MCHECHU: Nikishindwa kuleta tija NHC nihukumuni


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 01 December 2010

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) linataka kuleta mapinduzi katika sekta ya makazi nchini. Wakuu wake wanajua vizuri namna jambo hilo lilivyo gumu kufanikiwa.

Kuleta mapinduzi ya chochote kile kuna maana kubwa. Kwanza, waletaji mapinduzi hayo kusimama kidete kukataa shinikizo za kisiasa, zikiwemo zile zenye mwelekeo wa ufisadi.

Pili, kutumia raslimali kwa uadilifu mkubwa. Hulka ya wanasiasa wa Tanzania ni kufisidi na kutoweka bila ya kubanwa kisheria. Tatu, kupata washirika makini wa kusaidia kufanikisha mapinduzi hayo.

Lakini, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemiah Mchechu anasema hakuna kisichowezekana. Tangu alipoteuliwa kuongoza shirika hilo miezi saba iliyopita, anasema amekuwa akifanya kazi kwa uhuru mkubwa.

Mchechu alipoanza NHC hakupata shinikizo zozote kutoka kwa wanasiasa. Labda wakati ule walikuwa katika harakati za kutafuta madaraka akiwemo aliyekuwa waziri anayehusika na nyumba na maendeleo ya makazi, John Chiligati.

Pamoja na kurudi kuwa mbunge wa Manyoni Mashariki, Chiligati hakuteuliwa katika baraza la mawaziri jipya.

NHC inaweza kutimiza dhamira ya kuleta mapinduzi ya sekta ya makazi kwa kupatiwa timu kabambe ya wakurugenzi katika idara zake mbalimbali.

Mchechu atakuwa ana bahati ya mtende. Safari hii atafanya kazi chini ya mtaalamu makini kwa viwango vyote, Profesa Anna Tibaijuka, aliyetoka kuwa mkurugenzi mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia maendeleo ya makazi (UN-HABITAT).

Inatarajiwa Mchechu amepata mkuu muadilifu atakayemsaidia kulifikisha shirika hilo kwenye kiwango cha juu cha ufanisi huku wakizingatia anachokiita “fikra mpya.”

“Nimejipanga vizuri kwa kutafuta timu kabambe. Katika kila idara nimeleta nguvu kubwa ya kufanya kazi kitaalamu. Tunataka kuonyesha ukweli kwamba NHC ni dhahabu iliyojificha.

“Tutatumia raslimali zetu kwa ukamilifu wake ili kuongeza tija ya shirika na uchumi wa taifa letu. Ninaamini tutafanikiwa. Na kipindi changu kikimalizika mje kuniuliza na mkiona sikufanikiwa, basi tatizo litakuwa ni langu binafsi,” Mchechu anawaambia wahariri waliokutanika hivi karibuni kutambulishwa kikosi cha NHC na mpango wa kubadilika kiutendaji.

Mpango ni kurekebisha nyumba na kugeuza baadhi ya majengo kuwa ya kisasa ili kupandisha kodi hasa yale yaliopo maeneo kama Upanga, Masaki na Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Kwa majengo ya Tandika, Mchechu anasema yatauzwa kwa wapangaji waliopo.

Likiwa limeanzishwa mara tu baada ya uhuru wa Tanganyika, mwaka 1961, Shirika la Taifa la Nyumba limekuwa likijishughulisha zaidi na usimamizi wa nyumba kongwe za kurithi.

Shirika limekuwa likitumaini mapato yake kutokana na kupangisha nyumba zake. Nyumba nyingi zipo kwenye miji makao makuu ya mikoa na wilaya nchini kote.

Sasa NHC wamejipangia malengo katika kuleta mapinduzi ya makazi nchini. Mojawapo ni mpango wa miaka mitano utakaohusisha ujenzi wa majengo 15,000 mapya.

Ziko wapi fursa zitakazosaidia NHC kufanikisha mapinduzi ya makazi? Mchechu anasema fursa ya kwanza muhimu kuliko zote ni utajiri wa viwanja ambavyo ni mali ya shirika. Hivi vimetapakaa nchi nzima.

Utajiri wa mali za NHC upo zaidi jijini Dar es Salaam ambako ndipo mchango wa asilimia 60 ya pato la taifa hutoka.

Hata hivyo, Mchechu anasema, inasikitisha kuona jiji linakufa mara tu ofisi za serikali zinapofungwa. Baada ya kufungwa kwa ofisi za serikali ambazo nyingi zipo katikati ya jiji, watu wote wanatoka na kurudi nje ya katikati ya jiji wanakoishi.

Kumbe kawaida hiyo ni hasara kwa taifa linalotaka maendeleo. Watu watoke lakini huduma inatakiwa ziendelee. Kuna watalii wanahitaji huduma, lazima wazipate.

Ndipo ilipo hoja ya Mchechu. Anasema mpango wao ni kujenga maeneo yao na kuweka sehemu za huduma mbalimbali hasa kwa kuzingatia kuwa mengi ya raslimali zake zipo kwenye maeneo mazuri kiuwekezaji.

Kuna upungufu mkubwa wa nyumba za kuishi wananchi. Takwimu zinaonyesha nyumba milioni tatu, sawa na uwekezaji wa dola 180 bilioni, zinahitajika.

Kwa wastani, Mchechu anasema, kupatikane nyumba 200,000 kila mwaka, gharama yake ikiwa ni dola 12 bilioni.

Anasema, “tunakusudia kugeuza shida ya nyumba kuwa ni njia ya kukuza pato la taifa. Mipango yetu inachochea fursa kubwa ya maendeleo ya kiuchumi.”

Anasema zaidi ya asilimia 99 ya nyumba nchini zimejengwa kwa fedha zitokazo mifukoni mwa watu, badala ya mitaji itokayo benki. Nyumba moja huchukua mpaka miaka kumi kukamilika wakati ingewezekana kwa kati ya miezi tisa na 12 tu.

“Ukuaji wa sekta ya ujenzi wa nyumba za kuishi katika miaka 20 ijayo unawezekana kama mabenki yatashiriki kusaidia,” anasema huku akijivuna kuwa kwa upande mwingine, mpango huo utazalisha nafasi nyingi za ajira kwa wananchi.

“Zaidi ya watu milioni moja wataajiriwa na idadi itaongezeka kwa asilimia 20 na zaidi katika miaka kumi ijayo… manufaa yatakuwa kwa wananchi wasiokuwa na ujuzi,” anasema Mchechu, aliyekuwa mkurugenzi wa Benki ya Biashara ya Afrika (CBA) iliyopo nchini.

Mchechu anafanya ushawishi kwa mabenki kuingia katika kuleta mapinduzi ya makazi nchini kwa kusema hayatapata hasara yoyote kwa kuwa “kuna mahitaji makubwa ya nyumba nchini na sekta binafsi ndiyo yenye nafasi kubwa ya kutengeneza faida.”

“Utatuaji wa tatizo la nyumba unahitaji ushiriki wa sekta binafsi. Kwa sababu za wazi, sekta hii haijashiriki itakiwavyo. Hapa ndipo sisi (NHC) tunataka kupatumia kuleta mapinduzi,” anasema.

Mchechu anasema benki zitakazochangamkia mipango yao zitathibitisha namna gani NHC imeamua kubadilisha mfumo wa utendaji kazi.

Ndoto alizonazo zinatokana na mazingira yaliyopo nchini, lakini pia, uzoefu wa nchi nyingine, zikiwemo za Mashariki ya Mbali kama Singapore, ambayo hadi miaka ya 1970 ilikuwa haina maendeleo yoyote ya maana lakini leo, “Inatisha kwa sekta ya makazi,” anasema Mchechu.

Ni majengo kama yanayoonekana Singapore yanayomtia jeuri Mchechu kwamba lazima waanze kubadilika sasa kwa kuwa wana raslimali za kutosha.

NHC ilirithi majengo 26,705 ya kupangisha. Majengo 5,689 yalimilikishwa mwaka 1991 kwa mamlaka za serikali za mitaa na 4,666 zikauzwa. Kwa sasa, shirika lina majengo 2,389 yenye nyumba 17,111, zote zikiwa na thamani ya Sh. 1.045 trilioni.

Kila mwaka shirika hupata mapato ya Sh. 30 bilioni kutokana na raslimali zake hizo. Ingawa kuna mazingira bora ya utendaji kutokana na marekebisho ya sheria ya ardhi (1999) na NHC (1990) yaliyofanywa mwaka 2005, bado Mchechu anaona kuna vikwazo kiutendaji.

Anasema kuna vipengele vingi vya sheria vinampa mamlaka makubwa mno waziri anayehusika na masuala ya ardhi na nyumba. “Tunataka kufanya kazi kwa uhuru na katika mtizamo wa biashara zaidi vinginevyo vikwazo vya kisheria vitaleta shida,” anasema.

Kutokana na msimamo huohuo, Mchechu alionyesha wahariri ramani ya kinachokusudiwa kuwa kijiji cha kisasa kitakachojengwa eneo la Kawe, mkoani Dar es Salaam iwapo taratibu muhimu zitakamilika.

Kijiji hicho kitakuwa na huduma zote za kijamii zikiwemo maeneo ya kucheza watoto, shule, nyumba za ibada na huduma za kitalii, zitakazotoa fursa kwa wazamiaji baharini.

0
No votes yet