Mechi za marudiano za ushindi Simba, Yanga


Elius Kambili's picture

Na Elius Kambili - Imechapwa 22 February 2012

Printer-friendly version

SIMBA imewahi kufanya maajabu mara mbili. Mwaka 1979 ilichapwa mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Taifa na Mufulira Wandarers ya Zambia katika mechi ya Klabu Bingwa Afrika (leo Ligi ya Mabingwa Afrika).

Mashabiki wakafuta uwezekano wa miamba hiyo ya Mtaa wa Msimbazi, jijini Dar es Salaam kusonga mbele. Lakini Simba ilishangaza watu ilipoinyamazisha Mufulira mbele ya mashabiki wake kwa mabao 5-0.

Mara ya pili kwa Simba ni mwaka 2003 ilipokwaana na mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Zamalek ya Misri. Simba ilishinda kwa bao 1-0 Dar es Salaam na ikachapwa bao 1-0 Cairo. Ilipofika zamu ya matuta Simba ilishinda 3-2 na ikafuzu.

Hicho ndicho klabu ya Yanga inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika inaweza kujifunza kuwa Zamalek inafungika iwe ugenini au nyumbani kwao, Misri.

Baada ya kuikosa Dar es Salaam kufuatia sare ya bao 1-1 na Zamalek katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kwa mchezo ilioonyesha Yanga mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, inaweza kuitupa Zamalek katika mchezo wa marudiano ‘kwao’.

Kabla ya mechi, Yanga haikupewa nafasi ya kuifunga Zamalek. Mashabiki walijua klabu yao inakamilisha ratiba tu kwamba ingefungwa, tena kwa idadi kubwa ya mabao.

Tofauti na mashabiki wa Yanga, wenzao wa Simba, wakijivunia historia ya mafanikio katika michuano ya Kombe la Shirikisho (mwaka 1993 ilicheza fainali), walijawa matumaini ya kuifunga Kiyovu FC ya Rwanda jijini Kigali. Lakini Simba ikalazimishwa sare ya bao 1-1.

Siku zote, timu bora huweza kushinda mechi iwe nyumbani au ugenini. Klabu za Simba na Yanga zimeonyesha uwezo mkubwa katika mechi zao za mwanzo na zinaweza kushinda mechi za marudiano.

Ni maandalizi mazuri tu yatakayozifanya klabu mbili hizo zibaki katika michuano hiyo ya Afrika.

Historia ya mafanikio ya Zamalek iliwapa hofu Yanga, na historia hiyohiyo iliipa Simba nafasi kubwa ya kuibamiza Kiyovu. Wachambuzi wa michezo wakapotea na kilichotokea uwanjani ndicho kinachothibitisha soka ni dakika 90.

Si mashabiki na wachambuzi tu, hata wachezaji hawakujiamini, lakini muda mfupi baada ya kuanza mchezo, wachezaji Yanga wakajiona kwamba wanaimudu Zamalek; walikosa nafasi kadhaa za kufunga mabao na katika dakika ya 36 Hamis Kiiza aliwanyanyua juu mashabiki kwa bao safi.

Washambuliaji Davies Mwape na Kenneth Asamoah hawakuweza kuzitumia vyema nafasi za wazi walizopata katika eneo la hatari la Zamalek. Walichokifanya wachezaji hao si kitu kipya kama umewahi kuwaona katika mechi za Ligi Kuu ya Bara.

Siku zote Mwape na Asamoah hucheza katika kiwango walichoonyesha dhidi ya Zamalek, hakuna kitu kipya. Kuna baadhi ya mechi za ligi, washambuliaji hao hupoteza nafasi saba na kufunga bao moja. Si jambo la ajabu kwao.

Yanga ikirekebisha makosa ya Mwape na Asamoah, ikajipanga na kutumia vizuri nafasi inazopata, inaweza kuiondosha Zamalek kwao.

Kikosi cha Zamalek, hasa kile kilichomaliza mchezo ni kikali, hivyo safu ya ulinzi ya Yanga inapaswa kunolewa ipasavyo iweze kuzuia mikwaju ya washambuliaji wanaoongozwa na Amr Zaki.

Japokuwa ratiba ya michezo ya timu ya taifa inaweza kutibua kidogo mipango ya Yanga, kocha Papic bado ana nafasi ya kuchambua kikosi chake kikaweza kufanya vizuri. Wachezaji Shaaban Kado, Shadrack Nsajigwa na Stephano Mwasika ndio pekee walioitwa Taifa Stars kutoka Yanga.

Kwa upande wake Simba, haina cha kupoteza katika mechi ya marudiano kwani inacheza uwanja wa nyumbani, mbele ya mashabiki wake itakapokuwa ikitafuta tiketi ya kusonga mbele kwenye Kombe la Shirikisho baada ya kutoka sare ya 1-1.

Wataalam wa saikolojia inabidi wafanye kazi maalum kwa wachezaji ili waitambue kazi iliyo mbele yao. Kamwe hawapaswi kuibeza Kiyovu ya Rwanda ambayo haina uzoefu wowote wa michuano ya kimataifa.

Nafasi ya Simba kusonga inaonekana rahisi mdomoni kutokana na historia ya Kiyovu lakini ni ngumu kutekelezeka uwanjani endapo wachezaji hawatajituma ipasavyo ndani ya dakika 90 za mchezo.

Benchi la ufundi limeshaisoma Kiyovu kwa kila kitu na ni wazi litatumia vyema faida ya kucheza nyumbani kuiondosha klabu hiyo. Mipango mizuri itaifanya Simba isonge mbele.

Kwa zilipofikia Simba na Yanga, kazi kubwa ipo kwa wachezaji, viongozi na hata wadau wanaozisaidia timu hizo wakati mwingine. Kama kila mtu atafanya kazi yake ipasavyo, timu hizo zitafika mbali.

Kila mchezaji anapaswa kucheza kwa kujituma muda wote, uongozi lazima uhakikishe wachezaji wanapata huduma ipasavyo na wadau tuna wajibu wa kuzisaidia klabu hizi ili zisonge mbele.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: