Mawaziri wapya: Chama kilekile, muundaji yuleyule


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 02 May 2012

Printer-friendly version
Andrew Chenge akiwa mahakamani

“FUKUZA mawaziri wanane au ondoka mwenyewe.” Je, hii ni amri? Ni shinikizo? Ni maelekezo tu?

Vyovyote itakavyokuwa, hilo ndilo chimbuko la kazi aliyopewa Rais Jakaya Kikwete ya kufanya mabadiliko makubwa kwa baraza lake la mawaziri.

Ndani ya “Bunge la Aprili,” wabunge walimkoromea waziri mkuu Mizengo Pinda, wakitaka achukue hatua dhidi ya mawaziri wanane; la sivyo ang’atuke yeye.

Na taarifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), iliyotolewa jijini Dar es Salaam, Ijumaa iliyopita, ndiyo ilithibitisha kazi aliyopewa Kikwete: Kufanya mabadiliko makubwa katika baraza la mawaziri.

Kulivunja lote ni kufukuza hata waziri mkuu. Ni kutaka kuitisha kikao maalum cha bunge ili utaratibu uanze upya na jina la waziri mkuu liwasilishwe upya.

Mawaziri wanaotuhumiwa, wametajwa katika ripoti za kamati tatu za kudumu za bunge zikinukuu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh.

Ripoti ya CAG inayoonekana chachu kuu kwa wabunge kushinikiza mawaziri kujiuzulu, inaanika upotevu, wizi, ukwepaji kodi na matumizi mabaya ya mabilioni ya shilingi katika serikali na taasisi zake.

Hata hivyo, kilio cha kutaka Kikwete avunje baraza lake la mawaziri na kuunda upya, hakikuanza leo wala jana.

Ni zaidi ya mwaka sasa, viongozi wa upinzani, hususani Chama cha Demokrsia na Maendeleo (CHADEMA), vyama vya hiari, vyombo vya habari na wananchi wengine katika kada mbalimbali, wamekuwa wakitaka Kikwete aunde upya baraza lake la mawaziri.

Waliokuwa wakitaka Kikwete avunje baraza lake na kuunda jipya, wamekuwa wakituhumu baadhi ya watendaji serikalini, kushindwa kuwajibika, wizi na ufujaji wa mali ya umma. Kikwete hakujali maoni hayo.

Huenda angefanyia kazi kilio hicho mapema, haya yanayomtokea sasa yasingetokea.

Bali kuna swali muhimu la kujiuliza: Nani amesababisha serikali ya Kikwete kuchafuka na kutuhumiwa na wananchi kila kukicha?

Uchafu wa serikali ya Kikwete ulianza na kile kilichoitwa “wanamtandao wa Kikwete.” Mtandao huu ulikuwa kokoro lililobeba wanaohitajika na wasiohitajika.

Mtandao ukaenda mbele zaidi. Ukafanya kazi chafua ya kumchafua kila aliyeonekana tishio katika mbio za Kikwete kusaka urais.

Ni wanamtandao waliomchafua, Dk. Salim Ahmed Salim. Wakamtwisha tuhuma nzito ya kupanga njama za mauaji ya rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.

Wakadai ni mwanachama wa Hizbu – chama ambacho kilikuwa na uhusiano wa karibu na utawala wa sultani visiwani Zanzibar.

Kila kona ya nchi, wakasambaza taarifa kuwa Dk. Salim ni mwarabu; hizbu na mmoja wa walioshiriki katika njama za mauaji ya Karume. Kwa hiyo wakasema, “Bwana huyu hastahili kuwa rais.”

Naye aliyeingia ikulu kwa kumia genge hili, hakuishia hapo. Aliendelea kulilinda na kulitetea.

Akaopoa wale waliokuwa wakichafua washindani wake na kuanza kuwapa kazi serikalini na katika chama. Sifa za uteuzi zikageuka kutoka kuwa uadilifu hadi kuwa “mfuasi wa mtandao.”

Hili ni moja ya dhambi inayomtafuna Kikwete. Itaweza kukoma tu, pale atakapotoka hadharani kumuomba radhi Dk. Salim na taifa kwa yale yaliyofanywa na “wanamtandao” wake.

Kumekuwa na madai ya Kikwete kuingia madarakani kwa kutumia fedha zilioibwa kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Si serikali wala CCM iliyofanikiwa kujinasua kwenye tuhuma hizi.

Wizi mkubwa ulitokea serikalini kati ya Agosti na Desemba 2005; kipindi ambacho kilikuwa cha uchaguzi mkuu na watuhumiwa wengi wanadaiwa kuchangia kampeni za Kikwete.

Mazingira haya yamevunja uthabiti wa Kikwete katika uongozi; kusababisha ulegevu na kuzaa kimya kinene kila tuhuma zinapoibuliwa.

Ni wakati huo kampuni hewaya Kagoda Agriculture Limited, ilikwapua jumla ya dola za Marekani 30,732,658.82 (zaidi ya Sh. 40 bilioni) katika Akanti ya Madeni ya Nje (EPA), ndani ya BoT.

Makampuni mengine yaliyoiba “kikubwa,” ni Green Finance Ltd., na Meremeta.

Fedha ziliibwa kwa kisingizio cha “matumizi maalum ya usalama wa taifa.” Wenye usalama wa taifa wakanyamaza.

Hili lilielezwa vizuri kwenye hati ya kiapo ya wakili Bhyidinka Sanze wa kampuni ya mawakili ya Malegesi – Malegesi Law Chambers – ya Dar es Salaam, kwa Kamati ya rais ya kushughulikia wizi kwenye akaunti ya EPA.

Sanze ameeleza jinsi fedha za Kagoda zilivyotumika kufanikisha kampeni za CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

Sanze anakiri kuwa ni yeye alishuhudia “…mikataba ya Kagoda na makampuni mengine ya nje.”

Kiapo chake kinaeleza kuwa Rostan Aziz, Peter Noni na Bered Malegesi walimthibitishia kuwa Rostam alikuwa kwenye kikao ambako rais mstaafu, Benjamin Mkapa alitoa maelekezo kwa Gavana wa BoT, Dk. Daudi Ballali kutoa fedha hizo kwa Rostam kwa ajili ya uchaguzi.

Sanze anasema, “…niliitwa na Bw. Malegesi ofisini kwa Bw. Rostam Aziz… Niliwakuta Bw. Rostam Aziz, Peter Noni (Mkurugenzi Mtendaji wa sasa wa Benki ya Raslimali) na Bw. Malegesi; wakaniambia fedha hizo zinahitajika kwa ajili ya kugharamia uchaguzi wa CCM na rais wake.”

Hili ni andishi ambalo mpaka sasa halijakanwa na serikali, Mkapa, Rostam, Sanze, Malegesi wala Peter Noni.

Hivyo basi, ndani ya kipindi cha miaka saba ya utawala wake, Kikwete ameishia kuunda serikali kwa njia ya ulipaji fadhila. Ndio maana hawezi kupata watu makini.

Baraza la kwanza la mawaziri lilibeba mawaziri 30 na naibu mawaziri 31.

Akawa rais wa kwanza, tangu uhuru, kuwa na idadi kubwa ya mawaziri kiasi hicho. Baadhi ya wizara zilikuwa na naibu mawaziri wawili.

Wale walioonekana waadilifu na wanaoweza kufanya kazi kwa maslahi ya taifa, hawakuteuliwa kuingia serikalini. Inadaiwa ni kwa sababu hawakuwa wanamtandao; na hawakuwa chaguo la Rostam Aziz anayedaiwa kujitambulisha nchini kuwa ndiye alimuweka Kikwete madarakani.

Ni sawa na methali isemayo, “Alipaye mpigazomari, ndiye huchagua wimbo.”

Kikwete alibeba lundo la watu wanaotiliwa shaka uadilifu wao. Haikuchukua muda serikali ikavunjika. Akaunda upya baraza la mawaziri.

Kuundwa kwa baraza jipya la mawaziri kulifuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na waziri mtangulizi wake katika wizara hiyo, Dk. Ibrahim Msabaha.

Kujiuzulu kwa mawaziri hao kulifuatia tuhuma kwamba walinyamazia au walishiriki kupindisha maamuzi halali ya Baraza la Mawaziri  na kukiuka kanuni, taratibu na hata sheria katika kufikia maamuzi yaliyowezesha serikali kuwa na mkataba na kampuni ya Richmond.

Kikwete hakujifunza. Mambo yakawa yaleyale alipounda baraza lake jipya la mawaziri Februari 2008. Hili lilikuwa na mawaziri 26 na naibu mawaziri 21.

Nako akarejesha tena baadhi ya wanaotuhumiwa, ama kushiriki moja kwa moja vitendo vya ufisadi, au kunyamazia na hivyo kubariki na, au kushabikia vitendo hivyo.

Miongoni mwao, ni Andrew Chenge, Adam Malima na Lawrance Masha.

Chenge ni mmoja wa watuhumiwa katika sakata la ununuzi wa rada. Ametajwa kuhusika moja kwa moja katika kuliingiza taifa katika mikataba ya maangamizi kiuchumi, wakati alipokuwa mwanasheria mkuu wa serikali kati ya mwaka 1993 na 2005.

Lakini wachunguzi wa mambo wamesema alipewa uwaziri kulipa fadhila. Ni Chenge aliyehamisha wafuasi wa Fredrick Sumaye, mara baada ya Sumaye kushindwa kwenye kinyang’anyiro cha urais ndani ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama chake.

