Mbinu ya CCM Igunga


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 21 September 2011

Printer-friendly version
Uchambuzi
Mgombea wa CCM, Dokta Kafumu

Siyo bure! Kuna kitu wanataka. Kuna mafao wanapata au wanategemea.

Balozi aliyekamatwa Igunga, Nghoboko Maselle, siyo peke yake. Wako wengi. Wanaitika amri. Wanabeba daftari na kalamu. Wanaorodhesha wananchi – majina yao, kadi zao za chama na shahada.

Serikali inajua haya. Kwa mfano, Maselle, mjumbe wa Nyumba Kumi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), anadai kuwa aliagizwa na mwenyekiti wa kijiji chake cha Mwayunge Mashariki katika Kata ya Igunga, kuorodhesha wapigakura.

Tume ya Uchaguzi inajua haya. Kila mwaka wa uchaguzi, uandikishaji huu hufanywa na CCM. Kila uchaguzi mdogo, uandikishaji huu hufanywa na chama hichohicho.

Serikali na hasa Tume ya Uchaguzi, huambiwa haya. Hakuna hatua ambazo huchukuliwa. Hapa ndipo wananchi hujenga shaka:
Kama orodha hizo hazikutumika kuongeza idadi ya siri ya wapigakura kwa mgombea husika.

Kama uandikishaji haukutumiwa kutisha wananchi.

Kama hawataambia waliojiandikisha kuwa wasipopigia kura chama chao, watajulikana tu na watachukuliwa hatua. Vitisho.

Kama orodha hizi hazitaweza kutumiwa kutoa ahadi. Kwamba walioorodheshwa, watapewa chakula kwa kuwa, kama ilivyo Igunga sasa, kuna upungufu wa chakula.

Kama orodha hazitatumiwa kutoa ahadi za kusomesha watoto au hata kutoa fedha za kuanzishia na kuendeshea vikundi vya uzalishaji vya akinamama na vijana.

Yote ni kutishia wananchi ili wawapigie kura. Utaratibu huu unafanikiwa zaidi katika mazingira ya umasikini na ambapo elimu ya uraia na elimu ya kupiga kura haijafika au haijeleweka vizuri.

Wananchi wanajua wanaoandikisha wanalipwa nini na kiasi gani. Wanajua nani waliwatuma. Wanajua daftari hupelekwa kwa nani; na huyo nani hupata nini. Wanajua.

Inawezekana wale ambao wamekuwa wakiorodheshwa kila uchaguzi unapowadia, wana lao la kusema, lakini hawajawahi kupata fursa ya kutoa maelezo.

Inawezekana wanajua ni nani hasa hunufaika au hunufaika zaidi kutokana na utaratibu huu wa kuorodhesha wenye shahada za kupigia kura.

Kisichojulikana ni kwa nini hawajitokezi kusema wanachojua. Je, wanalishwa kiapo? Wanatishwa? Vitisho ni vya aina gani?

Kuna wale ambao shahada zao hazijawahi kuorodheshwa, lakini wanajua nani anafanya nini na wapi. Nao wamekaa kimya kana kwamba wana mafao katika “biashara” hii. Huenda wanayo.

Hao wote ndio naongea nao sasa. Wenye gazeti wamenikubalia kuwa wiki ijayo ukurasa huu ni kwa wale wanaojua kinachotendeka katika kuandikisha shahada za wapigakura.

Kuna motisha gani kwa mtu mzima, kuchukua daftari na kalamu na kuanza kuandikisha wapigakura na shahada zao, huku ukijua kuwa Tume iliishafanya kazi yake ya kuwaandikisha?

Nasubiri maelezo yako.

0713 614872 ndimara@yahoo.com www.ndimara.blogspot.com
0
No votes yet