Mawaziri, watendaji wajiandae


editor's picture

Na editor - Imechapwa 09 May 2012

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

KAMA mawaziri wapya wanafahamu sababu za kuteuliwa kwao sasa ili kuingia katika baraza la mawaziri, wana bahati kubwa.

Kama wanafahamu kuwa waliokuwa wakishikilia nafasi hizo walituhumiwa kutowajibika ipasavyo ikiwemo kuhusishwa na ufujaji wa fedha za umma na kutumia vibaya madaraka, hiyo ni bahati nyingine kubwa kwao.

Kama mawaziri wapya hawa wanajua hasa kuwa hawana kitu cha kufurahia kwa kuteuliwa kwao kuwa wasimamizi wa wizara hizo, nayo hiyo ni bahati kubwa.

Ukumbusho: Viti ambavyo wameanza kuvikalia baada ya kula kiapo, ni vya moto; havikaliki havishikiki kirahisi.

Tunazungumzia lundo la changamoto zilizo mbele ya mawaziri wapya. Kwamba yale yaliyochangia kutokomeza wale waliowatangulia, yangali mabichi.

Je, wamejifunza? Wamejiandaa kwenda mwendo mzuri wa kujenga matumaini au wanafurahia kukalia viti kwa sababu watachuma?

Misimamo yao ndiyo itawadhihirisha waliyoyadhamiria wanaposhika uongozi wa wizara.

Kama kuchuma watachuma maana watakuta machungu ya uongozi mbaya; vitendo vya ufisadi, rushwa, upendeleo na uzembe ndivyo vinavyosonga mbele badala ya tija.

Matatizo yaliyobainishwa kuwagusa mawaziri waliotemwa yamepunguza uwezo wa serikali kukusanya mapato na hivyo kusababisha ishindwe kuhudumia wananchi.

Yamezidisha malalamiko ya wananchi kuhusu ubovu wa barabara, ukosefu wa maji safi na salama, umeme, walimu, vitabu na mikopo kwa wanaoingia vyuoni, pembejeo za kilimo na ununuzi wa mazao ya kilimo.

Wizara ya Fedha na Uchumi, kwa mfano, imekuwa dhaifu katika kutekeleza jukumu lake la kulinda raslimali za nchi kama vile majengo, viwanja na hisa katika mashirika na kampuni zilizobinafsishwa.

Watendaji wa wizara hii wamekuwa legevu katika kusimamia uchumi wa nchi kiasi cha kusababisha kuongezeka kwa deni la taifa.

Mbaya zaidi, viongozi waandamizi serikalini wamekataa kubadili mwenendo mbaya wa matumizi ya fedha za serikali.

Eneo hili limeleta madhara makubwa. Mara kadhaa serikali imelazimika kukopa benki za biashara ili kukidhi mahitaji yake ya kuendesha shughuli zake.

Mtindo huu unajenga taswira mbaya kwa wananchi na hata kwa wafadhili au washirika wa maendeleo; ambao wamekuwa wakiishutumu serikali kwa matatizo hayahaya tunayoyaelezea.

Sasa, tunasema siku za serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujiimarisha hazipo tena. Hiyo ndiyo athari ya viongozi waandamizi kukataa kubadilika. Wameharibu kila kitu.

Mwezi mmoja uliobaki wa maandalizi ya bajeti ya mwaka wa fedha wa 2012/13 hautawasaidia. Baasi, wajiandae kukabili vishindo vya wabunge walioamua kutumikia umma badala ya nafsi zao kwanza utakapoanza mkutano wa bunge la bajeti katikati ya mwezi ujao.

0
No votes yet