Mengi ataja 'mafisadi papa' wanaoitafuna Tanzania


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 28 April 2009

Printer-friendly version
MWENYEKITI Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi

MWENYEKITI Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi amechukua ujasiri wa kipekee na kutaja baadhi ya raia nchini kuwa ni “mafisadi papa.”

Kwenye orodha ya watu watano aliowatuhumu, Rostam Aziz, mbunge wa Igunga na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndiye anatajwa kwanza.

Pamoja na Rostam kuwa karibu na Rais Jakaya Kikwete, ndani na nje ya chama, Mengi amesisitiza kuwa mafisadi hao ndio wanakwamisha juhudi za Kikwete za kupambana na ufisadi nchini.

Watuhumiwa wengine wanne ni wafanyabiashara Tanil Somaiya, Yussuf Manji, Jeetu Patel na Subhash Patel.

Mengi amekuwa raia wa pili kujitokeza hadharani na kutuhumu wafanyabiashara na viongozi wa kisiasa kuwa ni “mafisadi.”

Wa kwanza alikuwa Dk. Willibrod Slaa, mbunge wa Karatu (CHADEMA), aliyetaja viongozi na wafanyabishara 10 kuwa ndio wala nchi hapo 15 Septemba 2007 kwenye mkutano wa hadhara, uwanja wa Mwembeyanga, Temeke jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, jengo la Haideri Plaza, Dar es Salaam, wiki iliyopita, alisema haogopi na katu hatarudi nyuma katika suala la kupiga vita ufisadi nchini.

“Nchi hii ina mafisadi ambao kila kukicha wanaiyumbisha; hawazidi hata kumi. Lakini kuna watano ambao ni ‘mafisadi papa.’ Ukitokea kupigana nao kutokana na ufisadi, wanakuona wewe ni adui,” alisema.

Fuatilia watuhumiwa hao na tuhuma zinazowakabili.

ROSTAM AZIZ: Huyu ni mwanasiasa anayechukuliwa kuwa kinara anayedai kulindwa na kubebwa na nguvu ya kisiasa.

Ametajwa kuhusika na kampuni tata ya Kagoda Agriculture Limited ambayo imekwapua zaidi ya Sh. 40 bilioni kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA). Serikali haijachukua hatua kuhusu tuhuma hizo.

Rostam na kampuni yake ya Afritainer Limited, anatajwa kuwa na uhusiano na Kagoda na kuhusika moja kwa moja na kashfa ya mradi wa umeme wa dharura wa Richmond Development Corporation wenye thamani ya Dola za Marekani 172 milioni (zaidi ya Sh. 206.4 bilioni).

Anatajwa pia katika mradi wa umeme wa Dowans Tanzania Limited iliyorithi mkataba wa Richmond.

TANIL SOMAIYA: Pamoja na kuwa mara nyingi huwa anajificha nyuma ya pazia la watu wengine, Tanil anayemiliki kampuni kadhaa, ikiwamo ya uwakala wa Vodacom ya Shivacom, ni mmoja wa watuhumiwa wakuu wa sakata la ununuzi wa rada ya kijeshi iliyoigharimu serikali ya Tanzania zaidi ya Sh. 70 bilioni.

Tanil anatajwa kupitia kampuni yake aliyoanzisha na mwenzake, Shailesh Vithlani, ya Merlin International Ltd.

Mbali na rada, anatajwa katika sakata la ununuzi wa helikopta za kijeshi zinazodaiwa kuwa za viwango duni. Helikopta hizo sita, aina ya Agusta Bell, ziliuzwa na kina Tanil kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa Sh. 50.7 bilioni.

Tanil na mwenzake wanatajwa katika sakata jingine la magari ya jeshi aina ya IVECO yanayokadiriwa kugharimu Sh. 100 bilioni.