Naye Masha, ambaye alifanywa waziri wa mambo ya ndani, ndiye kampuni yake ya uwakili – IMMA Advocates – ilishuhudia mikataba ya Deep Green Finance Limited na baadaye “kufilisi” mkwapuaji huyo wa mabilioni ya shilingi ambayo yanadaiwa kutumika katika kampeni za CCM za 2005.

Ni katika kampuni ya IMMA pia rais aliteua wakili Aloysius Mujulizi, ambaye ni mmoja wa wanahisa, kuwa Jaji wa Mahakama Kuu. Ni hukohuko mtoto wa rais, Ridhwani Jakaya Kikwete, alikwenda kufanya kazi.

Wakili mmoja akawa waziri na mwingine kutoka kampuni ileleile akawa jaji wa mahakama kuu. Wengi wangali wanajenga shaka.

Mawaziri wa Kikwete ambao wameendelea kumtesa, hawafanani kwa vyovyote vile na naibu mawaziri ambao hawakuwa kwenye mtandao.

Chukua mfano wa Balozi Khamis Kagasheki, aliyefanywa naibu waziri wa mambo ya ndani, chini Masha.

Balozi Kagasheki ni mjuzi wa mambo ya kibalozi na utawala serikalini. Katika umahiri wa utendaji kazi, uzoefu, uaminifu na kujituma, Balozi Kagasheki amepiku mawaziri wengie.

Baadhi ya marafiki wa Kikwete wanasema wazi, kwamba Balozi Kagasheki hakuwa mwanamtadao. Ndiyo maana ameendelea kusota kwenye nafasi ya naibu waziri.

Kuna Dk. Harrison Mwakyembe. Katika serikali hiihii ambayo inahubiri kuandikwa upya kwa katiba ya nchi, Mwakyembe anafanywa naibu waziri ujenzi wakati wizara ya sheria anapewa asiye mjuzi wa sheria – Celina Kombani.

Sababu inatajwa kuwa kama ile ya Kagasheki. Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, Mwakyembe aliunga mkono Profesa Mark Mwandosya.

Lakini dhambi hii imefika mbali zaidi. Katika baraza la kwanza la mawaziri alilounda Kikwete, Desemba 2005, Benard Membe alifanywa naibu waziri.

Taarifa zinasema Membe alifanywa naibu waziri kwa sababu ya minyukano ya makundi iliyoibuka ndani ya kundi la mtandao, mara baada ya Kikwete kuingia ikulu.

Tatu, ulegelege wa serikali ya Kikwete umetokana na kuingia madarakani bila ajenda. Aliingia na wimbo, “Ari Mpya, Kasi Mpya na Nguvu Mpya.”

Serikali yake, imekuwa inatenda ama kwa kujua au kutojua, matakwa ya wale waliomuingiza madarakani.

Hili linathibitishwa na kigugumizi cha serikali cha kushindwa kuwachukulia hatua wale wanaotuhumiwa kufilisi nchi.

Chukua mfano huu. Mkurugenzi wa Shirika la Viwango la Taifa (TBS), Charles Ekelege ametuhumiwa kudanganya. Waliomtuhumu ni Bunge na Mkaguzi na Mdhibiti wa Fedha za Serikali (CAG).

Ndani ya kamati ya Bunge, Ekelege amekiri kudanganya. Amesema si kweli kwamba ofisi yake imekodisha jengo na imeingia mkataba na kampuni moja ya nchini Japan ili kufanya kazi ya ukaguzi wa magari.

Lakini Ekelege amekiri haya baada ta Kamati ya Bunge kwenda Japan, kwa fedha za umma, ambako hawakukuta ofisi wala wakala.

Hata pamoja na kukiri huko, bado serikali ya Kikwete inasema inashindwa kumfuta kazi Ekelege. Inasema sharti kwanza uchunguzi ufanyike.

Haijasema ni uchunguzi gani nje ya ule wa Bunge. Nani anaweza kuaminika zaidi ya chombo hicho cha wananchi? Huku ni kupoteza muda na kupeana ulaji. Basi!

Hakuna anayejua kigugumizi hiki cha serikali kinatoka wapi. Inawezekana naye ni miongoni mwa waliochangia kampeni za Kikwete 2010?

Angalia mfano mwingine. David Jairo. Ametuhumiwa kutumia vibaya madaraka. Hajachukuliwa hatua. Lakini Jairo alikuwa ikulu kabla ya kufanywa katibu mkuu wizara ya nishati na madini. Ukaribu wake na watawala unaweza kuelezeka.

Hivyo basi, katika mazingira haya, wale wanaofurahia kuvunjwa kwa baraza la mawaziri, muda si mrefu wataishia kuweka nyuso zao chini kwa aibu. Kikwete hawezi kuunda serikali thabiti.

Atapata wapi wa kuwafanya mawaziri? Je, atatoa kwenye chama kilekile – kilichochoka na kinachotuhumiwa kutumia fedha za wizi kuingia madarakani?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: