Miaka 20 ya mapandikizi ya CCM


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 07 March 2012

Printer-friendly version

MAGEUZI yalipoanza na hatimaye mfumo wa vyama vingi kuruhusiwa rasmi nchini mwaka 1992, watu waliotamani kuwa viongozi lakini wakawa wanakosa nafasi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) walijiunga na vyama vya upinzani.

Kundi la watu wengine waliojiunga haraka na vyama vya upinzani ni wale waliotamani kuiondoa madarakani serikali ya CCM.

Vyama vya upinzani – NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF) vilivyokuwa na nguvu wakati ule, na hata United Democratic Party (UDP), Union for Multiparty Democracy (UMD) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) vilivuna wanachama wengi kwa mtindo huo.

Waliokata tamaa ndani ya CCM au waliofukuzwa kwa tuhuma mbalimbali walikimbilia upinzani, si kutokana na mapenzi yao ila kwamba wamepata fursa mbadala ya kupambana, kuikomoa na kuiondoa CCM. Mtindo huu unatumika hadi sasa.

Hapo, vibaraka na mapandikizi ya CCM wakawemo. Kwa hiyo, mshikamano wa wanachama katika vyama vya upinzani, mathalani mwaka 2010, haukutokana na na msingi wa itikadi na uzuri wa sera, bali furaha ya wana-CCM kukitia adabu chama chao kupitia upinzani.

Upinzani ukaanza kuwa na idadi kubwa ya wanachama na walipoandaa chaguzi za ndani, baadhi walishinda, wengine waliteuliwa au walipewa vyeo.

Augustine Lyatonga Mrema mfano mzuri. Alipojitoa CCM hujku akiutema uwaziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, alikaribishwa na “akapewa” uenyekiti NCCR.

Mfumo huo wa upokeaji wanachama ndio unavitesa vyama vya upinzani hadi leo kwamba kwa vile tamaa ya madaraka ndiyo kivutio cha wengi na kwa vile uchaguzi ndiyo mfumo unaokubalika kidemokrasia katika kupata viongozi, walioshinda wakapongezwa bila hata kujua wanachokisimamia.

Matatizo yaliingilia hapo. Kwamba japo uchaguzi ndio mfumo unaokubalika kidemokrasia kupata viongozi, si kila anayechaguliwa kwa wingi wa kura anaweza kuwa kiongozi bora.

Hii ndiyo sababu utasikia viongozi wa mikoa au wilaya; mwenyekiti au katibu wa chama cha upinzani anajiuzulu na kurudi kuwa mwanachama wa kawaida CCM.

Miaka ya nyuma, viongozi wa upinzani walioshawishiwa kujiondoa na kujiunga na CCM walikuwa wanapewa vyeo vya ukuu wa wilaya au mkoa au ubunge wa kuteuliwa.

Masumbuko Lamwai alijitoa NCCR akarudi CCM ambako aliteuliwa kuwa mbunge kisha akateuliwa kuwa mwanasheria wa chama. Mbunge wa Bunda kupitia NCCR, Steven Wassira alirejea CCM na akapigiwa debe kuwa mbunge na sasa ni waziri.

Dk. Amani Walid Kabourou aliyeitetemesha CCM pale alipokuwa katibu mkuu wa CHADEMA na mbunge wa Kigoma mjini, alisalimu amri na kuja kujiunga CCM baadaye. Punde akapata ubunge wa Afrika Mashariki.

Danhi Makanga aliyeitesa CCM alipokuwa Mbunge wa Bariadi Magharibi kupitia UDP sasa ni mkuu wa wilaya ya Kasulu.

Wanasiasa hao ni mfano wa viongozi walioko upinzani ambao mapenzi yao yako CCM. Kwa hiyo haishangazi kusikia mtu anaachia nafasi ya uongozi katika upinzani ili aweke matumaini ya kupigiwa debe awe kiongozi au mbunge wa CCM.

Miaka 20 tangu mfumo wa vyama vingi uanzishwe kisheria, bado vyama vya upinzani havijafanikiwa kubaini na kutegua mtego wa vibaraka, wanafiki, ndumilakuwili au mapandikizi ya CCM.

Hata wanachama wa upinzani ambao ni mapandikizi ya CCM huamua kujaza vibaya fomu za kuomba kuteuliwa kuwania ubunge, na wengine hujiondoa wakati muda wa kuteua wagombea ukiwa umekwisha. Kwa mtindo huu, wanachama hufa moyo na kudhani wapinzani wote ni wababaishaji.

Na huu ni uthibitisho kwamba hata kama walishinda kupitia uchaguzi, mfumo unaokubalika kidemokrasia katika kupata viongozi, si kila anayechaguliwa kwa wingi wa kura anaweza kuwa kiongozi bora.

Baadhi ya watu hawana silka ya uongozi kwamba hata kama wamesoma, hawana uwezo wa kutatua migogoro, wana jazba, hasira, si wavumilivu na hawana subira. Jiulize, mtu anawezaje kuhama CCM akajiunga NCCR kisha akaenda TLP, CUF, CHADEMA, akaanzisha chama chake akaua na akaamua kurudi tena CCM?

Mtu anawezaje kuwa kiongozi wa upinzani lakini wakati wa kampeni akamtosa mgombea urais kupitia chama chake akamuunga wa CCM?

Kiongozi makini wa upinzani anawezaje kupanda katika majukwaa kwa lengo la kuponda chama kingine makini cha upinzani?

Nasisitiza, si kila anayechaguliwa kwa wingi wa kura anaweza kuwa kiongozi bora. Baadhi ya watu, kwa sababu tu ya kuwa wasemaji sana vijiweni, waropokaji mikutanoni, au wachekeshaji katika hafla, huweza kushawishi watu wakawachagua kuwa viongozi mahala fulani.

Vilevile, baadhi ya watu, kutokana na ukwasi, huweza kugharimia wapigakura na wakaibuka washindi. Mtu yeyote, atakayeshinda kura kwa vile ni mcheshi au amehonga mfumo wa uchaguzi, hawezi kuwa kiongozi bora.

Matokeo yake yanaonekana hadi sasa. Waliojiunga na upinzani kwa lengo la kutafuta umaarufu tu, wengi wao sasa wanajitoa. Wenyeviti, makatibu na waliopata kushika nafasi mbalimbali nyeti kwenye vyama vya upinzani wanajiuzulu na kurudi CCM kuwa wanachama wa kawaida.

Waliojiunga na upinzani kwa tamaa na papara kwamba uchaguzi huu chama chao kinaweza kutwaa dola, pale kinaposhindwa, viongozi hawa hukosa uvumilivu na hujilengesha CCM.

Kiongozi anawezaje kuacha mshahara (hata kama ni mdogo), posho na hadhi ya kuwa mwenyekiti wa chama na kuamua kuwa mwanachama tu? Jiulize, mwenyekiti wa mkoa wa CUF au CHADEMA au NCCR-Mageuzi au TLP anawezaje kuachia ngazi ili awe mwanachama tu wa CCM?

Kwa viongozi hawa uenyekiti katika upinzani una hadhi sawa na ile ya mwanachama wa kawaida katika CCM. Hawa ni kundi la wachekeshaji na mapandikizi.

Kipindi hiki ambacho vyama vya upinzani vinahaha kupata wanachama katika maeneo yote nchini kuanzia mkoani hadi vijijini, ni rahisi kukumbatia mapandikizi ya CCM.

Aidha, ni rahisi wachekeshaji, waropokaji na wengine wasio na maadili ya uongozi kuchaguliwa. Hawa ndio hukorofishana sana na wanachama ambapo njia rahisi, kwa baadhi yao huwa ni kurudisha kadi na kujiunga na CCM, si kwa mapenzi bali kwa vile hana pa kwenda.

Kundi jingine la watu wanaotibua utulivu katika vyama vya upinzani ni waliokimbilia nafasi za uongozi kwa uroho wakati hawana uwezo. Wanachotaka ni ufahari wa kuwa kiongozi, lakini anaposhindwa haraka huwatupia lawama wengine na baadaye hujiuzulu na kurudi CCM.

Kuwa katika vyama vya upinzani si lelemama, ni kuwa kwenye mapambano ya kudai haki wakati wote. CCM haitaki vyama vinavyotembelea wanachama wao wakati wote; inataka vyama vilale ndiyo maana hata wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2010, Rais Jakaya Kikwete alidai vyama vya upinzani ni vya msimu wa uchaguzi tu.

0789 383 979
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: