Mbagala wakanusha kauli ya serikali


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 04 May 2011

Printer-friendly version

MIAKA miwili baada ya tukio la milipuko ya mabomu katika kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Mbagala, Dar es Salaam, malalamiko yameibuka kuwa waathirika wengi hawajalipwa fidia wanazostahili.

Hata hivyo, tayari serikali imetangaza kumaliza kazi ya kufidia waathirika wa milipuko.

Mwandishi wa habari hii ameelezwa kuwa wakazi wa Mbagala ambao wanaoneshwa kwenye orodha ya wahanga, kuanzia Na. 401 hadi 461, hawajalipwa stahiki zao hadi sasa.

Kwa mujibu wa Mzee Khamis Mohamed King, ambaye namba yake ya fidia ni MA/1/410, kuna makundi matatu ya wanaodai fidia, ambayo ni wenye nyumba, wapangaji na majeruhi wa tukio hilo.

Anasema baadhi ya waathirika wanaendelea kuishi kwenye mahema, nyumba zisizo na milango wala paa; na wapo wengine wengi ambao nyumba zao zilipata mipasuko mikubwa iwezayo kusababisha nyumba kuanguka na kuleta maafa.

Khamis King anasema, “Kimsingi sisi tumeshangaa kuona serikali inatangaza kuwa imemaliza zoezi la kulipa fidia Mbagala. Ukweli ni kwamba tuko wengi ambao hatujalipwa na tulikuwa tunasubiri malipo yetu.”

Anasema, “…baadhi yetu tunaishangaa serikali hii. Yenyewe ndiyo iliahidi kulipa hadi mwaathirika wa mwisho; lakini leo inasema imemaliza kazi hiyo na hakuna anayedai. Bado tunadai.”

King ambaye nyumba yake sasa imezibwa kwa turubai juu baada ya mabati kuezuliwa wakati wa milipuko hiyo ya 28 Aprili 2009, anahoji “Sasa twende wapi? Huu ni uonevu na nafikiri kuna mazingira ya rushwa katika suala hili.”

Anasema baadhi ya waathirika wamefanikiwa kuona majina na picha zao katika kompyuta serikalini zikiwatambulisha kama waathirika wanaohitaji fidia, lakini cha ajabu kwenye malipo hawakuwapo.

Naye Seif Najume, kiongozi wa waathirika hao, anasema ilichukua miezi saba kwa baadhi yao kuweza kupewa sehemu ya kifuta jasho chao na serikali.

Anasema aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi, ambaye sasa ni waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu (Bunge na Uratibu), aliwalipa baadhi ya waathirika hao miezi saba baada ya tukio.

Anasema malipo hayo waliyapata baada ya kutishia kwenda kulalamika katika ngazi za juu.

“Sisi tulikaa miezi saba bila kusikilizwa. Wakati huo, wenzetu wengine walikuwa tayari wamelipwa. Tukaenda kwa Lukuvi na kumwambia tunakwenda kwa waziri mkuu kulalamika. Ndipo akasema, ‘basi chukueni hizi na halafu mlete madai yenu, serikali itayasikiliza,’” ameeleza.

Anasema, “Cha ajabu baadaye, katika mkutano tuliofanya pamoja naye (Lukuvi), serikali ilikuja na hoja mpya, kwamba majina yetu hayapo kwenye orodha ya watakaolipwa.”

Akizungumza kwa sauti ya uchungu, Seif anasema, “Sisi ni miongoni mwa wale ambao serikali ilifanya tathmini ya mali zetu na kupewa namba ya malipo. Lakini leo, tunaambiwa kuwa hatustahili kulipwa. Huu ni uonevu na tunamuomba waziri mkuu atusaidie kupata haki zetu,” anaeleza kwa msisitizo.

Anasema baada ya kufika ofisini kwa Lukuvi na kuzungumza naye, wakati huo akiwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, serikali ilitoa hundi kwa waathirika hao.

Katika malipo hayo, baadhi ya waathirika walipata Sh. 300,000 (laki tatu) na wapo waliopata Sh.400,000 (laki nne) kama kifuta jacho kwa ahadi kwamba wawasilishe upya madai yao ili serikali iweze kuyafanyia kazi na kuwalipa stahiki zao.

Anasema, “Hilo halijafanyika hadi sasa; badala yake serikali inatangaza imelipa watu wote na kwamba malipo kwa waathirika wa Mbagala yamefungwa.”

Akijibu madai hayo, Lukuvi amesema kama kuna watu wana matatizo kwenye suala la malipo ya fidia, serikali iko tayari kuwasikiliza.

Amesema, “Kimsingi tumemaliza zoezi la ulipaji fidia. Lakini kama kuna mtu au kundi la watu ambao wana madai kwenye suala hilo, tuliwaambia wayalete.”

Amesema, “Kazi ya serikali ni kusikiliza, kupokea malalamiko yote ya raia na kuyatafutia ufumbuzi wa kudumu. Nakukuhakikishia hakuna mwananchi ambaye anastahili fidia ambaye hatalipwa, kwa sababu yoyote ile.”

Akiongea kwa kujiamini, Lukuvi amesema, “Waambie walete madai yao haraka na serikali itayasikiliza.”

Muathirika mwingine wa mabomu ya Mbagala, Zaina Abdallah Kwangaya, ambaye kwa sasa anaishi katika hema katika eneo la Mbagala Kuu, anasema tangu tukio hilo, yeye na familia yake ya watu 10, imekuwa ikiishi kwa shida na mashaka.

Anasema hema aliloweka katikati ya kuta zilizosalia lakini zenye mipasuko mikubwa, ni bovu na linapitisha mvua. Nyumba yake ilikuwa na vyumba vinne; leo ni kuta tupu zenye mipasuko, bila milango, madirisha wala paa.

Alipoulizwa kwa nini anang’ang’ania kuishi mahali hapo, Kwangaya amesema, “Hatuna pa kwenda. Tumelazimika kuteseka humuhumu na watoto wangu. Ndiyo hivyo tena,” anaeleza kwa sauti ya masikitiko.

Aliyekuwa miongoni mwa wapangaji wa nyumba za waathirika, Salma Omari, amesema hawajalipwa fidia ya vyombo vyao kama serikali ilivyoahidi.

Amesema kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa, wapangaji waliokuwa wakiishi katika nyumba zilizoathirika, walitakiwa kulipwa fidia ya vyombo vyao vilivyoharibiwa; jambo ambalo halijafanyika hadi leo.

Mwathirika mwingine, Grace Mwankusye, aliyekuwa mamalishe kabla ya maafa hayo, alimwambia mwandishi huyu kuwa alivunjika mkono katika tukio hilo na hajalipwa fidia hadi leo.

“Nililazwa katika Taasisi ya Mifupa ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MOI), kwa muda wa miezi mitatu baada ya kuvunjika mkono kutokana na kuangukiwa na ukuta wa nyumba yangu.

“Tangu tukio hilo, nimeacha kufanya kazi ya upishi kwa sababu mikono haina nguvu tena. Watoto wameacha shule. Naishi maisha magumu sana. Ninaiomba serikali inilipe stahili zangu kama ilivyotangaza,” alisema.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kizuiani ambako yalitokea maafa hayo, Mashaka Selemani maarufu kwa jina la Gaddafi, alisema ni vema serikali itimize wajibu wake kwa vile wananchi hao wana haki ya kulipwa kama wengine waliolipwa.

Selemani pia alisema amepata taarifa kutoka kwa askari waliokuwa wakiishi katika kambi ya Kizuiani kuwa wao hawajalipwa fidia kwa mali zao zilizoteketea wakati wa milipuko hiyo. Haikuweza kuthibitishwa.

Waathirika hao wamedai pia kuwa kuna harufu ya rushwa. Wanadai tathmini ya thamani ya mali zao ilifanyika chini ya kiwango kwa vile baadhi ya wathamini hawakuingia hata ndani ya nyumba.

“Hivi mtu atajuaje thamani ya nyumba na mali zilizomo ndani yake bila ya kuingia ndani? ameuliza Issa Lunda mwenye namba ya fidia Na. MA/1/453.

Katika taarifa rasmi ya serikali iliyotolewa 31 Januari mwaka huu, serikali ilisema kuwa imekamilisha ulipaji wa fidia hiyo kwa kutumia kiasi cha Sh. 10.2 bilioni.

Kwa mujibu wa serikali, katika maafa hayo, wananchi 26 walipoteza maisha, 636 walijeruhiwa huku wengine 9,704 wakiharibiwa nyumba na kupoteza mali zao.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: