Mbinu za Magogoni zinavyojaribiwa majimboni


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 01 November 2009

Printer-friendly version

MALUMBANO kwa wadau wa uchaguzi Zanzibar yamefikia hatua mbaya.

Vyama vya upinzani hasa Chama cha Wananchi (CUF) vinaamini watu wapatao 170,000 hawatagusa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) na hivyo hawatapiga kura; matokeo yake itakuwa manufaa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho kwa Zanzibar, kinatajwa kupoteza kila uchaguzi tangu 1995.

Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi kinachotambuliwa na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar ya mwaka 1985 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2006, ndio kikwazo kikuu cha watu kuandikishwa.

Kifungu kipya kinaelekeza kuwa mtu anayetaka kuandikishwa mpiga kura, lazima awe na kitambulisho.

Si jambo tena la kuficha kuwa utoaji wake ni wa kibaguzi unaolenga kukidhi maslahi ya kisiasa ya chama tawala. Mfumo uliowekwa hautoi fursa na haki sawa kwa kila Mzanzibari kukipata.

Mfumo huo ulioandaliwa kwa ustadi ukishirikisha wataalamu wa idara mbalimbali za kidola, ni mpango maalum wa wakubwa kutaka ushindi mapema. Ni mpango “tunayemkubali aingie tusiyemkubali asiingie (na aliyemo atoke).”

Kwa njia hiyo, maelfu ya wenye haki watakuwa wameenguliwa katika daftari uandikishaji utakapokamilika. CUF wanakisia kuwa watu 170,000 watakuwa nje, wakiwemo wale waliopiga kura mwaka 2005 na kubaki na shahada zao.

Huu ndio ukweli. Ukizingatia yanayotokea vituoni na katika ofisi za Idara ya Usajili na Vitambulisho, unaona dhahiri wapangaji na watekelezaji hawaitakii nchi mema.

Kuueleza ukweli huu ni dhambi kwa viongozi wa serikali zote mbili – Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na ya Muungano pamoja na CCM. Wanachukia waonapo baadhi yetu tunayaeleza haya.

Ila kwa wakubwa hawa waliojipa uhalali wa kimungu wa kuongoza, waandishi wazuri ni wale wanaowafadhili na kuwapeleka Zanzibar na kurudi na taarifa za kupotosha au kuwasaidia.

Juzi tu tumesikia namna walivyomlisha maneno mwakilishi wa Gando, Said Ali Mbarouk, kwamba eti – pamoja na matatizo yote wanayopata wananchi katika kupata haki zao za kiraia zikiwemo kutafuta kuchagua na kuchaguliwa – amempongeza Mkurugenzi wa Idara ya Usajili na Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, Mohamed Juma Ame kwa kazi nzuri anayoifanya.

Idara hii iliyosheheni vijana wa Idara ya Usalama wa Taifa, inatuhumiwa kutengeneza mfumo wa kirasimu ambao tayari umethibitishwa na uzoefu kuwa hautendi haki. Ufuatiliaji wangu umebaini hata wengi wa wale waliosajiliwa na kupewa risiti, wataishia kukisikia tu kitambulisho.

Ukipitia mchakato wa usajili hadi kitambulisho kutoka, huwezi kukuta uovu. Ni kawaida ya kompyuta kukataa udanganyifu. Ila wanaotengeneza mfumo ndio wanaoutumia kudanganya kwa maslahi fulani. Takwimu ndio zinasuta wenye dhamira mbaya.

Fikiria mtu atafikaje kukata rufaa kwa mkurugenzi iwapo hakupata fomu ambayo lazima ipite kwa sheha? Masheha wanalalamikiwa kwa kuwa kikwazo; wenyewe wanajitetea “tunatekeleza maagizo ya wakubwa.”

Hawatoi fomu. Wakipewa cheti cha kuzaliwa kuthibitisha uhalali wa mtu, wanakivuruga ili kumtungia kesi mahakamani. Vipo vyeti vimevurugwa kwa kutiwa maandishi ya wino kwenye ofisi za umma wakati vimetolewa na ofisi nyingine ya umma. Uharibifu gani huu?

Nimesimuliwa kuwa viongozi wa CCM wa wilaya au majimbo ndio wanaosema “huyo mpe” na “huyo zuia.” Kijana mmoja alimtaja ofisa usalama kama ndugu yake na alipatiwa idhini kwenye tawi la CCM, ambayo alipoonyesha kwenye ofisi ya wilaya, alipewa haraka kitambulisho chake.

Hili ni zoezi lisilokwenda vizuri kiasi kwamba makundi ya wananchi – wakiwemo wenye shahada za kupigia kura – yanafika ofisi za idara hiyo katika jitihada za kutafuta kitambulisho lakini wanakwama.

Bado safari zao hizo hazimpendezi Mohamed na wakubwa zake, bali pia wanaziita ni mipango ya viongozi wa CUF kuhamasisha wananchi kufanya vurugu. Vurugu ili iweje? CUF wanadai wanaokataliwa ni wapigakura wao.

Nilibahatika kufika Ofisi ya Wilaya ya Magharibi (Meli Sita) baada ya kuarifiwa na msamaria kuwa amekuta kundi la watu na kubaini wanahangaikia kitambulisho baada ya kukwama mtaani. Wamekosa fomu kwa sheha watakataje rufaa kwa mkurugenzi?

Walikuwepo watu 300 hivi. Mmoja ni Time Juma Abdalla, mwanamke wa umri wa miaka 55 anayeishi Magogoni, mjini Unguja. Ana shahada ya kupigia kura Na. 220450008 iliyotolewa kituo cha uandikishaji jimbo la Mwakwerekwe, Aprili 2005.

Hajapata kitambulisho tangu 2006 na amechoka kumfuata sheha wake, Ahmada Othman. Time anadaiwa cheti cha kuzaliwa na kwa sababu hata chenyewe hajakipata kutokana na urasimu, ananyimwa fomu ya kukata rufaa kwa Mkurugenzi.

Ana watoto sita wa kupiga kura, lakini mmoja tu ndio ana kitambulisho. Watoto ni Juma (35), Fatma (32), Said (30), Ali (23), Khamis (20) na Ayoub (18). Wote baba yao ni Abdalla Ali, mume wa Time.

“Nimekuja tu mimi kwa sababu watoto wangu wamekata tamaa wanafanya shughuli zao maana tumehangaika sana,” anasema Time akilalamikia kuenguliwa na mfumo wa utoaji kitambulisho.

Hawakupiga kura katika uchaguzi mdogo wa Magogoni uliofanyika Mei. Hawataki kukosa uchaguzi ujao. Kiasi cha watu 1,800 walikosa uchaguzi huo kwa sababu ya mazonge. Kura 5,504 zilipigwa; mgombea wa CCM alitangazwa mshindi kwa tofauti ya kura 900 dhidi ya wa CUF.

Takwimu zinaonyesha vilitolewa vitambulisho vyapata 12,000. Wako wapi watu 7,000? Wamekufa? Au wamehama jimbo? Wakati huo hakukuwa na kinachoitwa “viongozi wa CUF wanazuia watu kujiandikisha.”

Wapo wanaojitapa leo kuwa walipiga kura Magogoni japo si wakazi wa jimbo hilo. Vijana wengi wa vikosi vya ulinzi waliandikishwa wakati jimboni kuna kambi moja tu ya Jeshi la Ulinzi (Missile), Welezo.

Mbinu zilizotumika Magogoni zinatekelezwa kwenye uandikishaji unaoendelea. Ni mfumo uleule wa “nani anatufaa tumuingize na nani hatufai tumzuie (atoke).”

Wanaotolewa ni pamoja na wale waliopiga kura 2005. Ni mfumo gani usiotambua wapiga kura waliopita? Tena katika daftari ambalo Tume ilisema lilihakikiwa na kukutwa zaidi ya 3,000 wameandikisha zaidi ya mara moja ambao haijulikani kwanini hadi leo hawajashitakiwa.

Mgogoro umeimarika. Vitisho vinatumika kuuzidisha. Viongozi wa CUF wanasema, “Tunakamilisha utaratibu ili kumshitaki Mohamed kwa madai ya kutokuwa mwaminifu na hivyo kukosesha wananchi haki yao.”

Yeye amekiri kuwa atashitaki viongozi wa Wilaya ya Chake Chake, iwapo hawatathibitisha kwa takwimu sahihi kuwepo watu 12,000 walionyimwa vitambulisho.

Wakati huohuo, wananchi wawili wanaendeleza utaratibu wa kuishitaki serikali mahakamani kupinga sheria inayoshurutisha kitambulisho ndipo mtu aandikishwe mpiga kura. Wanasema imevunja Katiba.

Wakati mgogoro ukichukua sura hiyo, tatizo linaendelea. Watu wanajitokeza majimboni kudai vitambulisho. Mkurugenzi anasema wametoa 515,000 Unguja na Pemba kufikia 29 Septemba. Wanaojitokeza hawanacho, ni mazimwi?

Ipo rai kwamba Mohamed apite majimboni aitishe majina ya vitambulisho alivyotoa. Itafumbua kitendawili na ukweli kujulikana. Amekubali kwa masharti kwamba “utaratibu huo ufuate sheria.” Vipi, haijulikani.

Serikalini hawajabadilika. Wanasema wanatekeleza sheria iliopo na kusisitiza mtu awe na kitambulisho ndipo aandikishwe vinginevyo “afuate sheria hiyo kukata rufaa.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: