Mbalamwezi: Prof Lipumba aache uenyekiti


Yusuf Aboud's picture

Na Yusuf Aboud - Imechapwa 02 February 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

OMAR Said Mbalamwezi amechoka na amekata tamaa kisiasa. Anaona Chama cha Wananchi (CUF) alichojiunga tangu kilipoanzishwa mwaka 1992, kinaelekea kubaya.

Anatoa rai itakayosaidia kuimarisha chama hicho kinachoonekana kupata nguvu upande wa Zanzibar lakini kikidhoofika mwaka hadi mwaka Tanzania Bara.

Anadhani ni wakati sasa kwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba kupumzika na kutoa nafasi kwa mwanachama mwingine kushika nafasi hiyo.

Mbalamwezi, katika mahojiano aliyofanya MwanaHALISI wiki iliyopita mjini Mwanza, anasema Prof. Lipumba ni tatizo kiuongozi na “si vizuri kuacha hali mbaya iliyopo.”

Mbalamwezi anasema chama kinaendeshwa kibabe, viongozi wakuu hawawajibiki na wanashindwa kuthamini mchango wa wanachama wao.

Haoni kama kuna mchawi mwingine isipokuwa uongozi wa mazoea wa viongozi wakuu.

“Hata kufanya vibaya kwa chama hiki katika uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani mwaka 2010, kulitokana na kutowajibika kwa viongozi wa kitaifa hasa upande wa Tanzania Bara,” anasema Mbalamwezi ambaye anachukuliwa kama ndio nguzo muhimu ya CUF mkoani Mwanza.

Kauli hii ya Mbalamwezi imekuja siku chache baada ya mwanachama mwingine maarufu wa CUF, Profesa Abdallah Jumbe Safari kujiondoa akilalamikia ubabe, chama kukosa mwelekeo na kutoweka kwa kaulimbiu ya miaka mingi ya “Haki Sawa Kwa Wote.”

Mbalamwezi, mwanachama aliyekipa wakati mgumu Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi wa mbunge mwaka 2000 na 2005 akigombea jimbo la Nyamagana, Mwanza, anasema:

“CUF inakabiliwa na matatizo makubwa na isipojirekebisha itaangamia.”

Miongoni mwa matatizo anayoyaona ni kwamba hata viongozi wakuu Bara hawakubaliki katika maeneo wanayotoka, tofauti na wale wa Zanzibar.

“Unajua kujiimarisha mikoani kwa upande wa Bara ni muhimu sana kwa chama chetu hiki, lakini viongozi wetu hawalifikirii hili na hata ukiwaambia hawachukui hatua,” anaeleza Mbalamwezi, mwenye umri wa miaka 63.

Anaamini Kwa mujibu wa Mbalamwezi, viongozi wa juu wameng’ang’ania ofisi kuu za Buguruni, Dar es Salaam tu huku wakisahau umuhimu wa kuweka nguvu za kuimarisha chama mikoani.
 
“Viongozi wa kitafa wamekuwa kama wakimbizi kwenye maeneo waliyotoka. Ukifuatilia matokeo ya uchaguzi mkuu utagundua hata Prof. Lipumba nyumbani kwao Tabora amepata kura chache kuliko mgombea wa CCM na hata wa CHADEMA.”

CCM ilimsimamisha Jakaya Kikwete wakati CHADEMA ilimsimamisha Dk. Willibrod Slaa kuwania kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Anaonya kuwa bila ya viongozi wake kuimarisha chama na kujiimarisha katika maeneo wanayotoka mpaka wakakubalika kwa wananchi, CUF itaendelea kupata shida kupenya nyoyo za Watanzania na kuwashawishi kukiunga mkono wakati wa uchaguzi.

Bali Mbalamwezi anahofia kwamba iwapo viongozi hawatakuwa tayari kubadilika, “chama hiki kitakufa.”

“Mafanikio waliyoyapata CHADEMA katika uchaguzi uliopita hayakuwa ya kubahatisha. Waliwekeza sana na walijipanga vizuri kuanzia kwenye uteuzi wa wagombea wao hadi kampeni zenyewe. Lakini sisi viongozi wetu walibaki wamelala,” anasema.
 
Siasa ni harakati, anasema, na kuongeza kuwa harakati hazina muda wa kulala mwanzo wa mwaka mpaka mwisho wa mwaka tofauti na wanavyofanya viongozi wa CUF.

“Viongozi wetu wa kitaifa hawana mawazo ya kukijenga chama mikoani, wanafikiri wakikaa Buguruni inatosha,” anasema na kutaka waige mfano wa wenzao wanaozunguka nchi kutangaza chama chao.
 
“Ukikaa kusubiri kampeni za kila baada ya miaka mitano ndipo uende kwa wananchi utasahaulika. Wenzako watakuwa wameshapita na kuwabadilisha mawazo waliokuwa wanakuunga mkono.

“Nasisitiza ili chama chetu kirudi katika enzi za mwaka 2005 lazima viongozi wahame Buguruni waje mikoani kufufua chama. Wafanye vikao na wagombea wote walioshindwa na kuwapa semina ili kuwatia moyo waendelee kukiunga mkono chama.”

Ubinafsi

Mbalamwezi anasema tatizo jingine la viongozi wengi wa CUF ni tabia ya kukataa ushauri wa au ushirikiano na vyama vingine vya upinzani.

“We angalia hapa kwetu Mwanza, madiwani wetu hawakuipigia CHADEMA kwenye kura za kuchagua meya, badala yake kura zao mbili walizipeleka CCM, wakati kama wangewapigia CHADEMA kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kupata nafasi ya naibu meya.”

Lakini Mbalamwezi ana jibu linamsumbua kuhusu mashakil yaliyomkuta wakati wa uchaguzi uliopita.

Analalamika kuwa alitoswa na viongozi wa makao makuu katika nia yake ya kuwania ubunge 2010.

Anasimulia, “Wanaonilaumu hawajui kilichotendeka. Wanachama wa CUF wengi walio nje ya wilaya hii ya Nyamagana hawaelewi kilichotokea hapa kwetu.”

Sasa ngoja niwaeleze, anasema. Alipogombea mwaka 2000 na 2005 hakupata msaada wowote wa fedha kutoka chama chake kwa madai kuwa hakikuwa na fedha.
 
Katika uchaguzi wa mwaka jana, Mbalamwezi anasema katibu wa wilaya ambaye pia ni mjumbe wa mkutano mkuu wa taifa wa CUF, Idd Katimba aliwaambia chama kingetoa fedha kusaidia wagombea wake.

“Nilipata nguvu na moyo,” anasema. Aliamua kwenda makao makuu Dar es Salaam kufuatilia kupata msaada.

Lakini, anasema, hakuonana na Prof. Lipumba kwa vile alikuwa safarini nchini Ujerumani na katibu mkuu, Maalim Seif Shariff Hamad alikuwa ziarani nchini Uingereza.

Alibahatika kuonana na Shaweji Mketo, Mkurugenzi wa Uchaguzi CUF. Lakini kuhusu suala la kusaidiwa fedha za kuendesha mikakati ya kushinda ubunge, anasema, alijibiwa kuwa “Chama hakina fedha na hakiwezi kuwasaidia chochote wagombea.”

“Nilipomwambia, mbona ninataarifa kuwa baadhi ya majimbo yametengewa fedha na chama, alikiri ni kweli lakini jimbo langu halimo.”

Mbalamwezi anasema kwamba alichopata kwa Mketo ni kauli kwamba atamsaidia Sh. 2 milioni kwa ajili ya kununulia vifaa kama jenereta na kipaza sauti.

Aliomba kupatiwa vipeperushi na fulana za chama, lakini alijibiwa na Mketo kuwa hakuna isipokuwa angempeleka kwenye duka linalouza ili anunue kwa fedha zake.

“Nilivunjika moyo lakini sikukata tamaa. Kwa kuwa nilikuwa peke yangu niliyechukua fomu ya chama kuomba niteuliwe kugombea, niliendelea. Nilirudisha fomu kabla ya kusafiri kwenda Dar es Salaam.

Mbalamwezi anasema aliporejea mjini Mwanza aliarifiwa na Katimba (katibu wa Wilaya wa CUF) kuwa binti mmoja aitwaye Zabibu Ramadhani alichukua fomu za ubunge nje ya muda uliyopangwa.

Anasema wakati wa kura za maoni ndani ya chama, alipata kura 76 huku Zabibu akiwa na kura 94.

Kwa kuwa alishindwa, anasema alimpongeza mshindani wake na kuahidi kuwa meneja wake katika kampeni.

Baadaye alifuatwa na wanachama waliomuunga mkono na kumshauri akate rufaa. “Nilikataa kwa sababu niliona wanachama ndio walionikataa. Ilikuwa uamuzi wao wa kidemokrasia,”

Anasema majina yao yalipendekezwa na chama kujadiliwa katika vikao vya juu vya uchambuzi. Huko, jina lake lilirudi.

Uamuzi huo anasema ulimshtua kwani kati ya kata 12 za wilaya, nne tu zilimuunga mkono kwenye kura za maoni. Kata nane zilimkataa.

Aliwajulisha viongozi wa wilaya kwamba hatogombea kwasababu hakushinda kura za wanachama na alihofia kutoungwa mkono na wanachama hao wa kata zilizomkataa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: