Mgawanyiko ndani ya CCM: Rais Kikwete anakimbia kivuli chake


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 01 November 2009

Printer-friendly version

UKWELI ni upi? Baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanakiri kuna mgawanyiko ndani ya chama chao.

Lakini Rais Jakaya Kikwete, ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa CCM, anasema chama hakina mgawanyiko wowote.

Akizungumza na wanachama wa CCM mkoani Mara wiki iliyopita, Kikwete alisema, “Ndani ya CCM hakuna mgawanyiko.” Alisema, “Mgawanyiko uko magazetini na ndani ya Bunge.”

Alihoji, “Hivi hapa Mara kuna mgawanyiko? Mwanza kuna mgawanyiko? Hivi Tanga kuna mgawanyiko? Singida umesikia kuna mgawanyiko?

Kwa ukakamavu akaongeza, “Ugomvi uko palepale bungeni. Wakiondoka wanauacha pale, wakirudi bungeni wanaendelea nao. Mgawanyiko huu tunaoambiwa kila siku hauko Musoma wala Bagamoyo.”

Hata hivyo, Rais Kikwete alisema ana uhakika kuwa jopo la watu watatu walioteuliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho, kutafuta chanzo cha mpasuko, litaweza kumaliza mvutano wa makundi hayo mawili na kupata mwafaka wa kudumu.

Jopo hilo linaongozwa na Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi. Wajumbe wake ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Pius Msekwa na Spika wa zamani wa Baraza la Kutunga Sheria la Afrika Mashariki, Abdulrahman Kinana.

Hapa ndipo rais anapothibitisha kuwa hakusema ukweli pale alipowaambia wanachama wake kuwa ndani ya CCM hakuna mgawanyiko.

Ndani ya bunge kuna minyukano ya wazi. Inaonekana kwa kila mmoja; wakati ndani ya chama mambo mengi hufanyika gizani. Hilo hata rais analijua.

Kwa mfano, rais anajua kuwa hata mkoani Mara ambako aliwaeleza wanachama na viongozi wake kuwa mambo ndani ya chama chao ni shwari, hali ni tofauti. Hata mikoa mingine aliyotaja, lipo jambo.

Mkoani Mara, CCM imegawanyika mapande mawili. Moja ni lile linaloongozwa na mjumbe wa NEC, Christopher Gachuma na jingine ni lile la mpinzani wake wa kisiasa, Enock Chambiri.

Makundi haya yamekuwapo kwa muda mrefu. Yanafahamika. Hata Kikwete anayafahamu. Hata uhasama kati ya makundi haya unajulikana tangu Kikwete hajaingia ikulu.

Kundi moja la hayo mawili likiunga mkono mgombea, jingine humkataa na kuunga mkono mgombea tofauti, hata kama mgombea huyo anatoka upinzani.

Na hili limejidhihirisha mara nyingi na katika maeneo mbalimbali. Kwa mfano, katika uchaguzi mkuu wa CCM mwaka 2002, Gachuma alimuunga mkono Dk. Magoti katika nafasi ya uenyekiti wa mkoa.

Wabunge wote saba wa mkoa wa Mara, ukimuondoa aliyekuwa mbunge Tarime mjini, Kisyeri Chambiri ambaye ni mdogo wa Enock, hawakuwa na Chambiri. Waliunga mkono mgombea wa Gachuma. Wale waliokuwa wanamuunga mkono Chambiri hawakuunga mkono mgombea wa Gachuma.

Hivyo basi, pamoja na kwamba Gachuma alishinda kwa kishindo nafasi ya NEC aliyokuwa anaiwania, lakini alishindwa kupitisha mgombea wake, Dk. Magoti.

Hadi sasa ikiwa ni zaidi ya miaka saba, uhasama kati ya makundi hayo mawili bado mbichi. Kinachopunguza joto ni Chambiri kutokuwa katika nafasi za juu za uongozi katika safu ya mkoani.

Lakini hiyo haiwezi kusemwa kuwa wafuasi wa kundi la Chambiri na hata Chambiri mwenyewe wanaweza kupikwa chungu kimoja na wale wa Gachuma au Gachuma mwenyewe.

Matokeo ya uchaguzi wa ubunge jimboni Tarime mwaka 2005 na uchaguzi mdogo wa mwaka 2008, yanathibitisha ni makundi hayo mawili yalioiangusha CCM.

Taarifa za ndani ya CCM zinasema kuwa katika uchaguzi wa 2005, Kisyeri Chambiri, aliyekuwa anatetea kiti, alishindwa katika kinyang’anyiro cha ubunge baada ya kuhujumiwa na kundi la Gachuma.

Wafuasi wa Gachuma walifanya kampeni za wazi za kumpinga Chambiri. Matokeo yake Kisyeri alishindwa na mgombea wa Chadema, Zakayo Chacha Wangwe. Hali hiyohiyo ilikuwa kwa wagombea wa udiwani. Wafuasi wa Chambiri waliangushwa.

Matokeo yake, jimbo la Tarime na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ikatwaliwa na Chadema. Chambiri hakuridhika. Akajipanga kulipiza kisasi.

Uchaguzi mdogo ulipofika, Chambiri alielekeza wafuasi wake kumpigia kura mbunge wa upinzani, Charles Mwera kwa madai kuwa aliyekuwa amepitishwa na CCM “alikuwa mfuasi wa Gachuma.”

Haya yote Rais Kikwete anayafahamu au alipaswa kuyafahamu.

Lakini kama hiyo haitoshi, ni yeye aliyeamuru Gachuma na Chambiri kugombea ujumbe wa NEC kupitia nafasi 20 za kundi la Tanzania Bara, badala ya uenyekiti wa mkoa. Katika kinyang’anyiro hicho, Gachuma alifanikiwa kupenya, lakini Chambiri alianguka.

Kushindwa kwa Chambiri katika kinyang’anyiro hicho, hata hivyo, hakukuwezesha kummaliza kisiasa mkoani. Hii ndiyo maana mgombea wa CCM mwaka 2005 alishindwa na yule wa upinzani. CCM waligawana kura na matokeo yake kumpa nafasi mgombea wa upinzani kupenya. Tuondoke Mara.

Hali ya mgawanyiko ipo mikoa ya Shinyanga, Mbeya, Singida, Kilimanjaro, Kagera, Tanga, Dar es Salaam, Arusha, Tabora, Manyara hadi Zanzibar. Ni makundi na kuparurana kila kona.

Kwa mfano, mkoani Arusha mgawanyiko ni mkubwa, huku makundi mawili makuu yakipingana ndani ya chama hichohicho.

Kielelezo cha mpasuko mkoani Arusha ni kesi dhaifu ya rushwa iliyofunguliwa kwa wabunge wawili wa mkoa, Michael Lekule Laizer na Elisa David Mollel.

Ni kutokana na mgawanyiko huo, viongozi wa CCM waliamua kuiacha kesi kuendelea hadi mwisho. Hadi sasa, makovu yaliyotokana na kesi hiyo hayajapona.

Hata kesi inayomkabili mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka, anayetuhumiwa kumtishia kwa bastola Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UV-CCM) Mkoa, James Milya, ni zao la mgawanyiko katika chama chao.

Hivi sasa makundi hayo yamepanuka na kuingia katika ngazi ya ubunge. Vita kati ya Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Batilda Burian na mbunge wa sasa wa Arusha mjini, Felix Mrema, ni kielelezo kingine kuwa hali si shwari kama mwenyekiti wa taifa wa CCM anavyosema.

Hata katika mkoa wa Mbeya, rais anajua kuna makundi yanayotokana na yeye mwenyewe kuendelea “kumbeba” Mkuu wa Mkoa, John Mwakipesile anayetuhumiwa kupambana waziwazi na mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe.

Mwakipisile na Mwakyembe walishindana katika kinyang’anyiro cha ubunge wa jimbo hilo katika uchaguzi mkuu wa 2005. Mwakyembe alishinda. Haikutarajiwa Kikwete kumbakisha Mwakipesile Mbeya, kama kweli alidhamiria kumaliza mgawanyiko na uhasama wa makundi.

Ni makundi hayo yaliyozaliwa kutokana na mvutano wa Mwakyembe na Mwakipesile yaliingiza hata wasiokuwamo. Majuzi, vigogo wa chama hicho walimuita mkoani mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale-Mwiru, kusimika kile kinachoitwa, “Makamanda wa UVCCM.”

Wengi wa waliosimikwa ni wale waliokwishaonyesha au kutangaza nia ya kugombea ubunge mwakani katika baadhi ya majimbo. Twende Tanga.

Katika mkoa huu, tayari kuna madai mazito kwamba Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba anaendesha “kampeni ya kumwondoa” William Shellukindo katika kiti cha ubunge ili apachike mtoto wake, Januari Makamba katika jimbo la Bumbuli ukija uchaguzi mkuu mwakani.

Makamba hajakanusha madai haya. Tayari taarifa zinazohitaji kuthibitishwa zinasema makundi yameanza kuota ndani ya chama, na sasa hali ya Tanga si shwari tena.

Tuje Tabora. Spika wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta anadaiwa kubeba baadhi ya viongozi, hasa mwenyekiti wa chama mkoa na kiongozi mashuhuri, Ismail Aden Rage, huku wenzake wakichukua wengine.

Katika mazingira haya, ndimo wanatajwa mbunge wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya na yule wa Igunga, Rostam Aziz kuwa upande mwingine. Taarifa zinasema makundi haya mawili yamegawa wanachama na viongozi. Kila kundi limebeba wafuasi wake.

Tuangalie mkoa wa Shinyanga. Nako mambo ni yaleyale, mgawanyiko wa chama. Baadhi ya viongozi wakiwamo wabunge, hawapikiki chungu kimoja na viogozi wenzao.

Kwa mfano, huwezi kusema kundi la mwenyekiti wa mkoa, Khamis Mgeja linaweza kukaa meza moja na lile la wanachama wengine wanaomuunga mkono mbunge kama John Shibuda au James Lembeli. Huwezi.

Mkoani Dar es Salaam wala hakuna ubishi kuwa mambo nako si shwari. Mjumbe wa NEC, Ramadhani Madabida amebeba wafuasi wake wanaopambana na wale wa mwenyekiti, John Guninita.

Ni kutafunana kwa makundi haya mawili kulikosababisha Makamba na mjumbe wa NEC, Salum Londa ambaye pia ni meya wa Manispaa ya Kinondoni, kuangukia pua katika kesi yao dhidi ya mbunge wa Chadema, Halima Mdee.

Kama ilivyo katika mikoa mingine, makundi yanayotafunana katika mkoa wa Dar es Salaam yamebeba wabunge na madiwani pia.

Hata katika mkoa wa Kilimanjaro, mambo ni kama huko kwingine. Tofauti yake na mikoa mingine, ni kwamba hapo kuna msuguano kati ya “wakuja” na wenyeji katika chama.

Kwa mfano, kundi moja linalombeba Thomas Ngawaiya (akiitwa wa kuja), halipikiki chungu kimoja na kundi linaloongozwa na naibu waziri, Dk. Cryrill Chami.

Hali hiyo inafanana na ile ya makao makuu ya CCM Dodoma, ambako Makamba, katibu mkuu, amebeba wahamiaji kutoka vyama vya upinzani na kuwapa vyeo na kuacha makada waliokibeba chama chao kupitia mazingira magumu.

Katika mazingira hayo, haikutarajiwa Rais Kikwete kukana ukweli kuwa mbali na kwenye bunge, hata ndani ya CCM, makundi ya wanachama yametamalaki na mgawanyiko umeshamiri.

Kwa hatua yake hiyo ya kutoeleza hali halisi ilivyo, hajengi chama chake, haweki misingi ya kumaliza makundi yaliyopo; na aweza kuwa anaangamiza chama na kujiangamiza mwenyewe.

Je, kwa hali iliyopo mkoani Mara na inayofahamika kwa viongozi, wanachama na wananchi wengine, rais alionekanaje mbele yao? Je, kanusho lake limemjenga au linambomoa?

Haihitajiki elimu ya juu kubaini kuwa kilichotokea katika kikao cha NEC kilichopita, ambapo wajumbe waliparurana hadi kufikia hatua ya kuundwa kwa kinachoitwa, “Kamati ya wazee wenye busara,” ni ushahidi wa kuwapo mgawanyiko ndani ya CCM.

Kusingekwa na mpasuko, NEC isingekuwa na sababu yoyote ya kuunda kamati ya Mwinyi; Spika Sitta asingesulubiwa; wajumbe wengine wakiwamo wale wa Kamati Kuu wasingetuhumiwa kufadhili upinzani.

Wala Makamba asingelazimika kumtafuta mwenyekiti wake kumuomba aruhusu wajumbe “waseme, kwani wanayo ya kusema,” muda mfupi kabla ya kikao cha NEC kilichomsulubu Sitta. Mgawanyiko upo tena mkubwa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: