4.5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: