Mbunge Kilasi atambia ripoti ‘feki’


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 28 July 2010

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli
Estherina Julio Kilasi

NILIBAHATIKA kusoma na kuipitia kwa kina ripoti ya miaka minne iliyoandaliwa na Mbunge aliyemaliza kutumikia Jimbo la Mbarali bunge lililokwisha, Estherina Julio Kilasi.

Mtu yeyote akipata fursa ya kuisoma ripoti ile na akaenda halmashauri kusoma vitabu vya ripoti ya maendeleo, atagundua kitu.

Atagundua kwamba hata mbunge alifunga safari hadi ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mbarali, George Kagomba, akaomba vitabu vya taarifa ya maendeleo ya wilaya, akasoma na kuchukua takwimu humo.

Takwimu hizo, ambazo mwaka jana zilitumiwa pia na Umoja wa Wakazi wa Mbarali Waishio Dar es Salaam kwa ajili ya kuandaa harambee, zinaonyesha mikakati ya halmashauri ya wilaya na mafanikio katika ujenzi wa miradi ya shule, zahanati, vituo vya afya, usambazaji wa maji, uboreshaji wa miundombinu ya barabara na ya ustawi wa jamii kwa ujumla.

Halmashauri imeainisha, katika kila mradi, kiasi cha pesa kilichotumika na kinachohitajika kukamilisha kazi, kupanua au kuanzisha miradi mingine.

Mbunge alifungua baadhi ya kurasa, akanukuu takwimu alizozihitaji na kuzitumia katika ripoti aliyoita “Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi; Desemba 2005-Juni 2009.

Kama mwanafunzi anayetazamia majibu kutoka kwa wenzake, na pengine akihisi kuwa angesutwa, ripoti yake aliacha isomeke Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali; Taarifa ya miradi ya maendeleo kwa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (Mmem) toka mwaka wa fedha 2005/06-2008/09.

Kwa kuwa amechukua ripoti ya halmashauri na kuitegemea kwa kiwango kikubwa alipoandaa ripoti yake, ripoti aliyoitoa imetokea haina mchango wake na haikujadili mambo kadhaa aliyopaswa kuyaelezea kama mbunge aliyemaliza kutumikia ubunge.

Mambo mengi katika taarifa yake yametajwa kijuujuu bila ya kuambatana na maelezo ya kina ili kuonyesha uhalisia wa masuala mbalimbali jimboni.

Kwa mfano, katika sehemu ya pili ya ripoti hiyo ya miaka minne kuhusu wajibu wa mbunge, amesema katika kipindi cha 2005-2009 kumekuwa na mafanikio mengi katika utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM.

Anasema amefanikiwa: Kuhamasisha wananchi kuchangia na kujiletea maendeleo; kushawishi serikali kuu ielekeze nguvu zake katika Jimbo la Mbarali; mwenyewe kama mwananchi kuchangia vifaa na pesa katika miradi mbalimbali kuunga mkono juhudi za wananchi; kuandika miradi ya maendeleo na kutafuta wafadhili; na kutoa ushauri na mwongozo kwa wananchi katika kutekeleza yale yote waliyojipangia.

Hata hivyo, taarifa haionyeshi ni ipi miradi ya maendeleo aliyoandika na wafadhili aliowatafuta. Pia hakuonyesha alivyofanikiwa kushawishi serikali kuu kuelekeza nguvu zake jimboni Mbarali.

Katika kipengele cha maji, ameeleza kwenye taarifa yake kwamba Mbarali hakuna tatizo la maji.

“Kwa sasa maeneo yenye kero ya maji yamepatiwa visima virefu vyenye uwezo wa kuhudumia watu 10,000. Tatizo hilo la maji wilayani Mbarali limepungua kwa kiasi kikubwa sana kama siyo kwisha kabisa,” anasema. Kwa mujibu wa sensa iliyopita, Mbarali ina wakazi 282,911.

Mbarali isiyo na matatizo ya maji haipo na kama ipo basi si hii iliyopo mkoa wa Mbeya. Hata mtu akipita barabarani – acha maeneo ya mbugani – kuanzia Igawa hadi Igurusi, ataona watu wakihangaikia maji mbali, na hasa kwenye mito na mabwawa.

Aidha, ripoti hiyo ambayo hata madiwani wameiponda kwa kukosa uhalisia, imejaa takwimu za matumizi ya pesa pasina kutaja vyanzo vyake; labda ni ruzuku kutoka serikali kuu au michango ya wananchi.

“Katika kipindi cha mwaka 2005 hadi sasa, Sh. 548,871,800 zimetumika katika miradi mbalimbali ya maji katika kata mbalimbali wilayani Mbarali,” inasema ripoti ya Kilasi.

Ameendelea kutaja kiasi cha pesa kilichotumika mwaka hadi mwaka. Kwa mfano, anasema kati ya mwaka 2005 na 2006 zimetumika Sh. 15 milioni; na 2008/2009 Sh. 192,133,300 zilitumika katika miradi ya maji kata za Ubaruku, Chimala, Rujewa, Igurusi na Madibira.

Kwa upande wa elimu, amesema katika kipindi cha 2005-2006 zilitumika Sh. 375,355,000 katika miradi ya elimu ya msingi. Ikiwa kuna mahali pesa hizo zinatoka na yeye kazi yake ni kuandika tu ripoti, uko wapi mchango wake?

Ripoti ina mchanganuo mzuri wa matumizi ya pesa hizo katika kujenga madarasa, nyumba za walimu, vyoo, ofisi na kununua madawati lakini hakutaja wapi pesa hizo zimetoka; ni nguvu za wananchi au mchango wa halmashauri.

Mathalani, mwaka wa fedha 2005/2006 anasema Sh. 105,100,000 zilitumika; mwaka 2006/2007 Sh. 64,525,000 zilitumika kwa madarasa, nyumba za walimu, vyoo, ofisi na madawati. Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali hupata ruzuku isiyopungua 3,260,279,566.

Hii ni moja ya kasoro kubwa za ripoti, na ni rahisi kuamini kwamba “ametengeneza” ripoti. Anaweza vipi kukumbuka pesa zilizotumika bila ya kutaja vyanzo vyake? Ni wapi anatambua nguvu za wananchi? Hivi amesahau hata kueleza halmashauri ilivyoanza kupata ruzuku baada ya miaka kadhaa ya kupewa hati chafu?

Ameshindwa pia kueleza kama tatizo la uhaba wa madarasa au wa shule limetatuliwa kwa kiasi gani.

Kuhusu elimu ya sekondari, ameshindwa siyo tu kutaja shule zilizojengwa bali hata kiasi cha pesa kilichotumika na kampeni zilizopo za kujenga shule za sekondari za elimu ya juu (A level) kutoka miongoni mwa shule 15.

Hadi kufikia mwaka jana, Mbarali ilikuwa na shule za msingi 103 na shule za sekondari 18 zikiwemo tatu za binafsi. Shule sita za sekondari za serikali kati ya shule 15 zimejengwa kipindi cha 2005-2009.

Katika hali ya kufunikafunika mambo, mbunge anatamba kwamba amechangia pesa kwa ajili ya kujenga miradi ya shule. Mbona hataji kiasi alichochangia, kwa mradi upi wa shule na lini.

Anasema: “Aidha katika mafanikio haya, mimi mheshimiwa mbunge mwenyewe nimekuwa nikichangia vitu mbalimbali kama vile saruji, bati, vitabu na fedha kwa kila sekondari.”

Inakuaje ameshindwa kuainisha katika ripoti yake – angalau hii niliyoisoma – mchango wake ni upi na katika mradi gani. Pengine nafsi imemsuta angetaja mradi wa shule fulani au maji au zahanati, wanajumuiya husika yaani wanafunzi, walimu na wazazi wa eneo husika wangemkana.

Mtu yeyote akisoma ripoti hiyo anagundua haraka kuwa mbunge ametia saini tu baada ya ripoti kukamilishwa na mtu mwingine ambaye hakuijua kazi hasa aliyofanya mbunge, ndiyo maana anajinasibisha kwa kuandika “mimi mheshimiwa mbunge….”

Hivi kuna ulazima au Kiswahili kinahitaji msisitizo huo? Hivi ukisema ‘mimi’ nikishirikiana na viongozi, madiwani neno mimi litakuwa na maana nyingine zaidi ya yule anayesema? Ayi, ayi Kilasi!

Kilasi anapaswa kukaza msuli wa kampeni kwani tofauti na miaka ya nyuma, safari hii anakabiliwa na mambo mawili: kushuka kwa imani ya wapigakura juu yake na kuibuka kwa washindani wenye mvuto kutaka kuteuliwa kugombea.

Washindani wake ni kamanda wa vijana wa wilaya Injinia Burton Kihaka; mwanasheria wa kujitegemea Dk. Ronlick Mchami; mwanasheria Idd Mtiginjola; mkurugenzi wa fedha katika Taasisi ya Elimu Tanzania (TET/TIE), Fred Sichizya; katibu wa CCM, Emmanuel Mteming’ombe; Dk Suleiman Kimatha; diwani Kilufi na mchumi Geofrey Mwangulumbi.

Kila mwanachama anayeomba kuteuliwa na chama kuwa mgombea ubunge ana malengo yake kwa ajili ya jimbo hilo.

Kwa mfano, Mwangulumbi anasema: “Natambua historia ya Bonde la Usangu na shauku kubwa ya wananchi kutaka mbunge wa kuwatumikia ili wajiletee maendeleo kwa haraka kwa kutumia rasilimali mbalimbali walizojaaliwa na Mwenyezi Mungu jimboni.”

Mkakati wa Mwangulumbi ni kuhakikisha wananchi wanatekeleza mpango wa Kilimo Kwanza kwa ufanisi halafu kuunda mfumo mzuri wa soko la mazao yao hasa mpunga unaolimwa kwa wingi wilayani Mbarali.

“Ni kusudio langu kushirikiana nao kuunda mfumo wa soko ambao utawaondolea adha ya kila miaka kulima mpunga na kisha kukosa soko. Naam, inawezekana kabisa kutumia kilimo cha mpunga kufanya mapinduzi ya kilimo bila ya kunyonywa na makabaila wala walanguzi.”

Mwangulumbi anatazama mbali: “Soko la Jumuia ya Afrika Mashariki ni kichocheo kingine, muhimu hapa ni kujenga hoja ya msingi kwamba sehemu yoyote yenye njaa ndiyo iwe soko la mpunga kutoka Bonde la Usangu. Kwamba Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) au Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) wanapotaka kununua chakula huenda barani Asia na kukileta Afrika kwenye njaa. Tunataka wabadili fikra ili sasa waje kununua nchini Tanzania na iwe ni chakula kilicholimwa Bonde la Usangu.

“Marais walikaa Rome, Italia wakapewa tafiti kwamba dunia inakabiliwa na baa la njaa, lakini wakati huo huo maeneo ya Madibira, Chimala (Kapunga), Ipatagwa nk mpunga unaoza kwa kukosa soko. Mfumo wa soko hauwezi kufanikiwa kama mfumo wa fedha haujakamilika.

“Inawezekanaje uchumi wa Mabadaga, Uturo, Mbuyuni, Chimala, Igurusi, Ihahi, Utengule, Ilongo, Igalako, Ruiwa uendelee bila ya kuwepo benki!” Hiyo ni hoja nyingine anayopanga kusimamia utekelezaji wake akichaguliwa mbunge.

Mwangulumbi anajali michezo na utamaduni, maeneo yaliyo nyuma sana Mbarali. Kubadilisha hali, anasema: “Inawezekanaje kuendelea kimichezo wakati utamaduni wetu tumeudharau, ngoma zote nzuri zimeachwa na hata michezo ya mpira, viwanja vimekuwa masoko na vimejaa vichuguu?

“Huu ni wakati wa kufufua michezo yote na kuboresha viwanja kwa mfumo wa kisasa. Tunaweza kupiga hatua za maendeleo katika nyanja hii na nyinginezo kwani baada ya wananchi kupata mfumo wa uhakika wa soko la mazao wanayolima, watapata uwezo wa kuchangia ujenzi wa shule, zahanati, miundombinu ya maji na wenyewe watajijengea nyumba bora.”

Mwandishi wa makala hii amejitambulisha ni mwenyeji wa jimboni Mbarali. Kwasababu binafsi ameomba jina lake lisichapishwe gazetini.
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: