Mchwa halmashauri Kahama unatisha


Ali Lityawi's picture

Na Ali Lityawi - Imechapwa 28 December 2011

Printer-friendly version

OKTOBA 10, 2005 umati mkubwa wa watu ulifurika katika uwanja wa halmashauri ya wilaya ya Kahama kumsikiliza Jakaya Mrisho Kikwete, akiomba ridhaa ya Watanzania wamchague kuwa rais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).

Aliwakuna zaidi kwa hotuba yenye matumaini iliyogusa kero ya wakazi wa wilaya ya Kahama hasa ahadi yake ya kuangamiza mchwa katika halmashauri yao. Akapata ushindi wa kimbunga.

Kikwete yule aliyetoa ahadi ya kuua mchwa halmashauri kwa Dudu Killer ama amesahau ahadi hiyo au hataki kutekeleza, mchwa wanaotafuna fedha za halmashauri ya Kahama wamezidi kunenepa.

Taarifa na malalamiko ya madiwani katika Baraza la Madiwani, ni kwamba ufisadi ndani ya halmashauri ya Kahama unazidi kukithiri kwa sababu baadhi ya madiwani, waliopaswa kuzuia wizi wanashirikiana na watendaji wasio waaminifu wa halmashauri kupata maslahi kupitia kampuni za wakandarasi zinazopewa zabuni. Madiwani wa CCM ndio wananyoshewa kidole cha lawama kwa kubariki ufisadi.

"Utetezi wanaoutoa watendaji wa halmashauri juu ya mafanikio yao ya kumiliki magari na nyumba kwa muda mfupi, eti ni kutokana na mikopo wanayochukua katika vyombo vya fedha. Kwa nini mafanikio hayo wayapate kwa kipindi kifupi tangu wahamishiwe au kupata ajira katika halmashauri ya Kahama?” anahoji Katibu wa chama cha TLP, wilayani Kahama, Paul Seleli.

Seleli anaungwa mkono na diwani wa Kahama Mjini (CHADEMA), Abbas Omary Jaffary ambaye anasema wamegundua mchezo mchafu unaofanywa kupitia uuzaji viwanja.

"Nimehangaika sana hadi nimefanikiwa kuzuia ujenzi wa vibanda vinane vya biashara eneo la stendi kuu ya mabasi baada ya kubaini taratibu hazikufuatwa,” alisema Jaffary.

Utata wa viwanja hivyo ni wa muda mrefu na anaujua Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja ambaye aliwahi kumwita mkuu wa wilaya katika kikao cha dharura kilichoitishwa kufuatia malalamiko ya baraza la wazee wa wilaya.

Katika kikao hicho kilichofanyika katika jengo la CCM wilaya ya Kahama, 9 Februari 2011, Mgeja aliagiza uwepo uwazi wa kutangaza nafasi hizo kwa kuwaachia wananchi wa kawaida kuomba maeneo hayo ili kuepusha viongozi na watendaji wa halmashauri hiyo kumiliki. Mkuu wa wilaya meja mstaafu Bahati Matala aliahidi kushughulikia suala hilo.

Lakini halmashauri imedharau uamuzi huo, ikaruhusu kuendelea kwa ujenzi wa vibanda hivyo chini ya kivuli cha kandarasi waliyopewa na halmashauri.

"Maamuzi yale ya Februari yalikuwa kiini macho kwani yameendeleza historia iliyopo ya serikali, kupuuza kila maagizo wanayoyapewa,” anasema Jaffary.

Katika kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani kilichofanyika 26 Julai 2011, madiwani walifichua ufisadi uliofanywa na halmashauri kupitia Idara ya Kilimo. Idara hiyo ilinunua, kwa mtindo wa zabuni pikipiki 12 aina ya DAYUN  kwa Sh. 2.525 milioni kila moja.

Lakini Jaffary alipinga akisema, "Pikipiki aina ya SANLG ambazo ni bora zaidi ya DAYUN hapa wilayani petu Kahama, inauzwa dukani kwa Sh. 1.6 milioni. Hapa inatutia shaka juu ya uadilifu wa watendaji wetu linapokuja suala la manunuzi ya rasilimali za halmashauri yetu."

"Sasa kigezo gani kilitumika hadi likawepo ongezeko la bei ya pikipiki hizo zilizonunuliwa na Idara ya Kilimo?” alihoji diwani wa Viti Maalum (CHADEMA), Asha Binde.

Hoja hizo, ndizo zilimlazimisha Kaimu mkurugenzi wa halmashauri, Hamis Mkunga katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashuri 4 Novemba 2011 kutoa taarifa ya utekelezaji.

"Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ametekeleza agizo lenu waheshimiwa kwa kuandika barua yenye kumbukumbu Namba KDC/ F.20/ 15 /Vol.XI / 132 ya tarehe 18 / 8 / 2011 kwenda kwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi ikielezea malalamiko kuhusu kupata ufafanuzi juu ya bei za ununuzi wa pikipiki hizo," anasema.

Halmashauri ilipata wakati mgumu iliposoma taarifa ya maendeleo ya Julai hadi Septemba mwaka huu ambapo madiwani 15 wa vyama vya upinzani, walipinga taarifa hiyo. Mwenyekiti wa halmashauri hiyo alilazimika kuunda kamati ya watu watano kufuatilia suala hilo la ununuzi wa pikipiki.

Pia madiwani hao wamefunga mwaka kwa kukataa taarifa ya mapato na matumizi ya fedha za halmasahuri.

"Tatizo pesa zinaishia katika matumizi  ya uendeshaji wa ofisi katu si maendeleo. Angalia kati ya pesa za makusanyo ya ndani kwa mwezi Septemba mwaka huu, zilipatikana Sh. 217 milioni, lakini tunaambiwa Sh. 15 milioni ndizo zilizorudi kwa wananchi kwa ajili ya miradi ya maendeleo, zilizobaki zote zilitumika kwa matumizi ya ofisi," anasema diwani wa Bulyanhulu (CHADEMA), Joseph Makoba.

"Inashangaza katika matumizi hayo mabaya ya fedha tunajumuishwa nasi waheshimiwa ili kuyahalalisha. Tazama taarifa iliyosomwa inaeleza halmashauri yetu ilitumia Sh. 24 milioni kwa sherehe za Nane Nane zilizowajumuisha madiwani. Swali, je, zilitumika wapi na madiwani gani? Mbona sisi hatukushiriki?"anahoji Sospeter Bunende, diwani wa Kata ya Idahina (CHADEMA).

Mbunge na Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige aliyehudhuria Baraza hilo alionya juu ya matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa na serikali kuu kwa halmashauri za hapa nchini.

"Madiwani wameshtuka kutokana na taarifa kuandikwa na wataalamu pasipo mchanganuo wenye kukidhi. Ni kweli tumerudi nyuma katika utekelezaji wa matumizi ya rasilimali za nchi.

“Napenda kuwaasa watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kahama, sisi hatuna nafasi ya kuwafundisha utaalamu wenu mliosomea, tunatambua mnafahamu wajibu wenu fika, hatutakuwa na haja ya kuwafuatafuata mkifuata maadili ya majukumu yenu kwa kuwajibika kwa uadilifu na ukamilifu," alisema.

Jambo jingine lililowaudhi madiwani ni kuidhinishwa kwa Sh. 1,816,500 kwa ajili ya kuandika vibao 22 vya maegesho ya pikipiki zinazotumika kubeba abiria huku gharama halisi ikiwa chini ya Sh. 30,000.

Viongozi wa CCM na serikali wanahangaika na falsafa ya kujivua gamba wakilenga watuhumiwa wa ufisadi kuwa wamesababisha ushindi wa rais kushuka hadi asilimia 61, ukweli mchwa huu ulioko katika ngazi ya halmashauri ndio gamba linalopaswa kuondolewa haraka.

078493315/ 0715933815 / 0767933815
0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)