Mauaji haya yakomeshwe


editor's picture

Na editor - Imechapwa 30 June 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

SERIKALI haina budi kusitisha mauaji yanayoendelea hivi sasa katika Wilaya ya Tarime, mkoani Mara. Hatukubali kurejea kwenye ushenzi.

Wananchi – tena wajomba – wanauana, wanachomeana nyumba na kuangamiza mali. Sababu zinazotolewa ni kwamba wameibiana mifugo – ng’ombe.

Zaidi ya watu 40 wanasadikiwa kuuawa. Huu ni ushenzi katikati ya ustaarabu.

Taarifa nyingine zinasema kuwa idadi ya waliofariki inaweza kuwa kubwa zaidi kwa vile kuna desturi za kuzika haraka na kimyakimya.

Kuna madai kuwa ushindani wa asili kati ya Wakurya na Wajaluo unafanya Wakurya wazikane kimyakimya na kwa haraka kuficha fedheha ya kuuawa na Wajaluo.

Hii siyo mara ya kwanza kwa mapigano kama haya kutokea. Yamekuwa yakitokea kwa kipindi kirefu hata kama hayakushirikisha idadi kubwa ya koo na hata kusababisha vifo vingi mara moja.

Wizi wa mifugo ni dondandugu katika koo hizi. Wanaoiba wanaweza kufahamika na walioibiwa wanaweza kujulikana tu bila kazi ngumu.

Wizi wa mifugo ulikuwa sehemu ya maisha wilayani Serengeti. Serikali ilijipanga kuanzia ngazi ya kijiji, kata hadi wilaya. Uchunguzi ulifanywa.

Kilichofuatia uchunguzi ni kupelekwa kwa askari kwenye maeneo husika. Waliwasaka watuhumiwa wote. Wezi walitajwa. Walikamatwa. Mifugo ilirejeshwa na mfumo wa kudhibiti wizi ukawekwa.

Kinachoendelea hivi sasa basi, siyo kigeni katika mazingira ya mkoa wa Mara. Uzoefu wa kukabiliana nacho upo. Watawala wa kata na wilaya walioshiriki kumaliza mgogoro wa Serengeti na maeneo mengine bado wapo.

Ni uzembe usioweza kusameheka kwa watawala wilayani, na hasa jeshi la polisi, kushindwa kuandaa mpango maalum wa kuchunguza wizi, kukamata wahusika na kuzima mauaji ya kikatili.

Tunasema katika mazingira ya vijiji, wanaofuga wanafahamika. Wanaochunga mifugo ya wengine wanafahamika pia.

Wenye mifugo mingi wanafahamika kwa karibu kila mmoja na wenye hata ng’ombe mmoja na mbuzi wawili wanajulikana kwa majirani zao.

Haya ni mazingira mwanana ya kuwezesha jamii nzima kushiriki kutambua nani ana nini, tangu lini na kutoka wapi. Ni rahisi kabisa kutambua nani katajirika usiku mmoja kwa kutoka kumiliki ng’ombe mmoja hadi 20 au 50 au 100.

Polisi wanashindwa vipi kufanya kazi hapa? Mkuu wa wilaya anashindwaje wakati kuna pa kuanzia? Wasiotaka kufanya kazi ya kulinda uhai wa wananchi na mali zao wanatafuta nini ofisini?

0
No votes yet