MBEZI BILUNGI: Wafanyakazi walitutelekeza tufe peke yetu


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 21 September 2011

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki

MBEZI Wilbard Bilungi hajapona. Hakika bado anaumwa.

Wala kinachomsumbua siyo kufikiria kile kilichotokea usiku wa manane Septemba 9, mwaka huu, eneo lenye mkondo mkubwa wa maji la Nungwi katika Bahari ya Hindi.

“Ugonjwa” unaomkatili Bilungi mawazoni mwake ni wa kufikiria “masikitiko” zaidi kuliko uhalisia wa jambo lenyewe – kuzama kwa meli ya Spice Islander 1 iliyokuwa ikisafiri kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Wete, kupitia Bandari Kuu ya Malindi, mjini Zanzibar.

Akiwa mmoja wa mamia ya watu walionusurika katika ajali hiyo, Bilungi, mkazi wa Kunduchi Mtongani, Dar es Salaam, anasema laiti kila ofisa wa taasisi husika za serikali, pamoja na nahodha na mabaharia wake, angetimiza wajibu wake ipasavyo, ajali isingekuwa na uzito namna ilivyotokea.

Anaelezea udhaifu mkubwa wa uwajibikaji kikazi kwa watu hao kama chimbuko kuu la kuzama kwa meli hiyo. Na hapo ndipo penye msukumo wa kupotea kwa roho za mamia ya watu wengi waliokuwa ndani ya meli hiyo.

Kwa Bilungi ambaye amezungumza na MwanaHALISI juzi akiwa nyumbani kwake, idadi inayotajwa na serikali, ya watu waliokufa katika tukio hilo, si halisi katika mazingira yoyote yale.

Mpaka sasa, serikali inasema kwamba watu waliokufa katika ajali hiyo mbaya zaidi kutokea katika historia ya usafiri wa baharini visiwani Zanzibar, ni 203 na waliopatikana wazima ni 619. Jumla yake ni watu 822.

Lakini, Bilungi anasema kwa kuchukulia wale waliopona kama yeye na wale waliotangazwa kuwa wamekufa, basi anaamini wale wenzao ambao hawajapatikana ndio wengi zaidi.

“Ndugu yangu kila nikifikiria watu waliokuwa katika deki mbili za meli ile, ambao walikuwa chini ya nilipokuwa mimi nimekaa, wale ni wengi sana zaidi yetu. Kule tumeacha wanawake wengi, watoto wengi, wazee wengi,” anasema.

Hapohapo ndipo Bilungi anapobadilika sura. Sasa anakasirika. Anauliza, “Hivi mabaharia wanaweza kujibu nini wakiulizwa sababu ya kufunga mlango wa kuingilia kule chini.”

Bilungi anasema alishuhudia mlango wa kwenda chini umefungwa wakati wafanyakazi wa meli wakihangaika kujiokoa. Kwa kuufungua mlango ule, Bilungi anasema, tayari iliashiria kuwa “wenzetu walioko kule chini wameambiwa kumoeni mfe.”

Anasema watu wengi waliojirusha kwenye maji walitokea sehemu ya juu ya meli, ikianzia na pale alipokuwa amekaa yeye na wenzake. Penyewe hapo, anasema, palikuwa pamesheheni watu.

Bilungi anawashitaki wasimamizi wa ukaguzi na safari za vyombo bandarini pamoja na nahodha na mabaharia wake, kwa sababu waliiachia meli kupakia abiria na mizigo kinyume na uwezo wake.

Anasema meli ilijaa tangu bandarini Dar es Salaam ilikoondoka kiasi cha saa 5 asubuhi siku hiyo ya Ijumaa. “Iliondoka ikiwa na abiria wengi tayari na mizigo ikiwemo magari na magunia ya bidhaa mbalimbali. Lakini safari yetu kwenda Unguja ilikuwa nzuri na tulifika bila hofu yoyote,” anasema.

Bilungi anasema hali ya mambo ilibadilika mara tu walipofika bandarini Zanzibar. Alihitaji kutoka nje ya bandari kwa ajili ya kupata mahitaji ikiwemo vocha ya salio la kwenye simu zake kwani, “simu zangu zilikuwa hazina salio.”

Alipiga simu akiwa safarini kutoka Dar es Salaam hadi zikakauka. “Nilianza kuzungumza na mwenzangu mmoja akiwa Pemba. Simu yake ikaisha salio. Nikalazimika kumpigia kwani tulikuwa hatujamaliza mazungumzo yetu,” anasema.

Alipotoka nje ya geti la kwanza, alikuta watu wengi wakisubiri kuruhusiwa kuingia bandarini ili kupanda meli; ile ambayo anasema ilikuwa imepata abiria si haba.

“Watu ni wengi na ilinichukua muda hadi kupata kutoka kwa kupitia upande wa kuingilia bandarini badala ya ule wa kutokea. Hapa niliomba kwa ofisa mhusika kutumia mlango huu na alinielewa... aliona ukweli watu wengi walikuwa wanasubiri kuingia ndani,” anasema Bilungi, mzaliwa wa mkoani Kagera miaka 39 iliyopita.

“Ukweli abiria niliwakuta nje ni wengi kuliko niliowaacha kule ndani ya meli. Katika hali hiihii, kuanzia saa 11 watu waliruhusiwa kuingia ndani,” anasema akielezea udhaifu aliouona mapema kwa maofisa usalama wa bandari Zanzibar.

Bilungi anasema ilipofika saa 2.15 usiku, mwenzake mmoja alimwambia aangalie upande wa nje kwenye meli. “Niliona meli imeanza kulala upande mmoja. Punde nikasikia watu wanapiga kelele. Nilipofuatilia nikakuta kumbe ni furaha za abiria kwa uamuzi wa wenye meli kupunguza watu,” anasema.

Hata hivyo, anasema furaha hiyo ilizimika muda mfupi. Ilibainika walitoka watu wasiofika 20. Kelele mpya zikaibuka watu wakipinga kitendo cha wenye meli kutopunguza watu zaidi.

“Nikichukua hawa waliotoka naona ni kama vile meli haikupunguka mtu maana kuna watu idadi kama hiyo waliingia kwetu kutoka meli ya Buraq,” anasema.

Meli ya Buraq nayo iliwasili katika muda uliokaribiana na Spice Islander 1.

Bilungi anasema ilipotimia saa 3.15 hivi, baada ya kutoka tangazo katika meli kutaka watu watulie sehemu zao na kwamba meli itakaa sawa inapoanza kuondoka, alipiga simu Na. 112 kuomba Polisi wachukue hatua.

“Iliita sana namba hii hadi kukatika, bila ya kupokelewa. Nilipopiga tena nikajibiwa ‘huduma unayoihitaji huwezi kuipata kwa sasa’ nikaacha,” anasema.

Bilungi anathibitisha alivyo mzoefu wa kusafiri kwa meli kwa kusema alishangaa meli kupiga honi moja tu saa 3.30 usiku badala ya mara tatu inapoanza kuondoka bandarini.

“Safari yetu ilikuwa na mashaka mengi huku hatari ikiwa wazi kabisa. Mwendo wa saa tatu tu hatari ikadhihiri. Mwenzangu alijaribu kuondoka tulipokuwa tumekaa. Alishindwa. Ila alinishtua kuangalia hatari.

“Kama nilishtuka na kukuta labda ndoto hivi. Kama ninadondoka hivi. Nikanyamaza. Saa 7 kasoro hivi nikasikia kimlango cha chumba cha walipo maharia na nahodha wao kimefunguliwa. Wakatoka watatu na kufungua sehemu wakatoka na lifejacket na haraka wakarudi ndani.

Nikasikia tangazo la meli kutaka watu watulie wafanyakazi wanaweka mambo yote sawa. Kumbe hali ishakuwa mbaya. Nikachomoa lifejacket pale.... Pembeni walikuwepo dada wawili, mmoja akalalamika mbona nami hunipi, naomba tupatie.

Alitoa lifejacket kwa ajili ya huyo dada lakini anahofu, “sijui kama alilipata. Mahitaji yalishakuwa makubwa kuliko yaliyopo.”

“Hapa tayari hali ilikuwa mbaya kwenye meli. Nikaanza kuona kila mtu anahangaika kivyake. Nikaona watu wanatoka chini kupanda juu, wengine wanajitupa baharini. Nami nikajitupa. Wale mabinti wawili jirani wakaniangukia, mmoja akanishika mwingine akavamia lile lifejacket.

“Niliwasihi watulie na yule aachie lile lifejacket maana likitoka tumekufa sote. Hapa bahari imechafuka, mawimbi makali yanatupiga. Tayari tumeiacha meli na naiona ileee inazama. Sikuona msaada wa wafanyakazi wa meli. Anayekueleza anakudanganya, walituelekeza tangu walipogawana malifejaketi.

“Wale kinadada wawili tuliachana na niliumia kuona yule mdogo amechoka na kumshuhudia anakufa. Baadaye niliona watu wamebaki kwenye mgongo wa meli. Nikazidi kushikilia kipande cha lifejaketi na nilikishikilia kwa zaidi ya saa tatu. Awali nilisikia mngurumo wa boti mbili bali sikuziona karibu. Pia nilisikia kama ndege nikapiga kelele bila ya kusaidiwa.”

Nusura yake ni pale ilipotokea boti ya wazungu ikipeperusha bendera nyekundu. Alifikiwa na baada ya kazi kubwa, mara alipoachia kipande cha lifejaketi, wakafanikiwa kumpata na kumwingiza kwenye boti hiyo.

Una maana msaada ulichelewa, anaulizwa. “Nini? Msaada? Ah ulichelewa mno. Sana tu. kama ungewahi, watu wengi wangesalimika. Na hili ni jambo ambalo ni vizuri nyinyi waandishi wa habari mkatusaidia kulieleza vizuri.”

“Wafanyakazi wa meli walitutelekeza, vyombo vya kutuokoa vilikuja tumeshachoka sana, mimi mwenyewe nilikuwa tayari naangalia nitakufa vipi. Hapa watu wengi walishakufa. Lakini nakwambiaje, watu wengi wamezama kule chini pamoja na meli. Basi inatosha,” anasema akiashiria kushindwa kufikiria machungu ya ajali.

Bilungi anasema angalau alipata moyo baadaye alipofanikiwa kuwashawishi wazungu kufuata upande alikokuwa ametokea, ambako walimkuta yule dada mmoja aliyeshika ndoo, na wakampata. “Walipomuingiza kwenye chombo tu, alizimia. Nataka kuamini ni mzima leo,” anasema.

Bilungi alikuwa akienda Wete ambako anashughulika na kazi ya ufundi kwenye miradi ya ujenzi wa shule za sekondari inayoendeshwa na Wachina.

0
No votes yet