Mbinga wanakwepa elimu, wanajaribu ujinga


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 07 December 2011

Printer-friendly version

MAZINGIRA duni ya utoaji elimu kwa baadhi ya shule katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma yanachochea wanafunzi kutoroka au kuacha masomo na kujiingiza katika shughuli za kilimo, uvuvi na uchimbaji madini.

Lakini hata shule zenye miundombinu mizuri ya madarasa na ya kutosha, kitaaluma zinafanya vibaya na mahudhurio ya wanafunzi ni mabaya.

Takwimu zinathibitisha. Shule ya Sekondari ya Mbangamao iliyoko kata ya Mbangamao ilipokea wanafunzi wa kutosha wa kidato cha kwanza mwaka 2001, lakini waliomaliza kidato cha nne mwaka 2004 ni saba tu. Madarasa matano hayana wanafunzi.

Mwaka 2005, Shule ya Sekondari ya Mkwaya ilichukua pia wanafunzi wa kutosha lakini waliomaliza kidato cha nne ilipofika mwaka 2008 walikuwa 10 tu. Shule hii pia ina ziada ya vyumba vya madarasa na walimu wa kutosha.

Ushahidi mwingine ni kwamba waliofanya mtihani wa darasa la saba katika shule ya msingi ya Darpori kata ya Mpepo mwaka 2008 walikuwa wanane tu; mwaka 2009 saba tu; mwaka 2010 shule haikuwa na wanafunzi waliomaliza elimu ya msingi, na mwaka 2011 ni wanafunzi 12 tu waliofanya mtihani.

Katika shule hii, wanafunzi wa madarasa mawili tofauti hukusanywa na kufundishwa katika chumba kimoja kwa zamu. Shule nzima ina vyumba vinne tu.

Kinachoshusha ari ya kusoma katika Shule ya Msingi Liwundi kata ya Liwundi ni shule kugeuzwa mahabusu. Chumba kilichopaswa kuwa ofisi ya walimu, sasa kinatumika kama mahabusu ya wahalifu au wakorofi.

Wanafunzi ambao ama kaka zao au mama zao au hata baba zao wanakuwa kwenye mahabusu shuleni hapo, hata kwa siku moja tu, hawawezi kutulia au kuzingatia masomo darasani.

Uamuzi huo ulifanywa na aliyekuwa  mtendaji wa serikali ya kijiji cha Mkili, ambaye sasa ni kaimu mtendaji wa kata ya Liwundi, Bosco Mapunda.

Katika Shule ya Msingi ya Ndingine, kata ya Ngumbo, uhaba wa miundombinu ya madarasa, umesababisha wanafunzi wanaoanza darasa la kwanza kukalishwa nje kwenye mbuyu. Ina maana hapo ndio darasa.

Kilio cha mkuu wa shule ya Mbangamao, Costica Mwang’omesi ni mwamko mdogo wa baadhi ya wazazi kwamba unachangia mahudhurio mabaya.

“Upo utoro wa wanafunzi kukosa vipindi, siku moja moja, mwezi na wa kudumu. Mwaka huu tu wanafunzi watano wameacha shule, hawakufanya mtihani wa kidato cha nne,” anasema Mwang’omesi.

Alichogundua, Mwang’omesi anasema ni wazazi wa wanafunzi hao kushindwa kutoa michango ya chakula,  kuishi kwenye mazingira yasiyoruhusu hali ya kujisomea nyumbani, umaskini pamoja na kuishi na wazazi au walezi wasio na mwamko wa elimu.

“Matatizo yetu ni uhaba wa walimu; mwalimu wa somo la sayansi yupo mmoja tu. Hatuna maabara, maji tunachota umbali wa kilomita moja tena kisimani, huduma ya afya, usafiri mgumu na hakuna umeme,” anasema.

Lakini anafurahi kwamba shule yake ina vyumba 16 vya madarasa na kati yake, vitano havitumiki. Vyumba vinne vinatumika kama madarasa; vitatu kama hosteli ya wasichana; kimoja hosteli ya wavulana; kimoja kama maktaba; kimoja kama stoo ya vifaa na kingine kama stoo ya chakula. “Vyumba ni vingi ila wanafunzi ni wachache,” anasema mwalimu Mwang’omesi.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Mkwaya, Anyandwile Mwasenga anasema wakati shule inaanza mwaka 2005 ilipangiwa wanafunzi 80 wa kidato cha kwanza, lakini waliripoti 50 tu. Mwaka huu ilipangiwa wanafunzi 51 lakini wameripoti 36.

“Mazingira ya shule ni kama unavyoona. Kuna majengo matano yenye vyumba vitatu vitatu na moja vyumba viwili. Viti na meza vipo vya ziada. Kuna wanafunzi 205 lakini kuna meza 372 na viti 265,” anaeleza Mwasenga.

“Utoro upo, na unasababishwa na mwamko mdogo wa kielimu wa wazazi na shughuli za kilimo. Baadhi ya wazazi huwatumia watoto kwenye shughuli za kilimo hasa kuvuna kahawa. Mwaka huu pekee tumefanikiwa kuwarejesha wanafunzi watatu watoro,” anasema.

Katika shule ya msingi ya Darpori, utoro umesababisha kubakiwa na wanafunzi 143 kutoka darasa la kwanza hadi la saba. Shughuli za uchimbaji madini ya dhahabu ndizo zinachangia wanafunzi kuacha shule kwa wingi.

Matatizo mengine kwa baadhi ya shule yanachangiwa kwa kiasi fulani na Idara ya Elimu ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kutofanya ziara kukagua maendeleo ya shule kitaaluma na ujenzi wa mejengo.

“Shule yetu haijawahi kupewa fedha zozote za ruzuku kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa madarasa,” analalamika Mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Ndingine, Aidan Millinga.

Ndingine inafanana kwa matatizo na shule nyingine za Ihanga na Litoromelo ambako walimu zaidi ya 30 wanaishi katika nyumba zilizoezekwa kwa nyasi. Baadhi ya wanafunzi huacha shule na kushiriki uvuvi kwenye mito Mdumbi, Chipindi na Ziwa Nyasa.

Ingawa baadhi ya shule ya sekondari kama Makita, Mbinga Day, Dk. Ali Shein, Ngumbo, Nanswea, Ngwilizi, Mbangamao, Mkwaya hakuna matatizo makubwa ya miundombinu, Idara ya Elimu ya Sekondari Wilaya ya Mbinga inakiri kuna matatizo mengine mengi.

“Kwa jumla kuna matatizo makubwa. Kuna uhaba wa walimu wa sayansi na vifaa. Kuna upungufu wa madarasa na maabara, wanafunzi kutojali elimu, wazazi kukosa mwamko na baadhi ya shule kuwa na wanafunzi wengi katika chumba kimoja,” anasema Kaimu Afisa Elimu Sekondari, Godfrey Mwakilembe.

Katibu Mtendaji wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Mbinga, Samwel Mhaiki anasema matatizo makubwa yanatokana na shule za sekondari kuanzishwa kisiasa. Mbinga ina shule 61 za sekondari zikiwemo 10 za binafsi.

Mhaiki anasema shule ni nyingi kuliko walimu. Waliopo wanafundisha vipindi vingi kuliko inavyotakiwa, lakini mishahara yao ni midogo sana, madaraja yanachelewa na wakipandishwa nyongeza zao zinachelewa. “Walimu hawana ari ya kufundisha,” anasema Mhaiki.

Aidha, Afisa Elimu wa Shule za Msingi anasema mahitaji ya vyumba vya madarasa kwa sasa ni 2,846 lakini vipo 2,036. Upungufu ni vyumba 810. Leja zinaonyesha kuna upungufu wa nyumba 1,748 za walimu. Kwa sasa zipo 1,065 tu.

Kitaaluma, Mbinga inajikongoja. Mwaka 2008 Mkwaya ilikuwa na wahitimu 10 tu kati yao wanane walipata daraja la nne wawili walifeli. Mwaka 2009 kati ya watoto 61 waliofanya mtihani, 32 walipata daraja la nne na 29 walifeli. Mwaka 2010 mmoja alipata daraja la tatu, 24 daraja la nne na 38 walifeli.

Matokeo katika shule ya sekondari Mbangamao, mwaka 2008 daraja la tatu walikuwa wanne, daraja la nne 44 na 30 walifeli; mwaka 2009 daraja la nne 31 na waliofeli 28; na mwaka 2010 daraja la tatu mmoja, daraja la nne 15 na waliofeli 84.

0789 383 979, jmwangul@yahoo.com
0
No votes yet