Mbio za urais CCM na hatima ya Z’bar


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 23 June 2010

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

KATIKA kipindi ambacho macho na masikio ya wawakilishi wa kibalozi wa nchi za magharibi wanasema waziwazi wangependa kuona Wazanzibari wanaridhia mabadiliko ya mfumo wa kiutawala Zanzibar, inashangaza viongozi wenyewe wa Zanzibar wanajikongoja katika suala hili.

Ukiacha Rais Amani Abeid Karume ambaye mbali na kutamka kuunga mkono na kuhimiza wananchi kusema NDIYO ifikapo tarehe 31 Julai, mwaka huu, amekuwa akikemea wasaidizi wake katika chama na serikali upande wa Zanzibar, hakuna mwingine anayetaka kujitoa hadharani na kutamka hivyo.

Hakuna harakati za kukampeni hadharani zinazofanywa na serikali kuhusu kura ya maoni; wala Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) haijaeleza ratiba ya kuanza kwa kampeni ya kushajiisha wananchi ili washiriki kikamilifu katika kura hiyo.

Lakini kinyume chake, kuna taarifa zilizoenea kwingi kisiwani Unguja, na hasa katika mji wa Zanzibar, kwamba idadi kubwa ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiwemo mawaziri wa serikali ya Karume, wanafanya kampeni ya siri kutaka kuikwamisha kura hiyo.

Ndio kusema hawataki mabadiliko ya mfumo wa utawala yaliyoazimiwa; na uendelevu wa hali nzuri ya utulivu wa kisiasa iliyojengeka tangu rais alipokutana na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad tarehe 5 Novemba mwaka jana.

Uchunguzi unaonyesha kwamba hata baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, wanashiriki kampeni hiyo kwa kufanya vikao vya ndani katika matawi ya chama. Baadhi yo ni wenyeviti wa mikoa ambao moja kwa moja, kwa mujibu wa Katiba ya CCM, wanakuwa wajumbe wa Kamati Kuu.

Kampeni ya kutaka wananchi wapige kura ya HAPANA wakati ukifika, imeenezwa mikoa ya Kaskazini na Kusini Unguja, pamoja na sehemu kubwa ya mkoa wa Mjini Magharibi. Harakati za kushajiisha watu waseme HAPANA zinazoendeshwa katika maskani maarufu ya Kisonge, ni ushahidi wa wazi wa mkakati unaoenezwa na viongozi wa CCM dhidi ya kura ya maoni.

Wanasema suala la “kula mseto ni la hiyari siyo la kulazimishwa. Hapana, hapana.” Ni kitu cha ajabu katika siasa.

Pale serikali tena inayoongozwa na chama kimoja tu cha siasa inapopeleka sheria katika chombo cha kutunga sheria halafu viongozi wake wakaipinga. Ungetarajia wawe mbele katika kuiunga mkono hasa pale inapoonekana kama ni hatua muhimu katika kukomaza demokrasia.

Kura ya maoni ya Zanzibar inakusudiwa kuleta ufumbuzi wa kudumu wa matatizo ya kisiasa ambayo yamekuwa yakiisumbua Zanzibar kwa miaka mingi, na hasa baada ya kurudishwa kwa mfumo wa vyama vingi.

Rais Karume amekuwa akikemea watu wanaoipinga na anawashangaa kwamba hivi wanachokitaka ni kipi zaidi ya umoja na mshikamano wa dhati miongoni mwa wananchi; nyenzo muhimu sana kwa nchi yoyote inayotaka kupata maendeleo ya kweli ya kiuchumi na kijamii.

Kwa kutambua hilo, wawakilishi wan chi za Ulaya wamekuwa wakipigia debe mwelekeo mpya wa kujenga umoja na mshikamano Zanzibar kwa kuwa wanaamini ndiyo njia pekee ya kuiwezesha nchi kuendelea.

Balozi wa Sweden anayemaliza muda wake wa utumishi nchini Tanzania, Staffan Harrstrom amenukuliwa akisema wiki iliyopita kwamba ana matumaini makubwa kuwa dhamira ya kutatua mgogoro wa kisiasa Zanzibar kwa njia ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa itatimia kwa Wazanzibari kuikubali kura hiyo.

Mgogoro huo umekuwa tishio kubwa kwa utekelezaji mzuri wa mipango ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii Zanzibar na nchi wahisani zimekuwa zikieleza hasa masikitiko yao kuhusu mbinu za baadhi ya wanasiasa kutaka kuendeleza siasa za uhasama. Sasa wakati watu wakitafakari hilo, hali imeanza kujionyesha kwamba ni kweli kuna viongozi wasiotaka mafanikio ya kura hiyo kwa maana ya kuipitisha kwa kuiunga mkono.

