Mchafu hawezi kumsafisha mchafu


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 07 September 2011

Printer-friendly version
KATIBU Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo

KATIBU Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, hivi karibuni alitajwa kwa jina bungeni kuwa ametengeneza mtandao wa viongozi wa kabila la Wabena katika Wizara ya Maliasili na Utalii. Mtandao huko uko Idara ya Wanyamapori.

Badala ya kuhangaikia kujisafisha kutokana na kashfa hiyo, Luhanjo ameonekana akihangaika kumsafisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo. Luhanjo akiamini kwamba yeye haguswi, alimrejesha kazini Jairo aliyekuwa amesimamishwa kwa wiki mbili.

Jambo la kujiuliza, mtuhumiwa anapata wapi udhu wa kumsafisha mtuhumiwa mwenzake? Sasa Luhanjo kazua balaa! Bunge linadai amelidhalilisha na kwamba amemdhalilisha Waziri Mkuu, Mizengo Peter Kayanza Pinda.

Bunge, moja ya mihimili mitatu ya dola, ndiyo sauti ya wananchi katika umoja wao kwa serikali yao na kwa rais wao. Rais na serikali yake hawatarajiwi kuipuuza sauti hii. Tuhuma peke yake za chombo kikubwa na muhimu kama huu dhidi ya mtumishi wa serikali ni ulazimisho tosha kwa rais aliye mwadilifu, msikivu na mtendaji mwema kumweka kando mtumishi huyo mara moja.

Tuhuma za Bunge dhidi ya Luhanjo, zinamwondolea sifa ya kuwa mtumishi wa wananchi. Amepoteza sifa ya kuwa mtumishi katika ofisi ya juu kabisa ya wananchi, Ikulu.

Wakati anamsafisha Jairo, Luhanjo alisema, “Hata huyu aliyefanya hivi (aliyetoa siri hiyo) tukimpata naye atapata haki yake…. Ni kosa kubwa kuvujisha siri za serikali...” Halafu akasema kuwa alichofanya Jairo ni utaratibu wa kawaida. Ndivyo wanavyofanya wote! Kama hivyo ndivyo nani anasema nchi hii inashida ya fedha?

Tuhuma ni kwamba Jairo alichangisha fedha kutoka katika taasisi zilizo chini ya wizara yake kwa lengo la kuhonga ili kupitisha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini. Luhanjo anakiri kuwa hii (huku kuchangisha) ilikuwa siri na wakimpata aliyeifichua “atapata haki yake…”

Hapa Luhanjo hakujua kuwa anapokiri kuwa hii ilikuwa siri hakika anakiri uwepo wa siri yenyewe. Kwamba siri hiyo ilikuwapo na tuhuma za Bunge dhidi ya Jairo ni uwepo wa hiyo siri.

Uchunguzi ulipaswa kulenga uwepo wa siri hiyo siyo mahesabu peke yake. Ni muhimu kujua kuna taasisi ngapi katika wizara zilizoombwa kuchangia na zilichangia kiasi gani, lakini pia tuhuma au sura au picha na hisia ya rushwa vilivyojitokeza katika siri hiyo.

Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utouh anahusika vipi na jukumu la kuchunguza na kupambana na rushwa? Hiyo ni kazi inayomweka mjini Edward Hosea katika wadhifa wake wa kuongoza Taasisi ya Kuchunguza na Kupambana na Rushwa, (TAKUKURU).

Kwa kuwa TAKUKURU haikumchunguza katibu huyo kwa kudhamiria, kupanga na kuchangisha fedha kwa lengo la kutaka kutoa au kutoa rushwa, Jairo hajachunguzwa.

Wakati Pinda anampigia simu rais kuhusu suala la Jairo, Luhanjo naye alikuwa anampigia simu rais huyo huyo kuhusu Jairo. Rais akaamua kupokea na kusikiliza simu ya Luhanjo.

Hicho ndicho kilimvimbisha kichwa Luhanjo akafikia hatua ya kutoa uamuzi wa kulidhalilisha Bunge na kumdhalilisha Waziri mkuu. Akajisikia kutenda kama aliye juu ya Bunge na juu ya Waziri mkuu. Ulevi, nooma!

Kama Luhanjo alibumburuka akamrudisha Jairo kazini bila idhini, rais alipaswa kumshikisha adabu! Sasa kwa kuwa hajamwadhibu, uamuzi ule unabaki kuwa ni wa rais. Na uamuzi wa kumrudisha likizo tena, nao unabaki kuwa wa rais yule yule. Wahenga walisema, “Mwosha, huoshwa!” Aliyemtuma kwenda Chato kumfedhehesha Waziri wa Ujenzi, John Magufuli mbele ya wapiga kura wake ndiye huyohuyo aliyemfedhehesha mbele ya taifa zima! Amefikishwa kwenye fundo, itabidi arudi kwa wakulima waliomlea!

Aking’ang’ania uwaziri mkuu uliochafuliwa atajiondolea heshima yote aliyojijengea mbele ya wananchi. Pinda hatakuwa wa kwanza kujiuzulu uwaziri mkuu baada ya kufedheheshwa sana.

Kwa ujasiri wa hali ya juu, Naibu Spika, Job Ndugai akamfukuzilia mbali Luhanjo na dharau zake akisema, “Siyo rahisi Waziri Mkuu kudharaulika halafu Bunge likanyamaza kimya, haiwezekani. Kama ni dharau inaweza kutokea huko huko wanakofanya dharau hizi na siyo ndani ya Bunge hili.”

Bado naamini ndani ya CCM wapo watu makini ambao wakiamua kusimamia wananchi hata kwa kutofautiana na walanguzi, wanaweza. Ndugai anasema, “Hukohuko wanakofanyiana dharau hizi.” Kiongozi huyu anajua kuwa viongozi wetu wanadharauliana.

Viongozi wanaodharauliana wazi mbele ya wananchi wanatofautiana vipi na genge la wahuni? Na hawa ndio wanataka wawatengenezee Watanzania mtu wa sampuli yao wa kumrithi Rais wetu! Washindwe na walegee! 
Luhanjo alitumwa kupima mafuta yaliyoko motoni kujua kama yamechemka. Badala ya kutumia kiwiko cha mkono kama wenye busara wanavyofanya, kapima kwa kichwa. Haya ndiyo madhara yake.

Luhanjo aliposema huo ulikuwa uchunguzi wa awali alikuwa na maana utafanyika uchunguzi mwingine au  alikuwa anawahadaa Watanzania?

Ikumbukwe kuwa awamu ya nne ilipoingia mwaka 2005 ilikuwa kikundi mtandao kilichoipoka nchi mamlaka kikaunda serikali. Kwa dhambi hii Pinda hahesabiwi humo!

Mtandao umepasuka lakini jiwe likipasuka vipande vyake hubaki sehemu ya jiwe. Mtikisiko uliotokea baada ya mwamba wa mtandao kutolewa kafara (kupasuka) waliobaki walimwangukia Pinda ili mgongoni mwake wafanye shughuli zao.

Pinda ashike neno hili ili kuanzia sasa atende kulingana na alama za nyakati kwani siku inakuja wanamtandao watakapotuzwa na wananchi wa nchi hii kwa mema yao waliyowafanyia. Pinda hatatuzwa pamoja nao.

Ole wao kama siku hiyo haitakuwa ni ya kuwatuza, kwa maana itakuwa ni siku yao ya kihoro!  Watahukumiwa na kuadhibiwa kulingana na dhuluma waliyoifanyia nchi hii na watu wake.

Nashauri Pinda abadilike awasimamie maskini wa nchi hii wanaodhulumiwa na kuporwa mali yao na mafisadi wanaotegemea dola. Walilie kwa uchungu waponda kokoto, wamachinga, mamalishe na vijana waliokata tamaa ya maisha na kuamua kuzagaa mitaani!

Kwanini wana wa maskini wakose elimu ya juu wakati serikali ina fedha nyingi kiasi cha kufanya matunuzi ya kufuru kila mahali? Mwenyezi Mungu anajua kuwa Rais yuko kimya kwa watu wake, lakini kwa kuwa Mungu ni Mungu anajua kwa nini yuko kimya. YEYE atawajibia waja wake!

0713334239, ngowe2006@yahoo.com
0
Your rating: None Average: 3.8 (5 votes)
Soma zaidi kuhusu: