Mbunge Lembeli aingizwa mkenge


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 28 July 2010

Printer-friendly version
James Lembeli

MBUNGE wa Kahama anayetetea kiti chake, James Lembeli, amesema hatua ya kutangaza “jimbo feki” wilayani kwake, imelenga kumwangamiza kisiasa.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Kahama, Sospeter Nyigoti alitangaza wiki iliyopita kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekubali kugawa jimbo la Kahama na hivyo kuanzisha jimbo jipya la Ushetu.

Nyigoti alinukuliwa akitangaza jimbo jipya kutokana na alichodai ni “maelekezo ya Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba.”

Kutokana na tangazo hilo, Lembeli na wenzake wawili, Raphael Mlolwa na Elichard Mulyasi waliamua kugombea ubunge jimbo la Ushetu ambako ndiko wanakotoka.

Lakini Jumapili iliyopita, Mkurugenzi wa NEC, Rajab Kiravu, alitangaza kuwa hakuna jimbo lililotengwa na kwamba bado wanatambua jimbo la Kahama.

Taarifa kutoka wilayani Kahama zinasema kutokana na kauli ya NEC, kampeni za kutafuta mgombea jimboni humo zimechukua mkondo mpya.

Imeamuliwa wagombea waliofanya kampeni “jimbo la Ushetu” sasa wafanye kampeni Kahama; na wale waliokuwa Kahama waende Ushetu.

Lembeli ameiambia MwanaHALISI kwa njia ya simu kutoka mjini Kahama kwamba kilichotendeka ni njama za kumdhoofisha na kutaka asigombee; au ashindwe kwenye kura za maoni.

Lakini Makamba alipoulizwa kwa nini alielekeza katibu wake kutangaza kuundwa kwa jimbo jipya la Ushetu aling’aka.

“Kwani wewe umesikia nimetangaza majimbo mapya? Kwa akili yako mwandishi mpelelezi kama wewe wa MwanaHALISI unakubali nikitangaza mimi jimbo jipya la uchaguzi?”

Hakuishia hapo, alisema, “…ninavyokufahamu wewe si Idrissa? Nikitangaza majimbo mapya si kesho utaandika ‘Makamba atoa mpya. Afanya kazi isiyokuwa yake.’ Mimi sitangazi majimbo mapya. Mnajua nani mwenye jukumu hili.”

Alipong’ang’anizwa kwamba Nyigoti ametoa taarifa kuwa ni yeye alimwambia atangaze jimbo jipya la Ushetu, Makamba alisema kwa ukali, “Nasema waaache kulalamika. Wachukue hatua maana wanao uwezo wa kujua nini cha kufanya.”

Alipoulizwa kama hiyo haikuwa njama ya kumuengua Lembeli asigombee ubunge kutetea kiti chake Kahama, Makamba alisema hakuna cha kuzuiwa mtu.

“Sisi ndio tunaandaa kila kitu. Siku zipo, kuna kesho na keshokutwa; si watachukua fomu warudi kugombea Kahama? Tatizo liko wapi,” aliuliza.

Makamba alisema uongozi wa Kahama una uwezo wa kushughulikia suala hilo ili kila mwanachama anayetaka kugombea apewe nafasi.

Lembeli akizungumza kutoka mjini Kahama juzi Jumatatu usiku, alisema “mafisadi ndio wabaya wangu. Wanajua ninapambana nao kwa kuibana serikali ndani ya bunge.”

Alisema hivi sasa mafisadi wameazimia kutumia kila njia kumwangamiza kisiasa.

Taarifa za baadaye zimeeleza kuwa Makamba alimpigia simu Nyigoti tarehe 21 Julai, na kumpa “taarifa ya Tume kukubali jimbo jipya la Ushetu” na akamtaka atangazie wanachama ili wanaopenda wachukue fomu za kuomba uteuzi wa kugombea jimbo hilo.

Serikali imetangaza Ushetu kuwa wilaya mpya lakini Tume haijaitangaza wilaya hiyo kuwa jimbo jipya la uchaguzi.

Lembeli amesema yaliyotokea si mambo ya bahati mbaya, bali njama za makusudi za kutaka kumnyima nafasi ya kutetea kiti cha ubunge Kahama.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: