Mbunge asiyesita kukomalia TICTS


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 23 June 2009

Printer-friendly version
Ana kwa Ana

ERNEST Mabina, mbunge wa Geita (CCM) mkoani Mwanza, ni miongoni mwa wabunge wachache wanaoweza kusema kile wanachokiona na bado wakabaki na msimamo huo hadi mwisho.

Katika mahojiano na MwanaHALISI wiki hii, katika hoteli ya Baraza la Kikristo la Tanzania (CCT) mjini Dodoma, Mabina pamoja na mambo mengine, analia na kampuni ya Kupakia na Kupakua Mizigo bandarini Dar es Salaam (TICTS).
 
Anasema haridhishwi na kimya cha serikali katika kushughulikia mkataba huo. “Kampuni ya TICTS haina maslahi kwa taifa. Ni wajibu wa serikali kuiondoa mara moja.”

Anasema mkataba wa TICTS na serikali ulihusu kazi ya kupakua mizigo, lakini TICTS wamejipa jukumu jingine la kuitunza mizigo hiyo.

“Hii kazi waliyojipa ina kipato kikubwa kuliko ile ya mwanzo, na kwamba wanaifanya bila mkataba na serikali. Lakini serikali imeamua kuendelea kufumbia macho jambo hili. Hili halikubaliki,” anafafanua.

Jumanne iliyopita, wakati akichangia hotuba ya bajeti ya serikali iliyowasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, Mabina alilizungumzia jambo hili hadi kuzusha zogo kati yake na Mwenyekiti wa Bunge, Job Ndugai.

Ni kutokana na hatua ya Mabina ya kutaka kuhoji mbunge mmoja mmoja juu ya uhalali wa mkataba kati ya serikali na TICTS.  Ndugai alisema, hatua ya Mabina kuhoji wabunge ni kwenda kinyume na Kanuni za Bunge kwani alidai jukumu hilo ni la spika peke yake.

Hata hivyo, wakati Ndugai anamzuia Mabina kuendelea na zoezi lake la kuhoji wabunge, Mabina alishawahoji, “Je, wabunge mnaukubali mkataba huu?” Wengi waliitikia, “Hapana!”

Amepata wapi ujasiri huu? Mabina najibu, “Sijui. Lakini kikubwa ni kwamba nimeingia bungeni kwa ajili ya maslahi ya wananchi. Katika hili, sina wa kumuogopa. Nimeamua kusimamia maslahi ya wananchi,” anasema.

Wilaya ya Geita ina majimbo matatu ya uchaguzi, ambayo ni Geita, Nyang’wale na Busanda. Jimbo la Nyang’wale linawakilishwa na James Musalika na mbunge wa sasa wa Busanda, ni Lolensia Bukwimba.

Wabunge wa majimbo haya wanafanya kazi kwa pamoja. Geita inasifiika kwa utajiri wa rasilimali na watu. Ina wakazi zaidi ya milioni moja na inaongoza kwa utajiri wa madini, hasa dhahabu.

Hata hivyo, Mabina anasema bado Geita iko nyuma kimaendeleo. Hakuna umeme wa uhakika wala maji safi na salama.

“Geita bado haijaunganishwa na gridi ya taifa. Umeme unachochea maendeleo. Geita kwa maana ya Busanda na Nyang’wale, hakuna umeme. Umeme umeishia Kasame. Naamini kama Geita mzima ingemulikwa na umeme wa gridi ya taifa, basi umasiki wa wananchi ungepungua,” anasema.

Kwa upande wa maji, Mabina anasema maji yaliyopo katika Ziwa Viktoria bado hayajawanufaisha wananchi wa Geita; serikali imepeleka maji hadi Shinyanga, lakini haijapeleka Geita.

Si Geita tu, hata Misungwi, Tarime, Bunda na Sengerema, maji haya hayajafika. Hatua hii imewachukiza wananchi wetu. Wao wanaona kama vile “wamezaa lakini wanakatazwa kunyonyesha mtoto waliyemzaa,” alisema

Anasema wananchi wa jimbo lake wanakabiliwa na hatari kubwa ya kupata maradhi ya matumbo kutokana na kutumia maji ya visima ambayo hayana uhakika wa moja kwa moja kwa usalama wa afya zao.

Kuhusu elimu, anasema hapo angalau kuna maendeleo kwa maana ya shule za kutosha ukilinganisha na huko nyuma.

Kwa mfano, Mabina anasema, mwaka 2000, kabla ya yeye kuingia bungeni, wilaya mzima ya Geita ilikuwa na shule tisa, ambapo kati ya hizo sita za serikali na tatu zilikuwa zinamilikiwa na Bodi ya elimu ya mkoa. Sasa kuna shule 48 zote zikiwa za serikali.

Anataja baadhi ya shule zilizopo katika jimbo lake kuwa ni Geita, Kivukoni, Kalangalala, Geita Sekondari, Shule ya Wasichana Nyumkumbu na Kwantolole. Baadhi ya kata zina zaidi ya shule moja. 

Kama ilivyo kwa mikoa mingine, Geita inakabiliwa na uhaba wa walimu huku baadhi ya walimu wakiwa hawajalipwa marupurupu yao kwa muda mrefu.

“Kwa kipindi kirefu, walimu wamekuwa wakichezewa kwa kukaa muda mrefu bila kupandishwa madaraja, wengi wanalazimika kusafiri umbali mrefu kufuata mishahara yao, mambo ambayo yanayochangia kurudisha nyuma morali wao wa kazi,” anasema.

Kuhusu barabara, Mabina anasema kuna matumaini kutokana na hatua ya serikali kumaliza ujenzi wa barabara ya lami kutoka Kyamnyorwa, Buzilayombo hadi Geita.

Anataja barabara nyingine zinazojengwa kuwa ni pamoja na ile inayotoka Nyehunge-Nzela hadi Nkome. Barabara nyingine ni ile inayotoka Nzela hadi Geita mjini ambayo ipo chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia (WB).

Ernest Gakeya Mabina, alizaliwa mwaka 1954 katika kijiji cha Isulwabutundwe, kata ya Lubanga, tarafa ya Kasamwa, wilayani Geita, mkoani Mwanza.

Alisoma elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Busilasonga kutoka mwaka 1966 hadi 1972 alipojiunga na Shule ya Sekondari Bwiru. Alihitimu kidato cha nne mwaka 1976.

Kutoka Bwiru, Mabina alijiunga na Shule ya Sekondari ya Shycom iliyopo Shinyanga ambako alihitimu mwaka 1978. Mwaka 1982 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ajili ya shahada ya uchumi. Alihitimu mwaka 1985.

Kati ya mwaka 1980 hadi 2000 aliajiriwa katika Ofisi ya Rais akiwa kama Mhasibu Msaidizi. Aliacha kazi serikalini mwaka 1987 na kujishughulisha na biashara.

Mwaka 2000 alijitumbukiza katika kinyang’anyiro cha ubunge ambapo alimshinda aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Ezekiel Malogoi Manyanya ambaye alikuwa mbunge wa Geita kati ya mwaka 1995 hadi 2000.

Mabina meshika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Jumuiya ya Vijana (UV-CCM). Hadi sasa ni Kamanda wa UV-CCM wilaya ya Geita.

0
No votes yet