Maswali muhimu kwa Jeshi la Wananchi


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 23 February 2011

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli
Jenerali Mwamunyange

NILIPOKUWA katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)—kwa mujibu—mwanzoni mwa miaka ya 1980, kuna mambo kadhaa niliyojifunza.

Nilianzia ukuruta kambi la Oljoro mkoani Arusha na nikamalizia mafunzo kama service man katika kambi ya Makuyuni iliyoko mkoani Manyara. Nidhamu lilikuwa somo kuu.

Bado nawakumbuka maafande waliotufundisha MM (Mbinu za Medani) na MK (Mbinu za Kivita) pamoja na shabaha. Mkuu wa kambi ya Oljoro alikuwa Kanali Khamsini na Makuyuni alikuwa Meja Mpakani. Kazi zilifanywa kwa zamu.

Kila siku ilikuwepo kambi ya zamu ambayo iliwajibika kwa shughuli za ulinzi, usafi wa mazingira na kupika.

Wakati tunafundishwa MM, afande Kajoro alikuwa anasema kambi lazima iwe na ulinzi wa asilimia 25 kila siku.

Kwa sababu ya hofu kwamba adui wa ndani au nje anaweza kuvizia, siku za mapumziko kama Jumamosi na Jumapili au sikukuu ulinzi ulikuwa asilimia 50. Lakini inapothibitika kuna ‘dalili’ za machafuko au ‘hisia’ za uhaini kama mwaka 1983 ulinzi unakuwa asilimia 75.

Pale inapothibitika nchi iko hatarini kama mwaka 1978 majeshi ya nduli Iddi Amini wa Uganda yalipovamia Kagera, ulinzi katika kambi zake unakuwa asilimia 100 huku askari wengine wakiwa vitani. Kambi hulindwa na wanajeshi.

Lakini, wiki iliyopita, mkuu wa usalama na utambuzi kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania, Brigedia Jenerali Paul Mella alikaririwa na vyombo vya habari akisema wakati milipuko inatokea Februari 16, 2011 kwenye maghala ya silaha kambi ya Gongo la Mboto, Dar es Salaam kikosi kilibakiwa na walinzi tu.

Brigedia Jenerali Mella alisema siku ile ilikuwa sikukuu, wanajeshi wote walikuwa kwenye mapumziko. Maelezo haya yanazua maswali.

Maswali

Nakiri kwamba sikuhudhuria mkutano wa wahariri na Brgedia Jenerali Mella pamoja na mwenzake Brigedia Jenerali Leonard Mndeme. Lakini kama walikaririwa sahihi, kuna tatizo.

Kwa nini kambi haikuwa na ulinzi wa kutosha siku hiyo ya tukio la milipuko?

Kwa kawaida, askari hutakiwa kuwa amerudi kambini ifikapo saa 12.00 jioni na huwepo gwaride kwa ajili ya kuita majina (roll call). Kwa nini hawa wa Gongo la Mboto walikuwa mitaani hadi saa 2.20 ilipoanza milipuko?

Brigedia Jenerali Mella anasema baada ya walinzi wale kutimua mbio, walitoa taarifa kwa wakubwa wao na yeye alifika kushiriki kuzima moto. Kambi ipi, maana kama ni ya Gongo la Mboto askari walioko kambini (mabechela) walijiokoa kwa kutambaa hadi barabarani na kutoweka, na waliokwenda kuamuru wakimbie pia walitambaa.

Brigedia Jenerali Mella alishiriki kuzima moto upi katika mazingira hatari kama hayo?

Maelezo ya Brigedia Jenerali Mella yanalazimisha watu waamini kwamba askari walijua kitakachotokea ndiyo maana wote walikuwa nje ya kambi hiyo hadi saa 2.00 usiku.

Vilevile maelezo hayo yanalazimisha watu kuamini askari walikuwa wanajua ndiyo maana ilipoanza milipuko midogo, wake na familia za askari waliooa walipewa taarifa waondoke kambini haraka.

Hiyo ndiyo sababu hakuna mwanafamilia wa askari aliyejeruhiwa au kufa kama ilivyokuwa milipuko ya kambi ya Mbagala.