Makada saba wa CCM waliojitokeza Jumatatu kutafuta ridhaa ya chama chao ili kugombea nafasi ya urais wa Zanzibar wamezunguka sana kuhusu suala hili ambalo limekuwa ndio la msingi kwa kila anayetaka kugombea nafasi hiyo. Hawataki kusema waziwazi kama wanaunga mkono kura ya NDIYO; wanajizungusha wee kabla ya kusema wanataka umoja na mshikamano.

Lakini Dk. Hamad Bakari Mshindo, kada mtaalamu wa lugha ya Kiswahili na Kiingereza aliyechukua fomu na kutangaza wazi kuwa ametokana na mifupa hasa ya chama tangu akiwa na miaka minane mwaka 1957 wakati huo ASP, anasema serikali ya umoja ilikuwepo tangu baada ya mapinduzi. Kwake, anasema, serikali hiyo huundwa kwa kuzingatia maeneo yote ya nchi, hata kama ni ya chama kimoja kilichoshinda uchaguzi.

Shamsi Vuai Nahodha, Balozi Ali Karume, Ali Juma Shamhuna, Dk. Hamad Bakari Mshindo, Dk. Mohamed Gharib Bilal, Dk. Ali Mohamed Shein na Mohamed Aboud Mohamed, wamechukua fomu kutaka ridhaa ya chama chao ili wagombee urais kupitia CCM.

Wote walisema wanapenda umoja na mshikamano lakini ikawa shida kwao kutamka moja kwa moja kwamba wanaiunga mkono kura ya NDIYO itakapokuja 31 Julai. Na angalau Dk. Shein, makamu wa rais wa Tanzania, mzaliwa na kisiwani Pemba, baada ya kuzunguka kama vile akitaka kukwepa kuwa wazi, alisema msimamo alioutoa Rais Jakaya Kikwete, kuwa CCM imeona serikali ya umoja wa kitaifa ndiyo njia nzuri ya kuleta utulivu kamili Zanzibar ni wa chama ambao lazima aufuate.

Balozi Karume amekuwa akieleza wazi kwamba serikali ya umoja wa kitaifa ndilo suluhisho la kudumu la mgogoro wa kisiasa Zanzibar. Anasema ameona hivyo kwa muda mrefu na alitarajia serikali kama hiyo ingeundwa tangu baada ya uchaguzi wa mwaka 2000.

Dk. Bilal, mzaliwa wa Zanzibar aliyetumikia uwaziri kiongozi kuanzia Oktoba 1995 mpaka Oktoba 2000, alisema anaipenda Zanzibar, na amekusudia kuijenga upya, lakini kwa kura ya maoni anasema, “Nitasubiri maamuzi ya wananchi. Watakachosema nitafuata na mimi nitapanua maridhiano yawe kwa wazanzibari wote.” Shamsi hajasema hasa anaunga mkono kura ipite.

Mara kadhaa amekuwa akihimiza wananchi kupendana na kufanya kazi kwa ushirikiano, lakini alipokuwa akifanya majumuisho ya hotuba ya makadirio ya matumizi ya bajeti ya ofisi yake katika Baraza la Wawakilishi wiki iliyopita, alijizuia kusema angependa kura ya NDIYO.

Alisema hasa kwamba asingependa kutamka hivyo kwa sababu amezungumzia suala la kura ya maoni mara tatu na kubaini kwamba matamshi yake yamewatia hofu. “Sasa sitaki kusema tena ieleweke tu kwamba hatuwezi kuishi katika mifarakano isiyokwisha,” alisema.

Mohamed Aboud Mohamed, naibu waziri katika serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu baada ya uchaguzi mkuu wa 2005, baada ya kuwa waziri tangu 1995 katika serikali ya mapinduzi Zanzibar, amekuwa akihimiza maelewano kwa Wazanzibari. Aboud ambaye ni mzaliwa wa Pemba, aliwahi kuwa mwakilishi wa Wawi kabla ya kuteuliwa na Rais Kikwete kuwa naibu waziri.

Iwapo CCM inaleta mbele wagombea wanaojivuta katika kukubali kura ya maoni itakuaje kura hiyo itakapokuja? Hili ndilo swali muhimu linaloulizwa na wananchi kwa sasa. Wengine wanaamini mgombea wa CCM ndiye atakayetoa dira iwapo kweli Zanzibar imejiandaa na mabadiliko. Muda utaamua hatima ya Zanzibar.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: