Mawaziri hawa wa Afya waondoke


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 07 March 2012

Printer-friendly version

NATARAJI wakati makala hii inasomwa, Rais Jakaya Kikwete atakuwa amefanikiwa au bado anahaha kupata waziri, naibu waziri na maofisa wengine wa wizara ya afya.

Wale wa awali watakuwa ama wamepelekwa likizo, wameshauriwa kufunga virago na kuondoka au wamejiondoa kimyakimya au waziwazi ili kuepusha janga.

Lakini katika mazingira ya utawala wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inawezekana viongozi wakawa bado wanafanya ajizi – kama kawaida yao.

Ikitokea wakapuuza tishio la madaktari la “kugoma kwa kishindo” – mgomo mzito na usiokoma nchi nzima – kuanzia leo, Jumatano; na madaktari wakakataa kukunjika; basi tutarajie maafa.

Watoto, vijana, watu wa makamo na vikongwe, watapukutika – watakufa, watazikwa, hawatafufuka siku ya tatu wala ya sita. Basi!

Bali vikongwe, watu wa makamo, vijana na watoto wa watawala na ndugu zao, watatibiwa “praiveti” au katika hospitali za nje ya nchi – India, Uingereza, Ujerumani…

Kufa – kila mmoja atakufa. Lakini mara hii, kama kuna ajizi, watakufa ambao wangepona na labda kuendelea kupumua kwa miaka mitano au 20 au 50 au hata 100.

Kwa zaidi ya wiki mbili sasa kumekuwa na uvumi kwamba waziri wa afya aliishaandika barua ya kujiuzulu, lakini bosi wake akamwambia, “…acha bwana, yataisha hayo.”

Hayaishi. Madaktari wanadai kuwa yale ambayo walikubaliana na waziri mkuu hayawezi kutekelezwa na watu walewale ambao walikuwa wanakataa kuyatekeleza kabla ya mgomo.

Hayaishi. Waziri na naibu wake ndio walikataa au walipuuzia au walishindwa kutoa malipo – posho ya kujikimu kwa madaktari wanafunzi. Sasa ama hawawezi kusimamia, au watahujumu mwafaka.

Hayaishi. Ni chini ya waziri na naibu wake, mgomo uliachwa kupanuka na kuhusisha madaktari katika hospitali za serikali jijini Dar es Salaam na nchini kote. Waliendelea kujifanya hamnazo!

Hayaishi. Ni waziri na naibu wake waliokataa, waliopuuza au walioshindwa kusitisha moto kabla haujaongezewa petroli kwa kuungwa mkono na chama cha madaktari na baadaye kuungwa mkono na mabingwa katika taaluma hii.

Katika mazingira ya kawaida, waziri Haji Mponda na naibu wake Lucy Nkya, hawakustahili kuwa ofisini pale wizara ya afya hasa baada ya kuona katibu mkuu na mganga mkuu wakiwekwa kando.

Jeuri ya kubaki ofisini haina uhusiano wowote na jeuri ya kuchapa kazi. Ukweli ni kwamba hawawezi kufanya lolote katika mazingira haya. Hii ndiyo maana kuna uvumi kwamba mmoja wao aliambiwa “…acha bwana, yataisha hayo!”

Hebu tuliangalie hivi: Mtu asiyetenda au asiyeonyesha nia ya kutenda ili kumaliza mgogoro uliopo, huwa ni sehemu ya mgogoro.

Mtu ambaye hutenda, kwa nia yote ya kuzamisha upande mwingine katika madai yanayoleta utata kati au baina ya pande husika, naye huwa sehemu ya mgogoro.

Huwezi kusuluhisha mgogoro kati ya wawili au baina ya watatu wakati hujaondoa doa la mmoja wao kuwa sehemu ya mgogoro.

Na inawezekana kabisa, kwamba kwa kutambua, kutenga na, au kuondoa mmoja ambaye ni sehemu ya mgogoro, unaweza kuwa umetatua asilimia 90 ya mgogoro wote.

Katika hili, kuwa na mawaziri ambao watasimamia mwafaka; wakati wao walishindwa kulipa Sh. 10,000 au 20,000 kwa madaktari wanafunzi; ama ni kukejeli madaktari au ni kupoteza muda tu.

Kutarajia kamati ya mwafaka chini ya waziri mkuu, kufanya kazi katika mazingira ambayo bado yanasimamiwa na madaktari wakuu walioleta mazingira ya maafa, ni matusi kwa zoezi zima la kuleta maelewano.

Kutarajia kamati ya mwafaka kufanya kazi chini ya mwavuli mpana ulioshikiliwa na Dk. Mponda na Dk. Nkya – walewale walioshindwa, waliopuuza au waliokataa kuona uhalali wa madai ya madaktari – ni kukataa kukiri maafa yaliyotokea.

Hii pia yaweza kuwa njia ya kudai kuwa maafa yalikuwa madogo na kwamba yangekuwa makubwa zaidi.   

Aidha, kuendelea kuona kuwa mawaziri hawa ndio pekee wenye uwezo wa kuongoza wizara ya afya; na kwamba hakuna mwingine yoyote; ni upofu usiosameheka.

Lakini kuzidi pia kung’ang’ania kuwa wawili hawa hawawezi kuondoka, “…acha bwana, yataisha,” ama ni kukiri ushirikina kwamba “walipatikana kwa dawa” na mpaka zivunde; au ni kufanya urafiki na disraili.

Kwa mujibu wa misingi ya uwajibikaji, kwa mwanasiasa na yeyote aliyeko mwenye mamlaka ya kusimamia wenzake, mawaziri hawa hawapaswi kuwa ofisini.

Madai ya madaktari yanaeleweka. Kwanza, wamenyanyasika mikononi mwa utawala wa wizara.

Kuna waliokosa nauli kwenda mahali pao pa kazi. Kuna waliokosa chakula. Kuna walioshindwa kuhudumia ndugu zao. Kuna walioshindwa kulipa pango na hivyo kutishiwa kufukuzwa au kufukuzwa.

Kuna waliodhalilika mbele ya jamii inayowazunguka kwani hawakutarajiwa kuwa katika hali ya ombaomba. Kuna waliopoteza imani katika serikali kwa kuwa viongozi wa wizara walishindwa, walipuuza au walikataa kuona tatizo.

Kwa kutumia maneno mepesi ya wanasiasa – kwa heshima na taadhima – mawaziri hawa waondoke.

Hata wasipopata kazi nyingine serikalini; bado wanaweza kujiajiri au kuajiriwa pengine. Kilichowaibua kutoka walikokuwa na kuwa mawaziri, kinaweza kuwasukuma kwingine kwenye neema zaidi au “vyovyote itakavyokuwa.”

Busara inaelekeza kuwa bora wawili waondoke. Hili halitakuwa tendo la aibu kwao, wala kukiri kufukuzwa na madaktari.

Hata ingekuwa ni kufukuzwa na madaktari, heri wafukuzwe na wao wafukuzike kuliko maafa makubwa ya vifo vya watoto na wakubwa; wanaume na wanawake.

Tuwatakie safari njema popote waendako.

0
No votes yet