Mchango wa kila mmoja unahitajika


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 29 September 2010

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

SIFA moja kubwa ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na mgombea wake urais, Dk. Willibrod Slaa, ni uwezo wake wa kuaminika kuwa kinaweza kuthubutu kufanya maamuzi magumu, jambo ambalo vyama vingi, kikiwamo Chama Cha Mapinduzi (CCM) limewashinda.

Matukio kama yale ya Mwembeyanga na jinsi walivyokomalia sakata la mkataba tata wa Richmond, Buzwagi, Meremeta na wizi ndani ya Benki Kuu ya taifa (BoT), chama hiki kimejiweka katika kiwango kingine kabisa kisiasa.

Vipo vyama vilivyojaribu kudandia, lakini hakuna kilichoweza. Kwa miaka mitano mfululizo, CHADEMA kiliongoza mapambano ya kutaka watuhumiwa mbalimbali wa ufisadi wajibike au wawajibishwe.

Hawakuitisha maandamano. Bali, walizungumza ndani ya Bunge na mbele ya wananchi. Mwamko wao wa ukabaki kuwa wakisomi zaidi kuliko wa kisiasa.

Hata uamuzi wa kumfanya Dk. Slaa kuwa mgombea wao wa urais, ulifanyika kwa misingi hiyo ya kuthubutu. Nani alitarajia kwamba mtu ambaye tayari alikuwa na uhakika wa kurejea bungeni, kubeba bendera ya urais?

Ulikiwa ni ujasiri mwingine na umakini wa vitendo. Matokeo yake hofu kuu imewaingia watawala wetu walioshindwa; hofu ambayo inatokana na kujua kile kinachowezekana kutokea.

Wana CCM na mashabiki wake wana hofu ya uwezekano wa mgombea wao, Jakaya Kikwete kushindwa katika uchaguzi huu. Mazingira yapo tayari, sababu ipo, na nia ipo. Tatizo ambalo lipo hadi hivi sasa, ni uwezo na mbinu.

CHADEMA wamepewa nafasi ya kihistoria ya kuongoza mabadiliko nchini, nafasi ambayo kama ingekuwa kwenye nchi nyingine yoyote, basi wala kusingekuwa na wasiwasi wa uchaguzi utaelekea vipi.

Hata hivyo, nilazima niseme wazi kuwa yeyote anayefikiria kuwa CHADEMA watapewa ushindi wa kuing’oa CCM kwa sababu wanastahili, anajidanganya.

Ni lazima wafanyie kazi kila kura. Wafahamu kuwa kura haziji kwa kuangalia umati wa watu wanaohudhuria mikutano ya kampeni au kusikia watu wakijibu kwa sauti moja ile “Nguvu ya umma!”

Wala ushindi hautakuja kwa kuangalia wasomi wangapi wanaunga mkono CHADEMA, ni watu wangapi wanaimba sifa zake au kuangalia vichwa vya habari vya magazeti! Ushindi utakuja kwa kupata kila kura moja kutoka kwa anayekubali mabadiliko.

Jukumu hili la kujikusanyia kura nyingi za ushindi haliwezi kuletwa na Dk. Slaa pekee, ama viongozi wenzake ndani ya CHADEMA.

Anayefikiria ati CHADEMA itapata ushindi kwa sababu Dk. Slaa anazungumza kwa hamasa na anaongoza mapambano dhidi ya ufisadi, atakuwa anaota ndoto.

Ushindi utaletwa na Watanzania ambao wanaona nchi yao haiendi wanavyotaka na hivyo wanajipa jukumu la kuiurudisha mikononi mwao.

Ushindi utaletwa na mamilioni ya mabinti, vijana na wazee wa taifa hili ambao mmoja mmoja watasema “CCM asante, lakini kwaheri!”

Wale ambao watasema wamechoka kuahidiwa pepo ya njozini wakati wachache katika jamii yetu wakiendelea kufurahia yale tuliyoyaita enzi zetu kuwa ni “matunda ya uhuru.”

Wala ushindi ambao watu wanaufikiria au kuuombea utokee hautakuja kwa kunuiwa au bila gharama. Hautaletwa na malaika kutoka mbinguni! Wale wanaotaka kuona CHADEMA inashinda au kufanya vizuri zaidi kuliko miaka mingine ni lazima wawe wa kwanza kushiriki katika kutafuta ushindi.

Kila timu ina wachezaji na makocha wake.

Kila mmoja ana nafasi yake! Siyo wote wanaweza kupewa nafasi ya ukocha na si wachezaji wote watapangwa kucheza.

Lakini wote ambao hawako katika kushiriki mechi wana nafasi ya kuitakia ushindi timu yao. Nakumbuka miaka ya shule ya msingi timu zetu hazikuwa na wafadhili wowote isipokuwa wazee na vijana wa mitaani ambao timu ilipokuwa ikicheza walitununulia machungwa ambayo tulikula wakati wa mapumziko.

Tuliposhinda nao walifurahia kwa sababu walijua kuwa ni sehemu ya ushindi huo. Siyo katika kutushangilia tukicheza, lakini katika kuhakikisha tunashinda.

Vivyo hivyo katika harakati za mabadiliko ya kisiasa. Mashabiki wanaokaa pembeni kushangilia lakini hawako tayari kununua machungwa kidogo kwa ajili ya timu au kufuatana na timu katika mechi za mbali, hao ni mashabiki uchwara.

Mashabiki watakaoleta mabadiliko kwa taifa ni wale ambao wataamua kushiriki kuileta ushindi. Si kwa sababu wanaichukia CCM, kwani chuki haitoshi kuleta mabadiliko, bali kwa kuwa wanatofautiana na CCM.

Tofauti hii ni ya msingi sana kiasi kwamba haiwezekani kupatana. Yaani, ni tofauti ambayo inagusa dhamira, mawazo, mipango na maono ya mtu.

Lakini yote haya yamo mikononi mwa wananchi na CHADEMA yenyewe. Naogopa kutoa tathmini ya kampeni hadi hivi sasa, lakini ninachoweza kusema kwa uhakika ni kuwa ili CHADEMA ishinde, ni lazima ifanye mara 100 zaidi ya ilichokifanya!

Kama kuna watu wanadanganyika kwa kuangalia picha za mikutano na kusema “mwaka huu wetu,” basi sitaki watu walie kuwa “CCM wameiba kura.”

CHADEMA inatakiwa kujipanga kwa kuwa na wasimamizi kila kituo. Kinahitaji kuwa na watu wengi na ambao inawalipa kwa kufanya shughuli za uchaguzi.

Eneo lolote kati ya hayo ambapo CHADEMA itapwaya, utakuwa mlango wa kushindwa! Kama hadi hivi sasa haijui ina wasimamizi wangapi na wanawasiliana vipi na makao makuu ya mikoa na wilaya, basi hilo litakuwa ni tatizo!

Katika kampeni hizi, CCM inazo fedha nyingi, ukilinganisha na CHADEMA. Ilikozipata yenyewe inajua. Lakini ushindi hauji kwa nguvu ya fedha pekee, bali unakuja kwa nguvu ya watu wanaojitolea.

Lakini nafasi ya fedha haiwezi kupuuziwa. Binafsi, sijui ni kwa namna gani wananchi wanahusishwa kuchangia sehemu ya ushindi wa kununua machungwa!

Hakuna njia nzuri na ya kuishtua CCM kama kuchangia chama kinachokitisha. Si lazima uchangie kwa simu, unaweza kuchangia kwenye akaunti yao.

Kwa kuchangia CHADEMA tuma neno “CHADEMA” kwenda Na. 15710 na utakuwa umechangia Sh. 350 kwa kila sms. Hii ina maana gani?

Ina maana kwamba leo Jumatano wasomaji wapatao elfu kumi tu wakiamua kutuma sms moja kwa siku watakuwa wamechangia Sh. 3.5! milioni. Wakiamua kuchangia kiasi hicho hicho kwa siku saba mfululizo, watakuwa wamechangia Sh. 24 milioni! Je, iwapo wataamua kuchangia zaidi ya mara itakuwaje?

Wengine wanaweza kuchangia kununua “machungwa” kwa kutumia M-Pesa kwa kutumia Na. 0758 22 33 44, 0764 77 66 73 au kwa kutumia Benki akaunti ya CHADEMA M4C - CRDB 0J1080100600 au MNB ni akaunti 2266600140.

Pendekezo langu kwa wale wanaotaka kuchangia ni kutuma neno hilo kwenda hiyo namba, halafu wawatumie marafiki na jamaa zao kwenye simu jumbe kuwa “nimechangia mabadiliko kwa kutuma sms kwenda Na. 15710 kuchangia CHADEMA; nawe changia.”

Hili likifanyika, katika siku chache zijazo wanaotaka mabadiliko wataona tofauti mitaani; wataona mabango zaidi ya Dk. Slaa, wabunge na madiwani.

Lakini wale ambao wanaona kuwa CHADEMA haifai kuongoza na CCM ndiyo inatakiwa iendelee kutawala, wana haki ya kukichangia chama hicho ili kiendelee kutawala.

Ni lazima wachangie kwa kufuata dhamira zao. Wala wasione aibu katika hili. Si lazima wote wachangie upinzani kwa kufuata mkumbo!

Anayechangia CCM achangie kwa sababu anaamini kwa dhamira yake kuwa kwa kufanya hivyo ni vizuri kwake na kwa watoto wake.

Tunataka CHADEMA watangaze kiasi kitakachokusanywa ndani ya siku hizi saba kama kampeni maalum. Lengo ni kutaka kuona kama kweli Watanzania wanataka mabadiliko na wako tayari kuyagharimia.

Itakapofika Jumatano ijayo tunataka kuona kama wana mabadiliko wataweza kuchangia Sh. 100 milioni! Ukilinganisha na kinachotumiwa na wanaotaka kurejea madarakani, kiasi hicho ni kidogo sana.

Wao wamepanga kutumia Sh. 50 bilioni katika uchaguzi huu. Hii ni sawa na karibu kutumia Sh. 700 milioni kwa siku!

Kama nilivyosema ushindi kwa Dk. Slaa utaletwa na wenye haja ya kubadilisha utawala uliopo.

Vyovyote vile ilivyo, kama kweli wananchi wanataka mabadiliko, siyo kusindikiza, ni lazima wachngie chama hiki kinachokaribia kufika ikulu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: