Matola: Kisago cha Yanga mazoezi kwa Waarabu


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 21 April 2010

Printer-friendly version

KISAGO cha mabao 4-3 ilichotoa Simba kwa watani wao wa jadi katika soka, Yanga ni kipimo tosha juu ya uwezo wa timu hiyo ya Msimbazi kabla ya kuumana na Haras El Hadood ya Misri katika Kombe la CAF.

Simba inatarajiwa kuumana na miamba hao wa Misri Jumapili ijayo katika mchezo wa kwanza wa raundi ya pili kwenye uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Miamba hiyo ya Ligi Kuu ya Bara, Simba ilifikia hatua hiyo baada ya kuikandamiza Lenghtens ya Zimbabwe kwa jumla ya mabao 5-1; ilishinda 3-0 Harare na ikaichapa 2-1 Dar es Salaam.

Matokeo hayo yameiweka Simba mahali pazuri na imepata mazoezi ya kutosha katika mechi za Ligi Kuu ambazo imecheza 21 bila kupoteza hata moja. Jumapili ilitandika Yanga kwa mabao 4-3 na leo inafunga pazi kwa kumenyana na Mtibwa Sugar.

Mwenendo wa timu hiyo na hasa matokeo mazuri dhidi ya Yanga yamewapa ari kubwa Simba katika kipindi hiki na kaimu kocha mkuu, Selemani Matola, anasema ameiongoza timu yake kuitandika Yanga lakii kocha Patrick Phiri ataiongoza katika mechi dhidi ya Hadood.

Matola amesema “Phiri hajaitosa” klabu hiyo ya Msimbazi kama inavyodaiwa na wadau kadhaa wa soka bali ana matatizo na anatarajiwa kurejea kuiandaa timu katika mechi ya Kombe la CAF.

“Phiri ana matatizo ya kifamilia na kama yatapungua, anaweza kutua Dar es Salaam, wiki hii,” anasema Matola, nahodha wa zamani wa timu hiyo yenye mafanikio.

Matola alikuwa akiweka mambo sawa baada ya kutolewa madai tofauti kuhusu sababu za msingi za kuondoka kwa Phiri. Baadhi wanadai aliomba nafasi ya kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Zambia na wengine wanadai anauguliwa na mwanawe wa kiume.

Mwandishi: Niambie ukweli kuhusu Phiri, anarudi au hapana?
Matola: Kaka, mengi yanasemwa na kuandikwa juu yake, lakini ngoja nikwambie ukweli. Phiri anauguliwa na mwanaye.

Unajua ilikuwaje, yule dogo anapiga kinywaji, sasa akawa na malaria akapiga dozi freshi. Sasa kabla ya dozi haijapoa, akapiga tena mtungi (pombe), akapoa yaani ikamsumbua kinoma (sana).
Ikabidi familia imjulishe kocha aende. Kwa kuwa kila kitu kilikuwa safi hapa, anaanza na kutuachia jukumu.

Mwandishi: Vipi kuhusu madai kwamba Phiri ameomba kuifundisha Chipolopolo?
Matola: Ninachofahamu mimi, hapo Chipolopolo (timu ya taifa ya soka ya Zambia) imepata kocha ni yule wa ZANACO- Wedson Nyirenda. Kwa hiyo kocha anarudi wakati wowote mambo yakiwa safi kwao.

Mwandishi: Vipi kuhusu wapinzani wenu Haras Al Hadood?
Matola: Tunawajua Waarabu, hatuna shaka nao, ni kama mbwa ukimjua jina haweza kuwa mkorofi. Kwa hiyo, maandalizi ni mazuri na tusubiri siku ya mechi wiki ijayo.

Mwandishi: Mbona hukukaa kwenye benchi kama ilivyotangazwa?
Matola: Kweli nakaimu nafasi ya Phiri, lakini Yanga mchana wa leo (Jumapili iliyopita) waliweka pingamizi. Viongozi wakasema basi haina shaka. Ndio sababu ya kukaa mbali ya benchi. Pale nilipokaa nilikuwa na simu yenye fedha za kutosha, hivyo nilikuwa nawasiliana na wenzangu cha kufanya.

Aidha kocha msaidizi, Amri Said amesema Phiri tayari ametuma programu ya mazoezi ya wiki moja kwa ajili ya mechi dhidi ya Hadood ambayo katikati inaingliana na mechi ya mwisho leo dhidi ya Mtibwa Sugar.

“Nimekuwa nikiwasiliana na kocha kila siku asubuhi na jioni. Hajaniambia anakuja lini, lakini amenitumia programu ya wiki hii kabla ya kuivaa timu ya Misri,” anasema Said maarufu kama Jaap Stam.

Simba, timu pekee ya Tanzania iliyosalia katika michuano ya kimataifa, ndiyo pekee inajua ujanja wa timu za Kiarabu.

Majigambo ya Matola yanatokana na mafanikio ya Simba dhidi ya timu hizo za Kiarabu.

Mwaka 1974 iliwahi kuitandika Mehla El Kubra bao 1-0 Dar es Salaam kabla ya timu hiyo kupata ushindi kama huo katika mechi ya marudiano hatua ya nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika.

Mwaka 1993 Simba iliipa kisago cha mabao 3-0 El Harrach ya Algeria jijini Dar es Salaam kabla ya timu hiyo kujikakamua kushinda kwa mabao 2-0 jijini Algiers. Ilikuwa michuano ya Kombe la CAF.

Mwaka 2003 ilikata tiketi ya kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuitoa kwa mikwaju ya penalty Zamalek ya Misri. Timu hizo zilifikia hatua hiyo baada ya Simba kushinda 1-0 Dar es Salaam na Waarabu hao kushinda pia 1-0 Cairo.

Pia Simba imewahi kuitambia Ismailia kwenye uwanja wa Uhuru japo Waarabu hao walisonga mbele kutokana na wingi wa mabao ya nyumbani.

Kwa hiyo, ushindi wa mabao 4-3 na uelewano mzuri ulioiwezesha kumaliza ligi bila kufungwa unatarajiwa kutumika kama kimbunga cha kuizoa Hadood.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: