Membe amwokoa Kikwete


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 16 September 2008

Printer-friendly version
NEC ilikaribia kupasuka
Ni katika sakata la Nape
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe ndiye alimwezesha Rais Jakaya Kikwete kubaini njama za kupasua Chama Cha Mapinduzi (CCM) , MwanaHALISI limeelezwa.

Hii ilikuwa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM mjini Dodoma Jumatano iliyopita, ambacho kilikuwa na zaidi ya ajenda kumi.

Suala ambalo waliokamia kumdhoofisha Kikwete walitaka kutumia ni lile la kumfukuza Nape Nnauye kutoka Umoja wa Vijana (UV-CCM).

Taarifa zinasema Membe alimweleza Kikwete kwamba lazima yeye, kama mwenyekiti wa chama, asimame kidete na kuchukua hatua kushughulikia suala hilo.

Awali, kwenye Kamati Kuu (CC), Kikwete alikuwa ameliona suala la Nape kutimuliwa kwenye chama kuwa jambo dogo na alinukuliwa akisema, “Hili ni suala la mtaani. Tusubiri liletwe. Likija tutalijadili.”

Kauli ya Kikwete iliimarisha pande mbili: Mafisadi ambao walikuwa wanaona Nape amewaingilia katika “mradi wao,” na wale ambao kimsingi wamekuwa wakishikilia kuwa mafisadi wafukuzwe kwenye chama.

Mgawanyiko wa wajumbe wa NEC ulikuwa wazi nje ya ukumbi. Lakini ulianzia kwenye CC ambako Abdulrahman Kinana alitaka kujua hatma ya Nape.

Mtoa habari alilieleza MwanHALISI kuwa kama Kinana asingeingiza suala hilo, basi wajumbe wawili wa sekretarieti walikuwa tayari kuvunja kanuni na kuwasilisha hoja hiyo mbele ya Kikwete.

Nje ya ukumbi wa NEC, hata hivyo, wajumbe walijiapiza kujadili suala la Nape. Wakati mafisadi walisema halijadiliwi, wapinzani wakuu wa ufisadi ndani ya chama walisema, “Kama ni mpasuko wa chama basi utokee leo.”

Ilikuwa baada ya Membe kushuhudia maapizo ya wajumbe, alikwenda moja kwa moja kwa Kikwete na kumweleza kuwa achukue hatua madhubuti kuhusu suala la Nape, vinginevyo “hadhi yake kama mwenyekiti na rais itadhoofika vibaya,” ameeleza mtoa habari.

Kwa mujibu wa taarifa za walio karibu na Kikwete, Membe alimweleza Kikwete juu ya kuchafuka kwa hali ya hewa, kinyume na wabaya wa Nape walivyokuwa wakimwonyesha.

“Hawa wanakudanganya,” Membe ananukuliwa kumwambia Kikwete. “Huko nje kuna presha kubwa. Ni vema ukalishughulikia suala hili kabla mambo hayajaharibikia mikononi mwako,” alisema mtoa taarifa wetu akimnukuu Membe.

Si hivyo tu, Membe amenukuliwa akimweleza Kikwete kwamba kama hakuchukua hatua kukabiliana na hali hiyo, tena kwa makini, “utazalisha Zuma.”

Zuma (Jacob), ni rais wa chama cha African National Congress (ANC) cha Afrika Kusini ambaye ameendesha vita vikali ndani ya chama chake na kuibuka mshindi.

MwanaHALISI imeelezwa kuwa Membe alimwambia Kikwete, “Huwezi kuondoka hapa bila kushughulikia suala la Nape, kisha tukabaki salama. Kuna presha ya ajabu. Hawa wanakudanganya,” mtoa taarifa anamnukuu Membe akimweleza Kikwete.

Taarifa zinaeleza Kikwete alimsikiliza Membe kwa makini na kwa kuonyesha kuelewa ukubwa wa tatizo alijibu, “Nakushukuru.”

Ni ushauri huu wa Membe uliompa Kikwete mawazo mapya na ujasiri wa kusema kuwa NEC inamtambua Nape katika nafasi zake zote kichama na kwamba kwa yaliyotokea UV-CCM anaweza kukata rufaa kwenye chama, kama atapenda.

Kwa mara nyingine kauli ya Kikwete ilikuwa ya athari kubwa kwa pande mbili. Mara hii, watetezi wa ufisadi wakinyong’onyea na upande mwingine ukitabasamu.

Awali katika CC, Makamba aliwasilisha mkataba kati ya UV-CCM na mwekezaji ambao umeleta utata ili uwekwe saini.

Ndipo Samwel Sitta, Abdulrahaman Kinana, Anne Abdallah, Yusuf Mohamed Yusuf (Mrefu) na John Malecela walitaka kuona mkataba wa awali na siyo ule uliofanyiwa marekebisho na Makamba na Nchimbi.

Baada ya wajumbe kulinganisha mkataba wa kwanza na wa pili, walibaini kuwa hata ule wa pili ulikuwa na kasoro kubwa. Walibainisha kasoro kuu tano.

Walizitaja kasoro hizo kuwa ni mkataba kuwa wa “milele,” jambo ambalo halikubaliki kokote duniani.

Kasoro nyingine ni shughuli zote za maamuzi, ushauri na udhibiti kuwa mikononi mwa mwekezaji na UV-CCM kuachwa bila jukumu.

Hali hii inaweza kusababisha mwekezaji kujiamulia kutamka gharama au thamani ya vifaa na majengo, hatua ambayo itakuwa ya msiba kwa umoja wa vijana.

Mkataba hauelezi kama unaweza kuvunjwa au kuvunjika na nini kifanyike iwapo hayo yatatokea.

Kasoro nyingine kubwa ni kwamba mkataba mradi halisi bali hisia kwamba kutakuwa na jengo la ghorofa 60 bila kufafanua mfumo, uimara na vifaa maalum vya kutumia katika ujenzi.

Aidha, mkataba unasema mwekezaji atatoa Sh. bilioni 16 kati ya 60 bilioni zinazohitajika na ambazo zinapaswa kulipwa na UV-CCM.

Kama huo ndio mgawanyo, kwa nini mwekezaji awe na asilimia 75 ya hisa na UV-CCM wachukue asilimia 25 tu? Hili ni suala linalohitaji kufanyiwa mabadiliko.

Kasoro hizi ndizo zilisababisha CC kuteua Kamati ya watu watatu kupitia upya mkataba huo. Wajumbe wa kamati ni Dk. Abdallah Kigoda, Andrew Chenge na Pindi Chana.

MwanaHALISI ndilo lilifichua mkataba tata katika toleo lake Na. 106 la 16 – 22 Julai 2008 ambapo lilieleza kwa mapana jinsi UV-CCM ilivyojitumbukiza “kwenye mkenge.”

Mara baada ya toleo hilo, Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la UV-CCM, Edward Lowassa aliripotiwa akitishia kushitaki gazeti akisema “limezidi” kumzulia uwongo.

Hata hivyo, hadi sasa Lowassa hajaenda mahakamani wala hajawasilisha malalamiko yake rasmi.

UV-CCM iliingia mkataba na makampuni mawili ya MMISML na ECCL ambalo hakika ni mkandarasi wa ujenzi. Lakini imefahamika kuwa ECCL ni mkandarasi, uhusiano ambao waweza kuleta utata mkubwa kati ya wabia hawa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: