Mgombea huyu hafai kuwa rais


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 29 September 2010

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

UKIWAULIZA Watanzania leo ‘popo ni mnyama au ni ndege’ utapata majibu yanayoonyesha kiwango cha uelewa wa kila mtahiniwa. Lakini jibu sahihi ni mnyama.

Watu wanaomwona popo akiruka watajibu ni ndege na wale waliosomea elimu ya viumbe watajibu ni mnyama. Uongozi wa juu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) una popo, watu wanaojifanya rafiki hali ni adui wakubwa – hawaeleweki.

Kamusi ya Kiswahili Sanifu inasema mnafiki ni mtu anayesema kinyume cha anavyotenda; mtu anayetoa ahadi na kisha asitimize; mzandiki. Je, ahadi za mwaka 2005 zimetimizwa.

Kamusi hiyo hiyo inasema unafiki ni hali ya kujifanya rafiki kumbe ni adui; hali ya kutokuwa mkweli.

Maana haiwezekani kiongozi apande jukwaani kulaani mafisadi, lakini akishuka chini anawaita mafisadi na kustarehe nao.

Najua tumetumia mifano hii mara kadhaa, lakini bado tutaendelea kuandika tukitumia mifano hii hadi masikio ya “viongozi popo” yazibuke na wananchi wajitenge na viongozi hao ndani ya CCM maana ni wanafiki kwa asilimia 100.

Wananchi bado wanakumbuka namna mwenyekiti wa CCM alivyomshughulikia kwa namna ya kipekee Hussein Bashe; akamvua uraia, akamwengua kugombea ubunge jimboni Nzega na kumnyang’anya vyeo vyote ndani ya chama chake. CCM wakashangilia asulubiwe.

Baada ya mambo kuwa magumu kwenye uwanja wa kampeni, Bashe ameitwa asaidie kuokoa jahazi aondoe mdororo ili chama cha Kikwete kishinde. Je, huu si unafiki? Mtu asiyefaa atasaidiaje wanaofaa?

Frederick Mwakalebela aliibuka mshindi katika kura za maoni jimbo la Iringa Mjini. Akahujumiwa kwa kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru). Akakamatwa na kufunguliwa kesi mbaya ya rushwa.

Walilotaka likawa. Jina lake lilipofika katika vikao vya uteuzi, mwenyekiti Kikwete akalichakachua akidai anakabiliwa na kesi ya kukosa uadilifu.

Lakini, wiki iliyopita, aliitwa katika mkutano wa kampeni mjini Iringa. Yuleyule aliyembambikia Mwakalebela kesi, aligeuka na kumsifu kuwa ni shupavu.

Sijui ni shupavu kwa lipi; rushwa aliyodaiwa kutoa? Kwa hiyo, kesi yake ni geresha? Asiye na maadili anakuwa shupavu? Kama huu si unafiki ni nini?

Mwaka 2006 nchi wahisani zilisusa kutoa misaada kwa madai hazijafanyika juhudi za kutosha kufanyia mageuzi Taasisi ya Kupambana na Rushwa (Takuru). Haraka haraka serikali ikafanyia marekebisho na kuunda taasisi inayojulikana leo kama Takukuru.

Kila anakopita Kikwete anatamba kuwa ameipa taasisi hiyo meno na anajisifu kwamba amewafikisha vigogo kortini kwa matumizi mabaya ya madaraka na wengine ameridhia kujiuzulu.

Kumbe hana dhamiri safi. Wakati kesi za watuhumiwa, mbunge wa Rombo, Basil Mramba na aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara Daniel Yona hazijaisha, mwenyekiti huyu amegundua kesi zinamwekea kiwingu katika kampeni zake za kurudi Ikulu.

Akavaa joho la popo akaruka hadi Rombo kuomba kura na kumnadi Mramba akidai ni mzee kijana ambaye mawazo yake yanawafaa sana.

Hajasema, mawazo yapi yanawafaa vijana? Yale ya kutumia vibaya madaraka? Kwa viwango vyovyote vile, huu ni unafiki.

Maana haiwezekani kiongozi huyo huyo akaagiza vijana wake wamfungulie kesi Mramba halafu akaruka kwa chopa na kuwaambia wananchi wasijali kesi iliyoko kortini ila wamchague mshtakiwa aliyepo mbele yao.

Kwa hiyo, kesi ile ni “babaishabwege” kama wanavyosema vijana mitaani?

Kabla ya kufika Rombo alikwenda kwa swahiba wake, Edward Lowassa kule Monduli. Akamsafisha kwa utuli waziri mkuu huyo wa zamani akisema, “Yaliyopita si ndwele, tugange yajayo.”

Kwa tafsiri nyepesi, Kikwete alitaka kusema kwamba zile tuhuma kwamba Lowassa alihusika katika kashfa ya Richmond alitungiwa tu na wabaya wake bungeni.

Kama alilijua hilo, kwa nini aliridhia kujiuzulu kwake? Kwa nini aliridhia kujiuzulu kwa Nazir Kamaragi, Dk. Ibrahim Msabaha kwa kashfa ile?

Ilani ya CCM mwaka 2005 ilionyesha, uchumi wa nchi ulikuwa umepanda kutoka asilimia 4 hadi asilimia 6.7 na kwamba kazi ilikuwa kuhakikisha unafika asilimia 10.

Lakini mwenyekiti wa CCM anapita akidai yeye ndiye amekuza uchumi kutoka asilimi 4 hadi 6.7. Jamani, huu si uongo?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: