Mengi: Siwezi kufilisika


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 14 March 2012

Printer-friendly version

REGINALD Mengi, mfanyabiashara na mtoa misaada kwa makundi mbalimbali ya jamii amesema hawezi kufilisika.

“Hata ningeishi kwa zaidi ya miaka 1,000, sitafilisika,” alisema jijini Dar es Salaam, Jumamosi iliyopita katika viwanja vya Mnazimmoja.

Mengi alitoa kauli hiyo baada ya kutunukiwa shahada ya heshima ya uzamivu (Ph.D) kutoka chuo kikuu cha Japan kinachotoa elimu ya Biblia kiitwayo Japan Bible Insitute (JBI).

Amesema, “Kila kitu nilichonacho ni mali ya Mungu. Nilikuja (duniani) mtupu; nitaondoka mtupu…”

Huku akitambua utajiri alionao na viwango vya fedha anazotoa kwa vikundi vya wahitaji katika jamii mwaka hadi mwaka, Mengi alisema, “Mimi ni masikini na masikini huwa hafilisiki.”

Shahada aliyopewa Mengi ni ya heshima inayotambua “juhudi zake za kusaidia makundi mbalimbali ya watu na kwa kutambua mchango wake kwa kanisa…”

Mengi, mmoja wa wafanyabiashara wakuu nchini, ni mwenyekiti wa makampuni ya IPP na amejitambulisha kwa miaka mingi nchini kuwa, mtoa misaada kwa wenye ulemavu, watoto wanaoishi katika mazingira magumu na walioathirika kwa ukimwi.

Mfanyabiashara huyo hutoa pia misaada kwa vikundi mbalimbali vya kijamii vikiwemo vya wanawake, hasa vikoba; saccos na watu binafsi.

Amesema hana hofu ya kufilisika kwani “…kila kitu nilichonacho ni mali ya Mungu.”

Kuna wanaoogopa kutoa misaada kwa wahitaji kwa kuogopa kufilisika, amesema na kuongeza, “…siwezi kufilisika kwa kuwa Mungu yuleyule yungalipo.”

0
No votes yet