Mbunge CCM apinga uteuzi wa JK


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 13 June 2012

Printer-friendly version

MBUNGE wa Mbozi Mashariki (CCM), Godfrey Zambi amepinga uteuzi wa mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete.

Amepinga pia uteuzi wa baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi na kile alichoita “utungwaji kanuni za zao la kahawa bila kufuata taratibu.”

Februari mwaka huu, rais alimteua Dk. Eve Hawa Sinare kuwa mwenyekiti wa TCB; hatua iliyofuatiwa na waziri wa kilimo (wakati huo Prof. Jumanne Maghembe) kuteua wajumbe wa bodi.

Hivi sasa Prof. Jumanne Maghembe ni waziri wa maji.

Katika barua ambayo Zambi amemwandikia Waziri wa Kilimo, Christopher Chiza, ambayo MwanaHALISI imeona, mbunge huyo anachambua  mjumbe mmoja baada ya mwingine na kusema hawakupatikana kwa uwiano wa kikanda.

Zambi anasema katika barua yake kwamba Dk. Sinare “hafai kuwa mwenyekiti wa bodi” kutokana na kuwepo kwa mgongano wa kimaslahi.

“Naomba ieleweke kwamba, Dk. Eve Hawa Sinare, mwanasheria wa kampuni ya uwakili ya Rex Attorneys, ndiye alipewa kazi na Benki ya NMB kwa ajili ya kulipiga mnada jengo la Kahawa Moshi (ofisi kuu ya TCB). Hadi sasa jengo hilo lina mgogoro,” anaeleza Zambi.

Anasema, “…inashangaza kumteua mtu ambaye amepewa kazi ya kulipiga mnada jengo hilo…kuwa mwenyekiti. Atakwepaje mgongano wa kimaslahi?”

Zambi anasema ana uhakika Rais Kikwete “amedanganywa” kuhusu mteuliwa wake. Anasema Dk. Sinare hawezi kutetea maendeleo ya Bodi kama mwenyekiti; na wakati huohuo kusimamia uuzwaji wa jengo ambamo ndipo zilipo ofisi kuu za TCB.

Anamshauri waziri Chiza amshauri rais kutengua uteuzi wa Dk. Sinare ili kuitendea haki bodi ya wakurugenzi; na menejimenti ya Bodi ya Kahawa iweze kufanya kazi kwa uhuru zaidi.

Barua ya Zambi ya 4 Juni 2012, imenakiliwa kwa Rais Kikwete, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro.

Wajumbe wa bodi ambao kuteuliwa kwao kumepingwa na Zambi, ni pamoja na mhandisi mstaafu wa maji, Miraji Omari Msuya.

Zambi anasema uteuzi wa Msuya  haukuzingatia sheria kwa sababu hajulikani anawakilisha kundi gani.

Mjumbe mwingine ni mwanasheria na mwenyekiti wa kampuni ya Lima anayosema inahusika na ununuzi wa kahawa, Eric Ng’maryo.

Anadai vyama ambavyo vinatambuliwa na vinaweza kuwakilishwa kwenye bodi ni Tanzania Coffee Association na Association of Coffee Growers, lakini siyo Lima anakotoka Ng’maryo.

Zambi ameituhumu pia Lima “kushawishi wakulima kuuza kahawa mbichi (mbivu) au red cherry kwa bei ndogo sana.”

Kuhusu Prof. James Teri, ambaye ni mtendaji mkuu wa Taasisi ya Uchunguzi wa Kahawa (TaCRI), Zambi anasema “Taasisi yake siyo ya serikali na hivyo kumteua mtendaji wake mkuu kwenye bodi kama mwakilishi wa serikali, si sahihi hata kidogo…”

“Mheshimiwa waziri, sababu nyingine kubwa ya kupinga uteuzi wa wajumbe wa Bodi ya Kahawa ni kutozingatia uteuzi wa wajumbe kwa kuzingatia maeneo makubwa ya uzalishaji kahawa nchini,” anaandika Zambi katika barua ya kurasa nane.

Anataja kanda ya Kaskazini, yenye mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Tanga; Mbinga (mkoani Ruvuma), Mbeya, Kagera, Kigoma na Tarime (mkoani Mara), kuwa ndiyo maeneo makubwa ya uzalishaji kahawa.

Analalamika kuwa Mbeya ambako inalimwa kahawa nyingi, hawakupata mwakilishi kwenye bodi.

Anasema, “…inashangaza sana kuona kwamba kati ya wateuliwa wote kumi (10) kwenye Bodi, watano (5) wanatoka mkoa mmoja wa Kilimanjaro…”

Tuhuma za upendeleo kwa misingi ya ukanda, ziliwahi kutolewa mwaka jana wakati wa mkutano wa bajeti.

Zilikuwa zikilenga aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo. Alikuwa  akidaiwa kuwa chanzo cha watu kutoka sehemu moja kujazana idara ya wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii iliyokuwa ikiongozwa na Waziri Ezekiel Maige.

Kabla ya kwenda ikulu kuwa katibu mkuu kiongozi, Luhanjo alikuwa Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Alihamia huko akitokea Wizara ya Maliasili na Utalii anakodaiwa alishawishi uteuzi wa watendaji kwa misingi ya ukabila katika Idara ya Wanyamapori.

Aidha, kanuni mpya za zao la kahawa ambazo Zambi anadai kupinga ni zile zilizojadiliwa kwenye mkutano wa wadau wa kahawa tarehe 24 na 25 Mei mwaka huu, mjini Morogoro.

Zambi anadai mkutano wa Morogoro uliambiwa kuwa kanuni mpya tayari zimesainiwa na waziri husika tangu 18 Aprili mwaka huu.

“Mheshimiwa waziri, napenda ufahamu kuwa kanuni hizo zimwetungwa kinyemela kwa sababu wadau wa kahawa hawakushirikishwa kabisa,” anaeleza Zambi.

Anadai kuwa kikao cha TCB mjini Moshi mwaka 2011, ambacho inadaiwa ndiko zilitungiwa kanuni, hakikuwa na ajenda hiyo na kwamba yeye mwenyewe alikuwepo.

Anasema, hata hivyo, kikao hicho hakikuwa cha wadau kwani kilikuwa cha wajumbe 30 tu. Amemweleza waziri kuwa kikao cha wadau kina wajumbe zaidi ya 200.

Zambi anasema hajaona kanuni hizo lakini anadai “…zitakuwa kanuni mbaya. Kanuni ambazo hazina faida kwa mfanyabiashara.”

Akiandika kwa niaba ya  “Wanambeya (wakulina wa kahawa),” anasema wana imani na waziri.

“Tunatumaini masuala haya mawili mazito sana, moja uteuzi wa wajumbe wa bodi bila kufauta sheria na utungwaji kanuni za zao la kahawa bila kufuata taratibu, utayafanyia kazi kama ambavyo nimeshauri,” anahitimisha barua yake.

0
No votes yet