YUSSUF MANJI: Mfanyabiashara anayeonekana kuogopwa na wengi ndani ya utawala, amehusishwa na ukwapuaji wa fedha za EPA na katika uuzaji wa majengo kwa mashirika ya hifadhi ya jamii ya NSSF na PSPF, yenye thamani ya jumla ya Sh. 83.5 bilioni.

Manji alikopa Sh. 9 bilioni kutoka NSSF na kujenga jengo ambalo aliiuzia NSSF tena kwa Sh. 47 bilioni (ikimaanisha amefanya biashara ya Sh. 38 bilioni chapchap) na wakati huohuo akaiuzia PSPF jengo hilo katika mazingira tata kwa Sh. 36 bilioni huku akiendelea kukaa katika jengo hilohilo bila kulipa kodi. PSPF wameamua kumfukuza.

Alikwepa kodi katika mauzo yote hayo hadi waliposhitakiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Kupitia kampuni yake ya Quality Group Limited, Manji anadaiwa kuingiza Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mkenge kwa kuchukua leseni ya kuendesha Bahati Nasibu ya Taifa iliyokuwa inamilikiwa na CCM.

Hadi sasa anadaiwa na kampuni ya CCM ya Tanzania Green Limited, Dola za Marekani 50,000 ambazo zilitumika kulipia leseni kwenye Bodi ya Bahati Nasibu (Gaming Board of Tanzania) 3 Mei 2004.

Hadi Bodi ya Bahati Nasibu inaifuta leseni ya bahati nasibu hiyo iliyokuwa ikiendeshwa na kampuni iliyoanzishwa na CCM ya Gaming Management (T) Limited, Manji hakuwa amelipa fedha hizo.

Manji anatajwa katika kunufaika isivyo halali na mabilioni ya shilingi za misaada kutoka serikali ya Japan za Commodity Import Support (CIS).

JEETU PATEL: Mmoja wa watuhumiwa wakuu wawili wa fedha za EPA ambaye amehusishwa na ukwapuaji wa zaidi ya Sh. 30 bilioni kupitia makampuni yake tisa tofauti.

Tayari amefikishwa mahakamani. Jeetu anatajwa katika kashfa nyingine kadhaa za fedha za nje kama ile ya OGL.

SUBHASH PATEL: Pamoja na tuhuma nyingine, Subhash ndiye aliingia mkataba tata na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kwa ajili ya kujenga na hatimaye kuendesha kitegauchumi hicho kinachodaiwa kuwa na thamani ya Sh. 12 bilioni.

Kwa mujibu wa mkataba huo, yeye kama mbia atamiliki asilimia 75 na kuachia wenye mali asilimia 25 tu. Mkataba huo ulisainiwa kwa baraka za aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa.

Baada ya mkataba huo kufichuliwa na MwanaHALISI, CCM iliushitukia na kuunda kamati ya kuupitia upya ingawa ni vigumu kuubadili kwa kuwa tayari mradi uliishaanza.

Subhash Patel anatajwa katika mradi wa mkaa wa mawe wa Mchuchuma na chuma wa Liganga, mkoani Mbeya ambako anatuhumiwa kutoa rushwa kwa baadhi ya wanasiasa, tuhuma ambazo zimefika ndani ya Bunge.

Ilielezwa ndani ya bunge kwamba Subhash alitoa rushwa ya mabati 500 na tani 29 za saruji pamoja na kusafirisha baadhi ya viongozi wa eneo la Mchuchuma hadi Dar es Salaam alikowalaza katika hoteli yake ya kitalii ili akabidhiwe eneo la ekari 1,400.

Mbunge mmoja alisema bungeni, “Pamoja na hayo, wananchi wetu tuwaombe watuelewe kwamba tukipeleka bati 500 Mchuchuma, tumeuza nchi, ni sawa na kuuza ng’ombe kwa kesi ya kuku.”

Mengi aliwaambia waandishi wa habari kwamba malengo yake ni kutimiza ndoto za Rais Jakaya Kikwete ambaye anataka “Maisha bora kwa kila Mtanzania.”

0
Your rating: None Average: 3 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: