Miaka 15 ya mwisho ya Eugene Maganga


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 06 October 2010

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
Eugene Maganga

WAKATI Eugene Maganga na wenzake wakipanga maasi dhidi ya serikali ya Mwalimu Nyerere mwaka 1982, nilikuwa na umri wa miaka miwili hivi.

Kwa hiyo, mimi sikujua lolote kuhusu tukio hilo wakati huo. Nilianza kusikia tukio hilo kupitia mazungumzo ya baba yangu na majirani au rafiki zake sebuleni kwetu, eneo la Polisi Ufundi, Dar es Salaam, katika miaka ya 1990.

Miaka michache baadaye nilipata bahati ya kuonana na ‘kufanya’ kazi na Maganga, aliyefariki dunia hivi karibuni, kwa ugonjwa wa kisukari katika hospitali ya Amana, Ilala.

Nilionana naye kwa Mara ya kwanza Aprili mwaka 2002, nilipoitwa kwenye usaili katika iliyokuwa kampuni ya Habari Corporation. Pamoja nami walikuwepo watu wengine zaidi ya 90, akiwamo Maganga.

Katika mazungumzo tuliyofanya kabla na baada ya kuitwa kwenye chumba cha usaili, Maganga alikuwa akinisisimua kwa masimulizi yake kuhusu tukio hilo la mwaka 1982.

Mchana nikaanza kusikia njaa lakini kwa vile sikutaka kukosa ‘hadithi’ zake, nilimwomba niende naye kula ili niendelee kufaidi. Akakubali.

Mimi ndiyo kwanza nilikuwa nimemaliza masomo ya kidato cha sita na sikuwa na kazi yoyote. Kwa bahati nzuri, baba yangu, marehemu Peter Kamwaga (Mungu amrehemu), alikuwa amenipa fedha za matumizi siku hiyo.

Nikatoa ofa kwa Maganga na kwa mwenzetu mwingine Deogratias Rutahindurwa. Ile ndiyo ofa niliyoifaidi.

Baadaye nilikuja kugundua kwamba Maganga alikwenda kwenye usaili ule kwa mguu, na alidai hakuwa amekula chochote na hakutaraji kula chochote baada ya mlo ule wa mchana tuliokula pamoja !

“Kijana, leo umeniokoa kweli. Nilikuwa sijanywa maji wala chai hadi sasa. Nakushukuru sana na Mungu akubariki,” hayo yalikuwa maneno yake kwangu na kufahamiana kwetu kukaanzia siku hiyo.

Kwa bahati mbaya kwake, hakufanikiwa kuajiriwa na kampuni hiyo, lakini alipewa ajira ya muda kuandika kwa kina tukio hilo kwenye gazeti la Rai.

Sisi wawili tuliajiriwa; mimi kama mwandishi na Ruta kama Mhariri wa Michezo wa The African. Maganga alisema kwa utani kwamba hakutaraji kupata kazi hiyo. “Nani anataka kuajiri mhaini?” alihoji.

Tangu alipoachiwa kutoka katika gereza la Butimba mkoani Mwanza mwaka 1995 kwa msamaha wa Rais Ali Hassan Mwinyi, Maganga, alidai aliishi maisha magumu.

Alidai jamii, wakiwamo ndugu, jamaa na marafiki zake, hawakuweza kumsamehe kwa kosa lake la kutaka kupindua serikali ya Mwalimu Nyerere. Hili ndilo kovu alilokwenda nalo kaburini.

“Ezekiel, mimi nafahamu watu waliofanya makosa huwa wanasamehewa. Mimi nilifanya kosa miaka mingi iliyopita lakini pamoja na kutumikia kifungo, watu bado hawajanisamehe.

“Ndani kabisa ya moyo wangu ninaamini sikukosea kwa kutaka kumpindua Nyerere. Watanzania walikuwa wanaishi maisha mabaya sana wakati huo. Tatizo nililonalo ni kwamba sijasamehewa tangu wakati huo,” aliniambia.

Hakuwahi kupata kazi na alidai, baadhi ya rafiki zake wa zamani walifikia hatua ya kumkimbia waziwazi wakati alipoonyesha amewaona na akitaka kuwasogelea. Alidai kuwa baadhi ya ndugu, walimpiga marufuku asikanyage katika nyumba zao.

Hadi wakati tumepanga mstari kuomba kazi, Maganga alidai hakuweza kufanikiwa kupata mke na sababu kubwa zilikuwa mbili. Kwanza, alama ya uhaini lakini pili ni ukosefu wa kipato.

“Hata kama mwanamke atanikubali, atakula nini? Kwa wiki moja naweza kula mara tano hadi sita wakati kwa kawaida Mtanzania anakula walau milo 21 (mara tatu kwa siku). Sasa nikiwa na mke si itakuwa balaa?” alieleza huku akicheka.

Kitu kilichonivutia kuhusu Maganga ni ule uelewa wake wa mambo mbalimbali ya dunia hii. Kwa vile alisoma vizuri katika miaka ile ya 1970 na kuweza kuishi nchini Uingereza wakati wa mafunzo ya kijeshi, huyu hakuwa mwanajeshi wa kawaida ambao wengi tumezoea kuwaona mitaani.

Msimamo wake

Siku za uhai wake, Maganga amekuwa akilaumu tabia ya Watanzania kupenda kulalamika tu bila ya kuwa na maamuzi yatakayofanya watoke hapo walipo.

Yeye alikuwa anajiona miongoni mwa Watanzania walioamua kufanya jambo tofauti na wengi wao. Kwamba wakati wananchi wengi walikuwa wakilaumu tu hali ngumu ya uchumi iliyokuwa ikiikabili Tanzania miaka ile, wao walikuja na suluhisho; kubadili serikali.

“Inawezekana wengi hawakubaliani na kile tulichotaka kukifanya lakini walau tulifanya maamuzi. Mtu anaweza kufanya uamuzi mbaya au mzuri lakini ni afadhali huyo kuliko anayelalamika tu kila siku bila ya kufanya lolote. Hapa ndipo ninapotaka tubadilike,” alisema.

Mwaka 2004 aliamua kujitosa kwenye siasa akajiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Hii ilitokana na hofu kuwa asingeweza kukubalika ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Hivi nani ndani ya CCM angetaka kumpokea mtu aliyepanga kumuua Mwalimu Nyerere na kupindua serikali yake? Ndiyo maana nikaamua kwenda CHADEMA. Hata hivyo, naamini Watanzania bado wanaishi katika maisha magumu kuliko inavyotakiwa na upinzani unaweza kuleta mabadiliko,” alifafanua juu ya sababu za kujiunga na CHADEMA.

Mwaka 2005 aliwania ubunge kupitia CHADEMA katika Jimbo la Tabora Mjini ambako hata hivyo alishindwa na aliyekuwa mgombea wa CCM, Siraju Kaboyonga.

Akiwa CHADEMA alikuwa ofisa katika Kurugenzi Ulinzi na Usalama nafasi aliyoipoteza alipohamia CCM.

Jumatano, Januari 10, mwaka 2007, Maganga alitangaza kuhama CHADEMA na kuhamia CCM akidai kwamba hakuridhishwa na namna vyama vya upinzani vilivyokuwa vikiendeshwa.

“Kile nilichokitarajia, sicho nilichokutana nacho katika upinzani. Hakuna mfumo mzuri wala utaratibu. Kwa mwenendo huu, hatuwezi kufika kokote,” alilalamika.

Pengine Maganga alikuwa akitafuta fursa ya ‘kupendwa’ na wale aliodhani hawakuwa wakimpenda. Pengine alikuwa akitaka kutubu makosa yake na pengine, alidhani kwamba akihamia CCM mambo yake yatakuwa safi, haikuwa hivyo.

Hatua hiyo haikubadilisha maisha yake kwa namna yoyote. Hali yake ya maisha iliendelea kuwa ileile hadi mauti yanamkuta.

Historia

Maganga ambaye alikuwa na umri wa miaka 26 mwaka 1982 alishirikiana na wenzake wanane kutaka kuipindua serikali ya Mwalimu Julius Nyerere. Walikamatwa wakafunguliwa kesi ya uhaini.

Mwaka 1985 Maganga na wenzake saba; Suleiman Kamando, Zakaria Hans Pope, Vitalis Mapunda, Mbogolo, Kajaji Badru, Hatibu Gandhi (Hatty MacGhee) na Christopher Kadego walihukumiwa kufungwa maisha jela. Pius Lugangila alitoroka.

Maganga alikuwa na cheo cha kepteni ndani ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (TPDF) wakati mwenzake.

Mohamed Tamimu, waliyeshirikiana naye katika hatua za awali za maandalizi ya mapinduzi hayo, aliuawa na vyombo vya dola siku chache kabla ya siku ambayo walikuwa wamepanga kufanya mapinduzi hayo.

Maganga ameacha watoto wawili.

0
Your rating: None Average: 4.5 (2 votes)