Mawaziri 13 kutupwa nje


Jacob Daffi's picture

Na Jacob Daffi - Imechapwa 15 February 2012

Printer-friendly version

RAIS Jakaya Kikwete aweza kufanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri wakati wowote sasa, imefahamika.

Taarifa kutoka ndani ya serikali zinasema mabadiliko ya baraza hilo yatafuatia kinachoelezwa kuwa ni “kuyumba kwa serikali.”

Mtoa taarifa anasema hatua ya kufanya mabadiliko makubwa au hata kuvunja baraza la mawaziri, inatokana hasa na serikali kushutumiwa mara kwa mara na wananchi kwa kutoonyesha kuwajibika.

Mambo ambayo yanatajwa kuyumbisha serikali hivi sasa ni pamoja na migomo na maandamano ya kupinga unyimaji haki na stahiki nyingine.

Mgomo wa madaktari uliochukua wiki tatu na kugharimu maisha ya wananchi, huku watendaji na wanasiasa wakiendeleza malumbano, ni moja ya sababu zinazotajwa.

Migomo ya wanafunzi wa vyuo vikuu ambayo imeendelea bila ukomo na shinikizo mbalimbali kutoka kwa wapigania haki za binadamu, ni miongoni mwa mambo yanayohitaji “ubongo mpya,” ameeleza mtoa taarifa ndani ya serikali.

MwanaHALISI limeelezwa kuwa baraza la mawaziri linaweza kufanyiwa marekebisho au kuvunjwa na kuundwa upya kwa “lengo la kurejesha hadhi, ufanisi na uwajibikaji serikalini.”

Jingine ambalo linatajwa kuchangia kuwepo uwezekano wa kufanya mabadiliko, ni baadhi ya wizara kuwa na mawaziri ambao hawana afya nzuri na wanahitaji kupewa muda wa kujihudumia.

Mahali pengine ni kule ambako mawaziri waliopo, ama wanapwaya kiutendaji kwa kutochukua hatua pale panapohusika, au wamejichimbia katika shughuli za binafsi kuliko za serikali.

“Mnaadika kila siku kuwa Rais Kikwete ni dhaifu; lakini usisahau kuwa udhaifu wa rais si wake binafsi.

Kwa hiyo akitaka kuuondoa sharti wengine waguswe; kama mawaziri na makatibu wakuu,” ameeleza mtoa taarifa serikalini.

Mabadiliko katika baraza la mawaziri yanaweza kwenda sambamba na mabadiliko katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo yalipitishwa na Halmashauri Kuu ya taifa wiki iliyopita.

Kwa mujibu wa katiba, Rais Kikwete amebakiwa na miaka minne ya ngwe yake ya pili ya utawala.

Baadhi ya wanaotarajiwa kukumbwa na mabadiliko hayo, ni Waziri wa Afya, Dk. Haji Mponda na naibu waziri, Dk. Lucy Nkya ambao wanadaiwa “kulea” mgomo wa madaktari hadi baadhi ya wananchi kupoteza maisha kwa kukosa tiba.

Madaktari wanafunzi wapatao 100 walikomalia wizara kuwalipa posho zao ili wapate nauli, chakula na kugharamia makazi yao, lakini wizara ikabakia “njoo kesho” na bila maelezo mwanana.

Kimya cha wahusika kilichofuatiwa na vitisho vya wizara, kilichochea madaktari wenzao kuunga mkono mgomo wa madaktari wanafunzi.

Ukaidi wa wahusika na hatimaye vitisho vya waziri mkuu, kulifanya madaktari bingwa kujiunga na wenzao na kudai, siyo posho tu za Sh. 10,000 na 20,000, bali sasa mishahara yao na nyongeza.

Kushindwa kumaliza mgomo ambao ungesitishwa katika hatua ya awali, kumeleta “jina baya kwa serikali, vifo kwa wananchi, ukosefu wa imani ya madaktari kwa serikali na kumeonyesha uzembe usiomithilika,” ameeleza mtoa taarifa.

“Katika mazingira haya, hata Waziri Mkuu Mizengo Pinda aweza kung’olewa kwa kuwa yote yalifanyika mbele yake; yalifanywa na mawaziri chini yake; na yeye alichochea hasira, ghadhabu na chuki ya madaktari kwa serikali pale alipowakemea huku wakidai stahiki sahihi,” ameeleza mtoa taarifa.

Naye Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja anaweza kuwekwa kando kutokana na kuandamwa na tuhuma kupitia bungeni ambazo zimekuwa ngumu kuzima.

Ngeleja, pamoja na kutuhumiwa kukusanya na kutumia mamilioni ya shilingi kwa kushirikiana na katibu mkuu wake, David Jairo isivyo halali, wizara yake imekuwa goigoi katika kumaliza tatizo la nishati ya umeme nchini.

Ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma iliyokuwa ikimkabili Jairo, imeonyesha jinsi Ngeleja na naibu wake, Adam Malima, walivyolipwa kiasi kikubwa cha fedha katika mazingira yenye mashaka.

Wengine wanaotajwa kuwa kwenye mkumbo wa kuwekwa kando ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Mark Mwandosya, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyrill Chami, na naibu waziri wa ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe.

Mawaziri hawa wamekuwa wakihudhuria matibabu nchi za nje kwa kipindi kirefu sasa na mtoa taarifa ndani ya serikali anasema “…siyo busara kuendelea kuwaweka ofisini wakati utendaji wao ni mdogo.”

Prof. Mwandosya na Dk. Mwakyembe wamekuwa wakipata matibabu nchini India kwa kipindi kirefu. Naye Dk. Chami ameanza matibabu nchini humo.

Mawaziri wengine ambao wanatajwa kuachwa iwapo rais atafanya mabadiliko makubwa ni Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani, waziri wa maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto, Sophia Simba na waziri wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta.

Kombani, Simba na Sitta wanaelezwa kuwa “hawaisaidii serikali.” Mtoa taarifa hakueleza jinsi gani mawaziri hawa hawaisidii serikali, isipokuwa alisema “rais mwenyewe anajua.”

Mwingine anayeweza “kwenda na maji” ni waziri wa utawala bora, Mathias Chikawe. Hajajibu tuhuma za kujihusisha katika miradi binafsi kwa mgongo wa serikali.

Mradi ambao unadaiwa kuwa mbioni kufanikishwa na Chikawe, ni biashara kubwa ya dawa za virutubishovya binadamu kwa wenyevirusi vya ukimwi iitwayo Secoment V.

Naye Malima, hajajibu tuhuma zinazomkabili za kutaka kuingiza nchi kwenye mkataba tata wa uchimbaji madini ya shaba wilayani Mpanda, mkoa wa Rukwa.

Mtoa taarifa anasema ni rais mwenyewe anayejua “nani hamfai hapa au pale, lakini watang’oka wengi ili kupata timu ya kumfikisha mwishoni mwa ngwe yake – 2015.”

“Mabadiliko hayo yanatarajiwa kufanyika kabla ya kumalizika mwezi au kama yamechelewa sana, itakuwa mwanzoni mwa Machi,” ameeleza mtoa taarifa.

Amesema, “Rais anahitaji timu mpya itakayokuwa na upya wa mawazo na msukumo katika kuleta mabadiliko haraka.”

“Hili jambo limekuwa likisemwa… hata baadhi ya viongozi, marafiki wa rais na wale wanaomtakia mema yeye na serikali yake, wamekuwa wakimshauri kuchukua uamuzi huo.

Sasa wakati umefika wa kufanya hivyo,” ameeleza waziri mwandamizi ndani ya serikali.

Baadhi ya wanasiasa wametajwa kuwa huenda wakachukua nafasi zitakazoachwa wazi.

Miongoni mwa wanaotajwa ni Prof. David Mwakyusa, mbunge wa Rungwe Magharibi, na mbunge wa

Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi. Hii itakuwa kurejesha uwiano wa viongozi ikiwa Rais Kikwete atampumzisha Prof. Mwandosya na, au Dk. Mwakyembe.

0
No votes yet