Mawaziri wawapa wapinzani mtaji mpya


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 13 June 2012

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Jumamosi iliyopita kilitumia misuli yake yote ya kifedha na raslimali watu katika juhudi za kujibu mapigo ya wapinzani wao wa sasa kisiasa, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Katika mkutano ule, CCM walifanikiwa mambo mawili. Kwanza walikusanya umati mkubwa pungufu kidogo au sawa na uliofanywa na CHADEMA wiki mbili zilizopita. Pili, walikwenda katika viwanja vilevile vya Jangwani kujibu mapigo.

Mkutano ule, kama ulivyotangazwa na katibu mwenezi wa mkoa wa Dar es Salaam, Juma Simba, uliitishwa kwa lengo la kuwapa wananchi majibu ya kero walizotoa wanachama wa mkoa wa Dar es Salaam katika ziara iliyofanywa na mlezi wao Abdulrahiman Kinana.

Huyo alitarajiwa kuwapa majibu. Lakini kumbe ilikuwa ghiliba. Mkutano ule ulikuwa wa hadhara ulioandaliwa kwa lengo la kuwapa fursa mawaziri kueleza namna walivyojipanga kufanya kazi zao.

Mawaziri, japokuwa ni kweli wanatoka chama tawala, wanawajibika kwa wananchi wote na si chama peke yake.

Hiyo ndiyo sababu mawaziri walijitokeza na harara kujibu shutuma za ugoigoi walizotupiwa na wapinzani wao; na siyo kutoa majibu Kinana alisikia nini kutoka kwa wanachama katika ziara yake.

Kwa hiyo, madai ya kuwepo majungu, fitina, uzembe, ubabe na kutofanyika vikao kwa mujibu wa taratibu au baadhi ya wanachama kupata madaraka kwa rushwa, hayakujibiwa.

Wanachama walikuwa na kiu yao lakini na viongozi walikuwa na yao moyoni. Kwa kuwa, Kinana hakuwa na majibu juu ya madai, hasa ya wanachama, mbinu pekee ya kufunika ilikuwa kuita mawaziri waeleze kile ambacho serikali imepanga kufanya katika bajeti ya mwaka 2012/ 2013.

Upande wa pili ni majibu ya mawaziri hao kuwapa mtaji mwingine wapinzani. Kila waziri aliyesimama alisifu serikali ya CCM kwa mipango mizuri ya kuwasomesha na sasa wanaitumikia.

Mawaziri hawa wanasahau kwamba wengi walianza kusoma enzi wa ukoloni, TANU iliendeleza mazuri yote kuhusu elimu, CCM ikavuruga.

Waziri wa kwanza kuitwa ‘kujibu’ kero za wanachama wa CCM alikuwa Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe. Alieleza mipango mingi.

Alichosahau ni kwamba wakazi wa Dar es Salaam wanakumbuka ahadi za neema ya maji tangu mwaka 1995 wakati wa kampeni na baada ya Benjamin Mkapa kushinda urais.

Mkapa alitembelea vyanzo vyote vya maji, lakini mpaka leo shida iko palepale. Maeneo mengi wanategemea maji ya visima walivyochimba wao wenyewe.

Mwenyekiti wa CCM, mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita alionekana kusaidia majibu akisema kwamba hii inatokana na watu wengi kuhamia Dar es Salaam.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka, alipewa jukumu la kueleza mahali ilikofikia mipango ya fidia na ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni.

Alichosema ni kwamba mambo yameiva. Hakufafanua malipo ya fidia kwa wakazi hao na wale wanaovunjiwa makazi yao eneo la Kurasini.

Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe alitoa ahadi za kufanyika safari za treni ya Tazara kutoka Mwakanga hadi Stesheni, na kutoka Ubungo Maziwa hadi Steshini kwa reli ya kati.

Mipango hii si mipya. Serikali imekuwa ikitoa ahadi kama hizi tangu miaka ya 1990 lakini utekelezaji wake hauonekani. Kinachokwamisha ni uhaba na uchakavu wa injini, mabehewa na akili ya nyongeza.

Ahadi nyingine iliyomo kwenye makabrasha ya serikali ni ununuzi wa feri mbili za kubeba abiria kutoka bandari ya Dar es Salaam hadi Bagamoyo ili kupunguza msongamano barabarani.

Maadamu amesema na amesikika, kazi ya wapinzani ni kufuatilia utekelezaji na uendelezaji wake. CCM wataumbuka.

Dk. John Magufuli, Waziri wa Ujenzi anafahamika sana kwa uwezo wa kukariri.

Wakijua kwamba hiyo ni “gia” yao ya kushawishi watu, walimpa nafasi ya mwisho.

Hakueleza kitu kipya ila kurudia takwimu – tarakimu lukuki za urefu wa barabara ambazo alidai serikali ya CCM imejenga; bila hata kushukuru wananchi walipakodi.

Hata ukimwamsha usingizini, Magufuli  atakwambia kilomita hizohizo 11,000 za lami zilizokamilika, wakandarasi wake pamoja na gharama.

Wananchi wamemzoea Magufuli na tarakimu zake. Wengine wanamwita “Jembe la CCM” lililokobokea kwenye mizizi ya mikaritusi.

Kati ya mawaziri hao wote, aliyeandaliwa kujibu vijembe na kujibu mapigo alikuwa Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais – Mahusiano), Steven Wassira.

Wasira alitoa kile alichodhani ni kero ya wakazi wa Dar es Salaam, hususan wana-CCM.

Kwa mujibu wa Wassira, kero ya wana-CCM ni naibu katibu mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Kuhusu Zitto, Wasira alisema mipango ya kufufua uchumi aliyowaeleza waandishi wa habari ameichota kutoka kwa Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk. William Mgimwa.

Halafu akasema Mbowe atakuwa anakufuru kusema nchi hii haijafanya lolote wakati baba yake, Aikaeli Mbowe alishirikiana na Mwalimu Julius Nyerere kudai uhuru.

Wassira aliyetarajiwa kueleza namna serikali ilivyojipanga kupunguza makali ya maisha, alisema serikali italima hekta 100,000 za ‘mchele’ katika bonde la Kilombero.

Halafu akasema watajenga viwanda vitano vya sukari katika maeneo ya Kilombero, Rufiji, Wami, Kagera na Malagarasi.

Kwanza, kuhusu mipango ya kilimo cha mpunga, siyo mchele kama alivyosema Wassira, si mipya.

Tangu miaka ya 1970 kulikuwa na kauli za kuanzisha miradi ya kilimo cha mpunga katika bonde la Rufiji kwa ushirikiano na Korea Kaskazini, lakini haikutekelezeka.

Mradi wa Bonde la Rufiji, pamoja na mambo mengine, ulilenga kuvuna maji kwa ajili ya nishati ya umeme na kilimo kikubwa. Viko wapi? Wassira anaimba ngonjera zilezile. Huyu msanii!

Wassira ameshindwa hata kuzungumzia kwa nini, pamoja na kuanzishwa sera ya Kilimo Kwanza, bado Tanzania hakuna uhakika na usalama wa chakula. Huyu ni msanii.

Tatu, ahadi za viwanda vya sukari, matunda katika wilaya za Korogwe, Lushoto na Muheza, zina umri sawa na wa serikali ya Kikwete.

Kwa kuwakumbusha wanachama wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, Rais Kikwete alitoa ahadi hizi tangu wakati wa kampeni zake mwaka 2005.

Mwaka 2006, katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM, Rais aliahidi kujenga viwanda vikubwa vya sementi na mbolea katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Kusanyiko la Jangwani la Jumamosi iliyopita, limewaonyesha wakazi wa Dar es Salaam kuwa wananchi wanakaa huku na serikali inakaa kule!

Watawala wanahutubia kutoka kileleni; wakitamanisha wananchi wenye njaa na kiu ya mabadiliko; lakini bila kutoa chochote cha kukidhi haja zao.

Kama waliokuwa kwenye madaraka kwa miaka 50 wameshindwa kueleza hata walichofanya na wanaendelea kutoa ahadi; si wangekaa pembeni na kuona majembe mapya yakikwatua?

0
No votes yet