Mbowe sasa acharuka


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 19 August 2008

Printer-friendly version
Kuburuza kortini wanaomchafua
Yumo anayesambaza disketi chafu
Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa CHADEMA

CHAMA  cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kina mpango wa kushitaki magazeti manne nchini kwa kumhusisha mwenyekiti wake, Freeman Mbowe na kifo cha aliyekuwa mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe.

Magazeti yaliyoko kwenye orodha ya kushitakiwa ni Rai, Mtanzania (yote ya kampuni ya New Habari Corporation), HabariLeo na Majira.

Mwingine anayeshitakiwa ni mwandishi wa taarifa iliyomuhusisha Mbowe ambaye jina lake halikuandikwa bali kulikuwa na “Mwandishi Wetu.”

Moja ya magazeti yanayoshitakiwa, Mtanzania liliandika kwenye ukurasa wake wa kwanza chini ya kichwa cha habari “Mbowe asherehekea kifo cha Wangwe,” kuwa akiwa Afrika Kusini, Mbowe alisherehekea alipopata taarifa za kifo cha Wangwe.

Taarifa za uchunguzi wa MwanaHALISI zinasema yule aliyejiita “Mwandishi Wetu” kwenye taarifa inayolalamikiwa, ni mmoja wa viongozi serikalini.

Gazeti hili lina jina la anayedaiwa kuandika habari inayolalamikiwa na kuisambaza kwa magazeti husika, lakini linalihifadhi kwa sasa.

Imeelezwa kwamba mhariri wa moja ya magazeti yaliyopelekewa taarifa inayolalamikiwa, tayari amekiri kuipokea na ameeleza chanzo chake kinyume na makubaliano ya awali.

Mkurugenzi wa sheria wa Chadema, Tundu Lissu amethibitishia gazeti hili kuwepo mpango wa kushitaki magazeti haya.

“Uamuzi tayari umechukuliwa. Hivi sasa ninakwenda kwenye kikao cha mwisho cha maamuzi kuhusu suala hilo,” alisema Lissu juzi Jumatatu jijini Dar es Salaam.

Magazeti ya Mtanzania na Rai yanamilikiwa na Rostam Aziz, Mbunge wa Igunga na mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM ambaye uongozi wa Chadema ulimweka kwenye orodha ya watuhumiwa wakuu 11 wa ufisadi nchini.

HabariLeo, dada yake gazeti la Kiingereza la Daily News, linamilikiwa na serikali. Gazeti hilo pia liliandika habari hiyo kwa urefu.

Gazeti la Majira linamilikiwa na kampuni ya Business Times Ltd., ya Dar es Salaam ambayo pia inachapisha magazeti ya Dar Leo na Business Times.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: