Matukio ya vurugu Simba, Yanga


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 16 May 2012

Printer-friendly version

MASHABIKI wa soka duniani kote huwa wastaarabu sana pale klabu wanazoshabikia zinaposhinda. Lakini kinyume cha hapo sekeseke hutokea.

Ulaya, kwa vile klabu humilikiwa na watu binafsi wenye uwezo au matajiri au kampuni, kocha ndiye husulubiwa kwanza kisha wasaidizi wake.

Kocha mkuu akitimuliwa kazi, msaidizi wake huchukua majukumu kwa muda wakati wamiliki wanatafuta mrithi wake.

Wamiliki wa klabu hufanya hivyo kwa sababu, kocha mkuu (meneja) hupewa fedha za kusajili wachezaji bora kutoka kokote duniani, hivyo klabu inapofanya vibaya, huona uchungu kwamba fedha zao zimepotea bure.

Manchester United na Arsenal zote za England ndizo pekee zimekaa na makocha kwa muda mrefu na sababu ziko wazi. Sir Alex Ferguson amekaa muda mrefu kwa vile anaipa mataji Man United wakati Arsene Wenger, japo hajaipa mataji Arsenal kwa muda mrefu, hajaipa hasara katika uendeshaji.

Wenger anasifiwa na kutolewa mfano hata na Fifa kwa kusajili vijana wasio na majina kuwanoa hadi wanakuwa hatari kisha huwauza kwa bei mbaya. Kila linapotokea shinikizo la mashabiki aondoke, wamiliki wa klabu hiyo wamekuwa wakizingatia faida ya kifedha na siyo faida ya kisoka.

Klabu nyingine zote hazina uvumilivu kuanzia Chelsea ya England hadi Real Madrid ya Hispania.

Barani Afrika na kwa mada hii hasa Tanzania ni tofauti. Kwanza klabu nyingi humilikiwa na wanachama wengi, na pili viongozi ni wa kuchaguliwa si kutokana na wingi wa hisa.

Tarimba Abbas, alipopigia debe mfumo wa kampuni katika klabu ya Yanga, alikuwa anataka wanachama wenye michango mikubwa ya kuanzia Sh. 100,000 ndio wawe na sauti ya mwisho. Alifanikiwa siku za mwanzo, lakini baadaye alipingwa.

Kwa vile, viongozi huchaguliwa na kupewa dhamana kwa muda ule uliotajwa katika katiba, klabu ikifanya vibaya, lawama zote humwangukia kiongozi na haraka wanachama hushinikiza aondoke.

Viongozi kama hayati Rashid Ngozoma Matunda, Jabir Katundu waliwahi kuonja ‘joto ya jiwe’ katika uongozi wao kwenye klabu ya Yanga. Wanachama waliwahi kwenda kumfanyia fujo hata mfadhili Murtza Dewji mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Lakini viongozi wa Simba wanajua vizuri ghadhabu ya wanachama. Wanachama waliwahi kuvamia nyumbani kwa aliyekuwa mwenyekiti wao Juma Salum wakafanya fujo na wakachoma uzio.

Kiongozi wa hivi karibuni anayeweza kueleza adha ya wanachama katika klabu hiyo ya Msimbazi ni Hassan Dalali. Alipogoma shinikizo la kujiuzulu, wanachama walipiga kambi nyumbani, wakamkoromea mkewe na wakaacha lundo la kinyesi. Dalali alijiuzulu.

Hii ndiyo sababu, wadau wa soka wanapotazama hali ya hewa katika klabu ya Yanga; wanaojua vurugu tangu miaka ya 1970, wanamshauri mwenyekiti wao Llyold Nchunga ajizulu.

Wadau wanaomshauri hivyo wanampenda wanamtakia amani na afya njema. Nchunga ana hiari ya kukubali au kukataa; ana hiari ya kupima nguvu za wanachama au la.

Mwaka 2008 Yanga wakiwa wamemchoka mwenyekiti wao Imani Madega ‘walimpindua’ katika mkutano uliofanyika katika Bwalo la Polisi, Oysterbay.

Lakini kwa vile Katiba ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) inakataza viongozi wanaoingia kwa mapinduzi, haraka alirejeshewa uongozi wake hadi ulipofanyika uchaguzi mkuu mwaka 2010 uliomwingiza Nchunga.

Wanachama walioshinikiza Madega aondoke ndio hao hao wanaotaka kiti cha Nchunga ili apewe mwingine; uongozi mzima ukijiuzulu utakuwa umetimiza utaratibu wa kikatiba hivyo Yanga watakuwa huru kuchagua viongozi wengine.

Narudia, makocha ndio wanaoadhibiwa katika klabu za Ulaya kutokana na matokeo mabaya ya uwanjani lakini Afrika na hasa Tanzania huwa viongozi.

Simba ilipokuwa na matokeo mabaya msimu uliopita, uongozi ulifanya juhudi za haraka kubadili makocha ili kuonyesha wamejua udhaifu ulipo. Uongozi wa Yanga ulifanya hivyo msimu huo ukaondoa ‘bakora ukaweka fimbo’.

Japokuwa wanachama huchukizwa na matokeo mabaya ya uwanjani, matajiri wanaozifadhili Simba na Yanga ndio huwa nyuma ya vurugu na mapinduzi.

Wafadhili waliochukizwa na msimamo wa kiuongozi wa George Mpondela “Castro” mwaka 1994 waligoma kutoa fedha ili Yanga iende Afrika Kusini kuumana na Moroca Swallows.

Hali ilipokuwa ngumu Mpondela alitafuta pa kutokea. Akajitoa Yanga, akaingia katika siasa, akapotelea huko.

Matajiri ndio wanapanga safu, wanachama wanatia tu muhuri.

Nani amesahau wafadhili walipogoma kutoa fedha za kumlipa kocha na nauli ya kupeleka timu DR Congo kwa mechi za kimataifa?

Nani amesahau Kostadin Papic alivyokosa msaada siku za mwisho za maandalizi muhimu ya timu kwa mechi za kimataifa hadi akaamua kuondoka?

Nani hajasikia nyimbo na maombi ya wanachama vijana wa klabu hiyo? Vijana wanatema cheche na ndimi za wazee ni moto kwa sababu nyuma yao kuna matajiri wanaotaka kubadili safu. Matukio haya ya vurugu yampe busara Nchunga kujali usalama wake.

0789 383 979
0
No votes yet