Milipuko duniani

Brigedia Jenerali Mndeme amesema kwamba matukio ya milipuko ya mabomu ni kawaida katika nchi nyingi na akataja baadhi kuwa ni Msumbiji na Nigeria.

Hivi Mndeme anataka Watanzania wasishtuke eti kwa sababu kuna wanajeshi wengine wazembe kama wao nchi za nje? Hivi kusema hata maghala ya Msumbiji yalilipuka ni utetezi?

Katika baadhi ya nchi huwa kuna hujuma. Mathalani Desemba 31, 2010 kikundi cha Boko Haram kililipua bomu katika mji wa Jos, Nigeria lililoua watu 31; Desemba 30, 2010 bomu lililipuka nje ya mahakama kuu Athens, Ugiriki, mlipuko wa Mumbai, India na mengine mengi.

Mifano mingine ni maafa makubwa yaliyotokea baada ya mtambo wa nyuklia Chernobyl kuvuja na kusambaza miali hatari katika Ukraine (Soviet) Aprili 26, 1986.

Kwa Soviet hiyo haikuwa mara ya kwanza. Maafa ya kwanza yalitokea katika mtambo wa nyuklia wa Mayak Septemba 29, 1957; Uingereza ilikumbwa na maafa katika Winscale Fire, Oktoba 10, 1957; Marekani ilitokea katika Three Mile Island Machi 28, 1978 na Japan ilikumbwa na maafa Tokaimura, Septemba 30, 1999.

Nigeria ilikumbwa na mlipuko mkubwa baada ya ghala la silaha kushika moto Januari 27, 2002. Ndugu na jamaa wengi wa askari walifariki dunia na wakazi wa maeneo ya jirani na kambi ya Ikeja, Lagos; na Maputo, Msumbiji ilitokea Machi 22, 2007 katika kambi ya jeshi karibu na uwanja wa kimataifa wa ndege.

Je, Brigedia Jenerali Mndeme yuko radhi kufananisha sababu za hujuma katika kambi au milipuko hiyo na iliyotokea Gongo la Mboto?

Sababu za milipuko

Hata kabla ya serikali kuunda Tume ya Uchunguzi wa milipuko ya Gongo la Mboto, Mnadhimu Mkuu wa JW, Meja Jenerali Abdurahman Shimbo ametaka wananchi wasifananishe sababu za milipuko ya maghala ya silaha katika kambi ya Gongo la Mboto na ya Mbagala kwani ni tofauti.

Kauli Meja Jenerali Shimbo inathibitisha kwamba jeshi linajua sababu za milipuko hii. Ni hujuma? Kwa nini hata kabla ya tume kuundwa tayari jeshi linajua sababu? Tume hiyo, itatoa majibu gami taofauti na haya wakati watakaoulizwa na tume ni wanajeshi hao hao?

Je, ndiyo sababu walikuwepo ‘walinzi’ tu kambini kama alivyokaririwa Brigedia Jenarali Mella?

Jenerali Davis Mwamunyange, mkuu wa majeshi nchini, katika taarifa yake kwa Waziri mkuu, Mizengo Pinda amesema wataanzisha utaratibu wa kuwapatia mafunzo wananchi wanaoishi kando ya kambi hizo ili ikitokea milipuko wajue namna ya kujihami.

Sawa, lakini baada ya maghala ya Mbagala kulipuka mwaka 2009 ilielezwa kwamba maghala mengi ya silaha hata Gongo la Mboto yana silaha kuukuu, zilizochoka na zilikuwa zinatakiwa kuharibiwa.

Zingeharibiwa silaha hizi, jeshi si lingekuwa limeokoa uhai wa watu?

Kwa nini, hakuna juhudi zozote zilizochukuliwa tangu mabomu yalipolipuka Gongo la Mboto kwa mara ya kwanza mwaka 2004?

Japokuwa Jenerali Mwamunyange amekumbuka shuka wakati kumeshakucha, ushauri wake ni mzuri ufanyiwe kazi kuepusha maafa siku zijazo.

<p> 0776 383 979</p>
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: