Maswali muhimu kwa Ali Fereji Tamim


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 09 May 2011

Printer-friendly version

ALI Fereji Tamim anaweza awe anapata urahisi katika kinyang’anyiro cha uenyekiti katika kila uchaguzi wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), lakini hajafanikisha hoja kuu anayotumia kujinadi.

Katika kipindi chote cha miaka 20 iliyopita, Ali Fereji amekuwa akitumia hoja ya kufanikisha mikakati ya ZFA kujiunga na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA)

Juhudi hizo zimeangukia patupu. Lakini kila akigombea Fereji anashinda kwa hoja hiyo hiyo, na akiingia yeye na timu yake wamekuwa wakidai wataongeza kasi.

Mwaka 1998 Tamim pamoja na aliyekuwa makamu mwenyekiti wa ZFA, Ibrahim Raza walidanganya umma waliposema Zanzibar imekubaliwa uanachama wa FIFA.

Madai hayo yalisababisha aliyekuwa Waziri wa Elimu na Michezo, Prof. Juma Kapuya kutangaza bungeni mjini Dodoma kuwa Zanzibar pia ni mwanachama wa FIFA. Siku chache baadaye ilikuja kubainika kuwa si kweli.

Ilikuwa rahisi Fereji na Raza kudanganya wadau wa soka kwa vile, katika kipindi kile cha kampeni za urais wa FIFA, Rais wa zamani wa FIFA, Joao Havelange alitua Afrika Mashariki na “pipi ya kuipa uanachama Zanzibar” ili wapigakura wote wa nchi za Baraza la Michezo Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) wamchague Sepp Blatter.

Kwa mara ya kwanza, Havelange aliwafanyia mipango Fereji na Raza kwenda Paris, Ufaransa ulikofanyika mkutano mkuu wa uchaguzi na fainali za Kombe la Dunia.

Hawakuingia kwenye mkutano ule kama walivyodhani, lakini walifanikiwa kuonana na baadhi ya viongozi wakuu na wakawajengea matumaini hewa.

Waliambiwa wasubiri marekebisho ya katiba ya FIFA yaliopangwa kufanyika Qatar. Walichoambulia ni ZFA kuruhusiwa kushiriki mashindano ya ngazi ya klabu kwa kanda ya Afrika.

Kikwazo cha FIFA kwa Zanzibar ni ibara inayotaka mwanachama awe nchi moja iliyohuru. Zanzibar ni nchi huru lakini kimataifa inayofahamika ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na miaka yote kizingiti ni hicho.

Kuanzia mwaka 2005 ZFA iliongezewa nguvu baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuunga mkono haki ya Zanzibar kuwa mwanachama pia wa FIFA.

Viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), serikali ya Muungano pamoja na mabaraza ya michezo ya Zanzibar na Bara yaliongeza nguvu katika kampeni hizo. Jibu la FIFA lilibaki palepale.

Mwaka jana aliyekuwa Naibu Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamhuna aliwajengea matumaini makubwa zaidi wapenzi wa soka wa Zanzibar aliporejea kutoka Uswisi akidai wamefungua rasmi jalada la kuomba uanachama.

Shamhuna alidai kwamba Rais wa FIFA, Sepp Blatter aliahidi kulishughulikia suala hilo baada ya kusikiliza hoja nzito.

Hoja mojawapo ni kwamba kuna nchi nyingine ndogo kuliko Zanzibar na si wanachama wa Umoja wa Mataifa zimepata uanachama wa FIFA.

Shamhuna alidhani kutokuwa mwanachama wa UN ni kigezo tosha cha kupewa uanachama FIFA. Vilevile atakuwa alitumia mfano wa nchi nne za Uingereza—England, Wales, Scotland na Ireland Kaskazini ambazo kila moja ni mwanachama wa FIFA—kuwa kigezo cha Zanzibar pia kupewa uanachama.

Hoja hizo zimetumiwa kuanzia miaka ya 1970 hadi sasa bado hakijaeleweka.

Mara baada ya Fereji kushinda katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, aliibuka na hoja ya Zanzibar kujiunga FIFA. Kwa miaka 20 Fereji amekwama katika kizingiti kilekile, atakuwa na miujiza gani miaka minne ijayo?

Fereji anakuja na mikakati gani mipya ya kushawishi FIFA ikubaliane na ombi lao, maana kama ni projo Wazanzibari wamezisikia sana.

Fereji afafanue namna atakavyoruka vifungu vya ibara ya 10 kuhusu masharti ya uanachama.

Ibara hiyo yenye vipengele nane inasema;

 1. chama chochote cha soka ambacho kinaandaa na kusimamia soka katika nchi yake kinaweza kuwa Mwanachama wa FIFA. Kwa tafsiri neno “nchi” hapa litakuwa na maana taifa huru ambalo linatambuliwa kimataifa. Bila kuathiri kifungu cha 5 na 6 hapa nchini chama kimoja tu ndicho kitatambuliwa katika kila nchi.
 2. Uanachama utaruhusiwa ikiwa chama kinachoomba kimekubaliwa kwanza kuwa mwanachama wa muda wa shirikisho la soka la bara (hapa ni CAF) angalau kwa miaka miwili.
 3. Chama chochote kinachoomba uanachama wa FIFA kitapaswa kuiandikia sekretarieti kuu ya FIFA.
 4. Chama kitume maombi kikiambatanisha na Katiba ambayo itakuwa na vipengele vifuatavyo:
  1. kutii wakati wote Katiba, Kanuni na maamuzi ya FIFA na mashirikisho yake;

  2. kuzitii Sheria za Mchezo;

  3. kutambua Mahakama ya Usuluhishi wa Migogoro ya Michezo kama ilivyofafanuliwa katika sehemu ya II. Uanachama 11

 5. Kila chama cha soka katika nchi nne zinazounda Uingereza kitatambuliwa kuwa Mwanachama wa FIFA.
 6. Chama cha soka katika nchi ambayo haijapata uhuru kinaweza, kwa idhini ya chama katika nchi iliyohuru, pia kinaweza kupewa uanachama wa FIFA.

  Viongozi wote wanaosema wanaongeza nguvu na kasi kuhakikisha ZFA inakuwa mwanachama wa FIFA waeleze namna watakavyokwepa kizingiti cha ibara hiyo; vinginevyo utakuwa ubabaishaji.

0
No votes yet