Meremeta, Serikali, na Mafisadi


George Marato's picture

Na George Marato - Imechapwa 15 April 2008

Printer-friendly version

KILIO kinaendelea kwa miaka mitano sasa katika vijiji sita vya Kata ya Buhemba, Wilaya ya Musoma ambapo kuna mgodi wa dhahabu uliokuwa unamilikiwa na kampuni ya Meremeta.

Zaidi ya nyumba 100 zilivunjwa ili kupisha mgodi uliotangazwa kuwa ni wa serikali. Wananchi waliachwa bila kinga ya jua, mvua na upepo. Mashamba yaliharibiwa.

Zahanati iliyokuwa ikitoa huduma kwa wakazi wa vijiji hivyo ilivunjwa. Shule ya msingi iliyokuwa na wanafunzi wapatao 600 wa darasa la kwanza hadi la saba ilivunjwa.

Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) iliyoitwa Buhemba ilivunjwa. Askari walihamishwa kwa mikokoteni ya kukokotwa na ng'ombe ili kupisha mgodi. Askari wengi hadi sasa bado wanapanga katika vijiji vya Butiama, Rwamkoma na Bisarya.

Hivyo ndivyo mgodi wa dhahabu wa Buhemba ilivyonyanyasa wananchi; kuvuruga miundombinu ya afya na elimu, pamoja na mfumo wa maisha wa wakazi wake kwa ujumla. Mbiu ilikuwa kupisha mgodi wa serikali.

Buhemba ni kilometa 49 kutoka Musoma mjini, mkoani Mara. Ni katika Kata ya Buhemba yenye vijiji sita ambavyo ni Byatika, Magunga, Matongo, Milwa, Talani na Kinyalili ambako shughuli kuu ni ufugaji na kilimo cha mahindi, maharage, viazi vitamu na muhogo.

Vilio vya wananchi katika eneo linalozunguka mgodi vilianza miaka sita iliyopita pale waliposhawishiwa, na wengine kulazimishwa kuhama, ili kutoa nafasi kwa uchimbaji wa dhahabu.

Viongozi waliofika Buhemba kabla ya mgodi kuanza, walisema huo ulikuwa mradi wa serikali na kwamba mapato kutokana na mgodi yangeboresha maisha ya wanavijiji.

Si hayo tu. Viongozi walisema kwamba mgodi huo ulikuwa na lengo la kusaidia Jeshi la Wananchi (JWTZ), kikosi cha Nyumbu. Uchimbaji ulianza rasmi mwaka 2002.

Diwani wa Kata ya Buhemba, Vitalis Odero ndiye kitabu cha historia cha vilio vya wananchi. Anasimulia kwa uchungu jinsi wananchi walivyoswagwa nje ya makazi na kuharibiwa kwa miundombinu yao.

Wananchi walipoteza zahanati iliyohudumia wananchi wengi wa vijiji sita. Leo hii, wanatembea kilometa 25 kwenda kijiji cha Butiama kufuata huduma za afya.

Wanafunzi wapatao 600 waliokuwa wanasoma katika shule iliyovunjwa, walisambazwa kwenye shule nyingine na kusababisha usumbufu mkubwa wa kutembea masafa marefu.

Vitalis Odero anasema, "Tuliahidiwa huduma bora mbalimbali za jamii ikiwa ni pamoja na kujengewa shule, vituo vya afya na barabara. Tuliamini kuwa, kwa vile mgodi ulikuwa mali ya serikali, wananchi wangenufaika."

Kwa miaka minne ya uchimbaji dhahabu, Meremeta haikutimiza ahadi hata moja kwa wananchi na viongozi waliotoa ahadi hawapatikani kujibu maswali.

Walichoambulia wananchi ni kukamatwa ovyo mara kwa mara na kupigwa na walinzi wa kampuni kwa madai ya kuingia katika eneo la mgodi. Kwa muda wote wa uhai wake, uongozi wa Meremeta haukuwahi kuitisha mkutano wowote kuzungumza na wananchi.

Kwa upande wa uchafuzi wa mazingira, uchimbaji umeacha mashimo makubwa na marefu ambayo wananchi wanalalamika kuwa ni "makaburi yao na mifugo yao."

Diwani Odero anasema uchimbaji umesababisha uharibifu wa mito miwili:  Nyabigori na Kinyonga. Hii ilikuwa chanzo cha maji safi kwa wakazi wa vijiji hivyo.

"Mito hii ilikuwa tegemeo kubwa kwetu kwa matumizi mbalimbali. Sasa imeharibiwa kwa kemikali mbalimbali kutoka kwenye shughuli za mgodi," anasema Odero.

Hivi sasa, wakazi wa eneo linalozunguka mgodi wananunua maji. Ndoo moja inauzwa hadi Sh.500. Hii ni nyongeza kwa dhiki za wakazi hawa na mtihani mgumu wa utawala bora kwa watawala.

Odero amesema, "mifugo yetu ikinywa maji ya mito hii inakufa. Ukipanda mazao kando ya mto, ama hayaoti kabisa au yanaota na kukauka baadaye." Madai haya ya wakazi bila shaka yanahitaji kuthibitishwa kisayansi.

Karibu na eneo la mgodi kulikuwa na bwawa. Linaitwa Kiarano. Lilijengwa na serikali ya Mwalimu Julius Nyerere kwa lengo la kutoa huduma ya maji ya kunywa na kunyweshea mashamba kwa wakazi wa vijiji vya kata ya Buhemba.

Hivi sasa maji ya Kiarano yamepungua sana kutokana na matumizi makubwa ya katika mgodi, lakini pia ubora wa maji umetoweka kutokana na mwingiliano wa kemilaki za mgodini. Maji haya hayafai tena kwa matumizi ya binadamu na mifugo, wanaeleza wakazi wa Buhemba.

Vilima vingi vyenye mawe, miti na nyasi, vinavyosemekana kusheheni utajiri wa madini mbalimbali ikiwemo dhahabu, na ambavyo vilidhihirisha mandhari ya asili ya Buhemba, sasa vimepotea.

Badala yake kuna mashimo ya vina virefu. Hadi sasa watu wawili na ng'ombe wapatao 10 wamekufa baada ya kuanguka kweye mashimo hayo. Haya yanathibitishwa na diwani wa Kata ya Buhemba.

Kwa maelezo ya serikali, mgodi wa dhahabu wa Buhemba sasa umefungwa kutokana na "uzalishaji kupungua" na Meremeta "imefilisiwa."

Swali kubwa ni je, kweli Meremeta ulikuwa mradi wa serikali? Kama jibu ni ndiyo, vipi serikali inaweza kubomoa shule, zahanati, nyumba za kuishi, kuharibu mashamba na mazao ya wananchi bila kuwafidia?

Vipi serikali inaweza kuteketeza vyanzo vya maji safi ya wakazi wa Buhemba – mito miwili na bwawa – na kuwaacha wananchi wake katika hatari ya magonjwa na kifo?

Kama Meremeta ilikuwa mali ya serikali, na shabaha yake ilikuwa kusaidia kikosi cha JWTZ cha Nyumbu, vipi mafao ya kampuni hiyo hayakuwatoa katika dhiki, askari wa JKT waliohamishwa Buhemba baada ya kambi yao kuvunjwa?

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Dk. Kanael Kimat Kunei anasema Meremeta haikuwahi kutoa hata senti moja kuchangia maendeleo wilayani humo.

Uhalali au uharamu wa Meremeta ni suala linaloendelea kuchunguzwa. Kilichokamilika ni Meremeta kufilisiwa na waliorithi mali na madeni, TANGOLD kulundikiwa na serikali zaidi ya Sh. 10 bilioni.

Sasa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovic Utouh anasema Meremeta siyo mradi wa serikali na ofisi yake haijawahi kukagua hesabu zake.

(Mhariri: Kuna serikali ngapi nchi hii? Moja inamiliki Maremeta na nyingine inakana Meremeta. Serikali ipi inasema ukweli?)

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: