Mch. Mwasapile awapa changamoto madaktari


editor's picture

Na editor - Imechapwa 16 March 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

KATIKA kipindi cha wiki mbili zilizopita habari kubwa kwenye vyombo vya habari zinahusu maelfu ya wagonjwa kumiminika katika kitongoji cha Samunge wilayani Ngorongoro mkoa wa Arusha ili kupata tiba asili.

Baadhi ya wagonjwa wanatoka majumbani, wengine wanatoroko hospitali na kwenda katika kitongoji hicho ambako mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Ambilikile Mwasapile anatoa tiba hiyo.

Kwanza walianza wagonjwa wenye kipato cha chini na baadaye wakafuata wenye kipato cha juu, wanasiasa na viongozi serikalini wanaosumbuliwa na magonjwa sugu kama kisukari, kansa, presha na ukimwi.

Wagonjwa wanakimbilia kwa Babu kwa vile wanaamini anatoa dawa inayoponya magonjwa yanayowasumbua.

Hakuna uthibitisho wa kisayansi juu ya uhalisia wake, lakini jambo moja lililo wazi, watu wanatoa ushuhuda kwamba wanajisikia wamepona baada ya kunywa dawa hiyo inayoambatana na imani.

Taarifa zinasema baadhi ya watu wanaofuata tiba asili ni wagonjwa wanaoendelea na dawa walizoandikiwa na madaktari katika hospitali zinazotambuliwa na serikali.

Kinachowafanya wagonjwa wengi waende kwa Babu, kwanza ni imani yao kwa tiba asili, na pili ni ukweli kuwa dawa za kisayansi zinashindwa kutibu maradhi yanayowasumbua.

Maelfu ya watu wanaumwa. Wanapofika hospitalini, wanaandikiwa dawa. Wanatumia kama walivyoelekezwa na madaktari, lakini wanaendelea kulalamika, hali zao zinazidi kuwa mbaya. Wanaamua kusaka tiba mbadala.

Maana yake ni kwamba mfumo wa tiba ya kisayansi unawaangusha wagonjwa kwa kutoponya maradhi yao; sasa wanakata tamaa.

Wanakatishwa tamaa kwanza na utafiti duni katika nyanja ya utabibu, na pili ni mfumo unaoendekeza uzembe, rushwa na ufisadi.

Nani hakumbuki wagonjwa wawili waliopasuliwa tofauti na magonjwa yaliyokuwa yakiwatesa katika hospitali ya taifa ya Muhimbili? Nani amesahau wauguzi walivyokataa kumhudumia mjamzito, hadi anakufa, wakitaka alipe kwanza fedha kule Ukonga? Nani hakumbuki kiburi cha wauguzi na madaktari hospitali za Mwananyamala na Amana?

Katika baadhi ya zahanati na hospitali, madaktari huwa wamelewa; humwandikia dawa mgonjwa bila kumpima; vipimo vyenyewe gharama ni kubwa.

Haya yote yanachangia wagonjwa kutoroka hospitalini na kusafiri hadi Loliondo ambako gharama ni Sh. 500 tu na hakuna longolongo.

Serikali itumie changamoto hii kutoka kwa mchungaji Mwasapile kupitia upya mfumo uliooza wa utoaji tiba hospitalini ili kurejesha imani kwa wagonjwa nchini.

0
No votes yet