Membe anasaka urais kwa kuchapa kazi jimboni?


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 14 December 2011

Printer-friendly version

KATIKA gazeti la MwanaHALISI la tarehe 7 -13 Novemba 2011, mwandishi Kondo Tutindaga ameandika makala iliyobeba kichwa cha maneno: “CCM na urais wa makanisani.”

Maudhui ya makala yake hiyo, ilikuwa ni vita ya kugombea madaraka ya urais mwaka 2015 ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Anasema wapo baadhi ya viongozi waandamizi ndani ya CCM wanausaka urais kwa udi na uvumba; baadhi yao wameamua kutumia nyumba za ibada kusaka nafasi hiyo.

Miongoni mwa waliotajwa, ni Bernard Membe, waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa. Mwandishi anasema Membe amefadhili ujenzi wa kanisa kubwa katika jimbo lake la uchaguzi la Mtama; na hatua yake hiyo, imelenga mbio za urais.

Wengine waliotajwa kutumia makanisa kutaka kuusaka urais ni mbunge wa Monduli aliyejiuzulu uwaziri mkuu, Edward Lowassa na spika wa zamani wa Bunge, Samwel Sitta.

Mwandishi anasema Membe amekuwa akifanya kampeni zake kwa kujenga makanisa kila mahali katika jimbo lake la Mtama, mkoani Lindi.

Amedai kuwa tayari ujenzi wa baadhi ya makanisa umekamilika. Anasema sasa yuko katika harakati za kutafuta viongozi mashuhuri ambao watakuwa wageni rasmi kwenye sherehe za ufunguzi wake.

Napenda nikiri kwamba namfahamu vema Membe. Ni mbunge wangu na rafiki yangu wa karibu. Hivyo ninapoamua kujitokeza kujibu maelezo yanayomhusu, nikiwa mpigakura wake, nasikitishwa na taarifa hiyo inayolenga kuficha ukweli na kupotosha umma.

Kwanza, mwandishi anataka kuuonyesha umma kwamba mafanikio ya kisiasa na hasa mbio za urais za Membe zinajiegemeza sana katika dini ya kikristo, kama ilivyo kwa viongozi wengine ambao wametajwa kama wanaotumia nyumba hizo za ibada katika kujiweka sawa au hata kujisafisha.

Pili, tuhuma hizo zinalenga kumuonyesha yeye kama kiongozi mdini na ambaye anaangalia ukristo kama ndiyo njia pekee ya kumpatia mafanikio, huku akisahau madhehebu mengine na hasa Waislamu ambao kitakwimu ndiyo wengi katika jimbo la Mtama.

Tatu, kuchanganywa kwa waziri Membe na viongozi wengine ambao wanakabiliwa na kashfa za ufisadi na kukosa uadilifu, kunamaanisha kuwa naye ana upungufu kimaadili na anaamini kwamba dini ni ngao muhimu ya kuficha uovu au upungufu huo.

Wakati si nia yangu kujadili dhamira ya Membe kama ana nia ya kugombea urais wa Jamhuri kwenye uchaguzi wa mwaka 2015, kwa sababu naamini ana haki na sifa za kufanya hivyo akitaka au akiona inafaa, ni dhahiri kwamba mwandishi wa makala hiyo alikuwa na dhamira ya kutaka kumshushia hadhi mhusika.

Nasema hivyo kwa sababu kama mwandishi angefanya juhudi kidogo tu ya kuzungumza na wapigakura wa jimbo la Mtama au hata watu wachache wanaotoka kwenye jimbo hilo wanaoishi jijini Dar es Salaam, angegundua kuwa katika muda wake wa utumishi kama mbunge wa jimbo la Mtama, waziri Membe amefadhili na/au kusimamia ujenzi wa kanisa moja tu lililopo katika kigango cha Rondo Chiponda, ambako ndiko anakotoka.

Kanisa hili lilijengwa baada ya lile la awali lililojengwa na wamisionari wa kizungu zaidi ya miongo mitano iliyopita kuchakaa kupita kiasi katika paa na kuta zake. Mabati yake yalikuwa yanavuja na yanahatarisha usalama wa waumini na wapita njia.

Kwa kuwa yeye ni miongoni mwa waamini katika kanisa hilo, aliamua kulikarabati ili wananchi wapate mahali salama pa kuadhimisha ibada zao.

Ni wazi kuwa suala la uhuru wa kuabudu na kuhakikisha kwamba uhuru huo unatekelezwa katika mazingira ya kibinadamu na yenye staha limekuwa ni kipaumbele chake katika utekelezaji wa ahadi zake jimboni Mtama na wanufaika wakubwa ni waumini wa kiislamu ambao katika awamu yake ya uongozi ya mwaka 2005-2010 wamefanikishiwa ujenzi wa misikiti ya kisasa mitano (msikiti mmoja kila tarafa).

Membe anafanya harakati kuhakikisha kwamba wapiga kura wake wanatekeleza nguzo za dini zao; wala jitihada hazikuanza jana wala juzi. Zimeanza takribani miaka minne iliyopita.

Katika muda huo, amefadhili safari za mahujaji (wa Kiislamu na wa Kikristo) kwenda kutekeleza ibada za hija huko Saudi Arabia (kwa waislamu) na Israel (kwa wakristo); waumini wasiopungua 15 huenda kwenye safari hizo za ibada kila mwaka.

Tofauti nyingine ya Membe na wale waliounganishwa naye, ni kwamba wakati yeye anatenda yote hayo kwenye jimbo lake, wenzake wamekuwa wakipita kila mahali wakiwa na kundi la waandishi wa habari kufungua makanisa na kuendesha harambee.

Aidha, mipango ya Membe haijapata kugeuzwa kuwa mbao za matangazo, na pengine ndiyo sababu mwandishi wa makala ile amekosea katika mambo ambayo ni rahisi sana kuyafahamu.

Kwa mfano, huwezi kufananisha uamuzi wa Membe wa kujenga nyumba za ibada kwenye jimbo lake na mbio za urais ambazo zinahitaji “uwekezaji” kwenye majimbo zaidi ya 290 ndani ya Jamhuri ya Muungano.

Kama Membe anasaka urais ama la sijui lakini kwa hili la kutoa misaada jimboni kwake, kukuhusisha na urais, hakika hakukufanyika kwa haki.

0
No votes yet