Mawaziri sawa, makatibu wakuu hapana


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 24 November 2010

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

WAKATI ukuta, ukipambana nao utaumia. Uteuzi wa mawaziri alioufanya Rais Dk. Ali Mohamed Shein umejumuisha mawaziri wanane kutoka Chama cha Wananchi (CUF) kuingia katika Baraza la Mapinduzi (BLM), nguzo kubwa ya kuendeleza misingi ya mapinduzi ya 12 Januari 1964.

Kwa upande mwingine, uteuzi huo umeweka zege kwa waliokuwa mawaziri wa Dk. Salmin Amour Juma (Komandoo). Hawa ni watu wa kambi inayodhibiti maskani maarufu ya CCM ya Mwembekisonge.

Ni maskani ambayo ustawi wake hutegemea fedha za juujuu kutoka serikalini. Athari za matumizi yake ni kuendeleza mitizamo ya kihafidhina inayobeza watu na hasa wanasiasa vigogo kutoka Pemba.

Kisonge upo ubao wa matangazo unaojulikana kwa kampeni chafu dhidi ya siasa za maridhiano na umoja wa Wazanzibari. Wabunifu wa maandiko hayo, huangalia hali ya nchi na kuitafsiri kwa kebehi na hata matusi. Kilicho muhimu zaidi kwao ni kufurahisha nafsi zao bila ya kujali kama wamemtusi mtu au jamii.

Mtu aweza kuwa mzuri leo kwao, akabadilishiwa kibao kesho kwa kuandikwa vibaya. Kwa mfano, wakati aliyekuwa rais, Amani Abeid Karume akisisitiza maridhiano, Kisonge wakisema “HAPANA mseto.”

Mpaka dakika ya mwisho, hawakubadilika. Hawakutaka na hawataki umoja unaohimizwa na maafikiano ya kujenga siasa safi. Wanataka utengano uleule wa waliotoka Pemba na wale wa Unguja. Wanasema “Mapinduzi Daima.”

Kweli kabisa. Baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa 2 Novemba, Kisonge waliandika ubaoni: “Kura moja mtu mmoja. Huyo… Ahmada umelewa. Kwisha.”

Akisemwa Karume ambaye alisisitiza katika uchaguzi “mtu mmoja atapiga kura moja.” Kwa sababu mpango huo ulivurugwa makusudi na mtandao wa kihafidhina ukisaidiwa na mashushushu na kuwatumia watendaji wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), historia ya nchi kutokubali mabadiliko ikajirudia.

Wanasema Karume amelewa, mfano wa yule kijana aitwaye Ahmada katika kazi ya sanaa iliyofanywa na Bibi Fatma binti Baraka kwa umaarufu Bi Kidude; msanii gwiji wa taarab asilia ya pwani, mkazi wa Rahaleo, mjini Zanzibar.

Huwezi kuamini, rais aliyeachia ngazi kikatiba na kutandika msingi wa siasa za maridhiano anatukanwa na wana maskani. Anaonekana dalali.

Karume ni shujaa kwelikweli kiuongozi. Mabaya yote yaliyotendwa chini yake, yamezibwa na mwisho wake. Amebadilisha desturi za watawala wengi Afrika kuanza vizuri wakamalizia vibaya hadi kukataa kuachia madaraka kisheria. Ameotesha mbegu za amani na utulivu wa kweli Zanzibar.

Dk. Shein anaanzia hapo kujenga jamii mpya, yenye masikilizano, upendo na utashi wa maendeleo ya kweli.

Uteuzi wake umezingatia hili. Amewarudisha mawaziri wengi waliofanya kazi na Karume. Amerudisha waliokuwa Serikali ya Muungano wakimsaidia Rais Jakaya Kikwete. Hawa ni Balozi Seif Ali Idi, makamu wa pili wa rais, aliyekuwa naibu waziri katika serikali ya Kikwete.

Amemuita Omar Yussuf Mzee, naibu waziri wa Kikwete aliyejijengea sifa ya utumishi mzuri. Sasa anaongoza wizara ya fedha, uchumi na mipango ya maendeleo.

Mohamed Aboud Mohamed, naibu mwingine wa Kikwete aliyekuwa iliyokuwa wizara ya usalama wa raia chini ya Bakari Harith Mwapachu na baadaye wizara ya Afrika Mashariki. Leo yupo chini ya Makamu wa Pili wa Rais.

Dk. Shein hata hivyo, ameunda serikali kubwa isivyotarajiwa kwa kutazama hali ya uchumi ya Zanzibar. Serikali ya mawaziri 19 wakiwemo watatu wasiokuwa na wizara maalum ni kubwa. Ukijumlisha manaibu waziri sita, tuna serikali ya mawaziri 25.

Baadhi ya wadadisi wanasema baraza jipya la mawaziri linakidhi matakwa ya wakati: kwamba kuwaingiza hata waliotuhumiwa kwa ufisadi na kupinga maridhiano ni changamoto muhimu kwani watalazimika kubadilika na kuthibitishia Wazanzibari kuwa walikosea. Inavumilika.

Kinachofuata ni uteuzi wa makatibu wakuu. Hizi ni nafasi muhimu zinazohitaji viongozi makini.

Mazoea ni kuteua upya waliopo. Nyongeza hutoka kwa wakuu wa idara na taasisi waliokuwa wasaidizi wa makatibu wakuu. Viongozi walio chini yao nao huweza kupandishwa.

Baadhi yao wameanza tambo. Wanatamba kuwa ukaribu wao na Dk. Shein utalipa. Watateuliwa tu. Wale waliopo waweza kuteuliwa upya kama wamefanyakazi kwa uadilifu na wanacho cha kuonyesha.

Tatizo baadhi yao wana madoa. Wana rekodi mbaya kiutumishi. Walipewa dhamana na kuitia aibu serikali mbele ya wananchi na wafadhili.

Walifisidi misaada na hawakuchukuliwa hatua yoyote. Hatutarajii watu kama hawa kuteuliwa makatibu wakuu wa serikali ya maridhiano.

Kuna mkurugenzi alithibitika kununua gari iliyokwishatumika (reconditioned vehicle) kwa bei ya gari mpya kwa ajili ya mradi uliopatiwa fedha za mkopo na Benki ya Dunia kupitia Serikali ya Muungano.

Alipogundulika na wakaguzi, Benki ya Dunia wakalazimisha serikali ilipe fedha za mradi ili inunuliwe gari iliyotakiwa. Serikali ilitoa fedha nyingine nyingine na ile kongwe ikabaki kwa aliyekuwa waziri wa kilimo.

Nyaraka zilionyesha Sh. 44 milioni zililipwa kwa muuzaji wa gari kongwe ambayo bei yake halisi ilikuwa ni Sh. 19 milioni. Maana yake, Sh. 25 milioni ziliibwa.

Mvuvi mmoja maarufu wa kijiji cha Makunduchi, Wilaya ya Kusini Unguja, anasema yeye na wavuvi wenzake wamenyimwa zana za uvuvi za kisasa zilizotolewa na mradi kwa kuwa ni wanachama wa CUF.

Anasema, “huyu bwana ni rafiki yangu lakini aliniambia hivihivi kuwa hanipi boti maana sisi hatuipendi CCM. Lakini nini CCM na mradi wa wananchi ambao unakwenda kwa mkopo tunaoulipia.”

Katika mradi huohuo, Kamati ya Baraza la Wawakilishi ilikuta kampuni isiyosajiliwa imepewa zabuni ya kuuza boti tatu za ukaguzi wa maeneo ya hifadhi ya bahari.

Ikagundua upotevu wa vitabu viwili vya risiti kwa ajili ya malipo ya leseni za uvuvi wa bahari kuu. Leseni moja hulipiwa dola 18,000. Maana yake mamilioni ya shilingi yaliibwa.

Kamati ikagundua matumizi mabaya ya mapato yanayokusanywa maeneo ya hifadhi ya Menai, Mnemba na Misali yanayosimamiwa na mradi wa usimamizi wa hifadhi na mazingira ya baharini (MACEMP).

Unaposhuhudia ofisa huyo akivikwa joho la CCM hadharani na kutajwa ni kamanda wa UV-CCM wilayani unaanguka kwa mshangao maana Sheria ya Utumishi Serikalini hairuhusu. Anayetaka kushiriki siasa lazima kwanza achukuwe likizo. Yeye yupo kazini.

Haitarajiwi ofisa kama huyu awe mmoja wa makatibu wakuu katika serikali mpya. Huyu hamfai Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Said Ali Mbarouk (CUF) wala waziri mwingine. Rais na makamu wake wawili wanapaswa kuona hili.

Itakuwa ni mazoea mabaya na bahati mbaya rais kuteua watu kwa kujuana. Haitakuwa serikali yenye heshima mbele za wananchi.

Wananchi wanataka mtumishi mwenye rekodi nzuri ya utendaji. Aliyelinda mali za serikali, aliyetekeleza majukumu yake kwa ufanisi na tija ikaonekana na yule aliyejenga watumishi wenzake kielimu kwa kuwapatia fursa za kujiendeleza. Serikali haina uhaba wa watumishi hawa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: