Meya, ofisa kilio kitupu


Editha Majura's picture

Na Editha Majura - Imechapwa 10 February 2010

Printer-friendly version

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete, amefanya ziara ya siku tatu mkoani Dar es Salaam kwa staili ya aina yake. Amebeba watendaji wa serikali ili wawe wanajibu maswali.

Je, wenyeviti wa vyama vingine vya siasa wakihitaji kusindikizwa na watumishi hao wa serikali, watawapata? Hawa ni watumishi wa umma, si wa CCM.

Hata hivyo, watumishi wachache waliotarajiwa kuwepo hawakuwepo. Hata walioitika wito huo, badala ya kujibu maswali kama walivyotakiwa, walianika matatizo yanayowakabili.

Mara rais akaita muhusika mkuu wa huduma ya ardhi ajibu maswali. Aliyejitambulisha kuwa ni Kamishna Msaidizi wa ardhi, Joseph Shewiyo, akasogelea kipaza sauti.

Akajihami kwa kuanza kueleza mgawanyo wa utendaji kazi zao. Rais akamkatisha kwa kumwambia, “Majibu usiyoyajua sawasawa usitupe sisi. Si kuna bibi au bwana ardhi wa wilaya, eh? Wako wapi?” Alihoji rais.

Swali hilo halikujibiwa wala walioitwa hawakuwepo. Rais akaendelea kusema, “Wadogo zako hawapo bwana; jibu maswali yako.”

Mwenyekiti wa serikali ya mtaa Mivumoni akataka kufahamu kwa nini hawajagawiwa viwanja vilivyopimwa katika mradi wa viwanja wa manispaa, wakati viwanja viliishapimwa.

Kamishna: Awali mradi ulikuwa ukitekelezwa na wizara kwa majaribio. Agizo likatolewa kwamba upelekwe kwa manispaa. Ikaamriwa fedha za mradi zigawanywe kwenye manispaa. Hilo likatekelezwa kwa manispaa zote, zikiwemo za mkoani Morogoro. Asilimia kubwa ya manispaa zimefanikisha miradi hiyo isipokuwa manispaa ya Kinondoni.

Wizara ikalazimika kutekeleza jukumu hilo tena, katika manispaa ya Kinondoni. Tayari mazungumzo na wananchi yamefanyika. Tatizo lipo kwenye kulipa fidia. Manispaa iliweka mazingira magumu…(Rais akamkatisha).

Rais: Mbona unaenda mbali? Swali ni dogo sana, wanasema hivi, mmewaahidi viwanja, tayari vimepimwa, mbona hamuwapi? Mbona mnawasumbua? Wajibu hilo. Kama watu wako wamefanya madudu, sema tu.

Kamishna: Tatizo (bila kulitaja) bado linashughulikiwa na viongozi wa manispaa kwa kushirikiana na wizara.

Rais: Ni kiongozi yupi wa manispaa anashughulikia tatizo hilo, maana wewe ndiye wa wizara, manispaa ni wawili, mkurugenzi na meya? Wote wapo hapa. Tueleze ni yupi kati yao?

Kamishna: Kimya.

Ndipo Meya wa manispaa ya Kinondoni, akanyanyuka bila kuitwa na kuelekea kilipo kipaza sauti, na bila kujitambulisha akasema, “Swali la kiongozi wa Mivumoni ni la msingi sana…”

Wananchi (kwa pamoja): Taja jina lako (Ni katika ukumbi wa Vijana, Kinondoni).

Meya: Jina? La nani? Mimi?

Wananchi: Ndiyo wewe.

Meya: (Kama anayehamaki)He! Haya, naitwa Salim Salehe Londa, Meya wa Manispaa ya Kinondoni.

Londa alieleza kuwa manispaa ilitekeleza jukumu hilo vizuri. Tatizo lilijitokeza wakati wa kuwalipa fidia wenye ardhi ambapo baadhi waligoma kupokea fidia zao. Alisema walitaka nao wagawiwe viwanja lakini hilo halikupatiwa ufumbuzi.

Alieleza kuwa kiini cha mradi huo kushindikana si wananchi wala manispaa, bali wizara ya ardhi ambayo huingilia kazi za manispaa.

Alisema wizara, badala ya kusimamia sera na mipango, inaingia na “kucheza ngoma yenyewe.” Hawataki hata kutoa hati za kumiliki ardhi. Hati zilizoombwa tokea 1986 hazitolewa hadi sasa.

Londa alieleza kwamba rais akitaka maswali kutoka kwa viongozi hao katika huduma ya ardhi, kila mtu ana swali, tena la msingi. Aliongeza, “Hata mimi nina malalamiko yangu mengi kuhusu ardhi.”

Je, hapa ahadi za CCM zimetekelezwa kiasi cha kujiamini na kuahidi kushinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: