Miaka 20 ya uporaji, mateso Loliondo


Paul Leitura's picture

Na Paul Leitura - Imechapwa 30 March 2011

Printer-friendly version

KWA karibu miaka 20 sasa, wananchi wakazi wa Loliondo wamekuwa wakiwindwa kama wahalifu.

Wamekuwa wakifukuzwa hapa na pale. Wamechomewa nyumba na maboma. Wameumizwa kwa risasi za moto kutoka bunduki za askari wa FFU.

Kisa? Waondoke kwenye makazi yao ya miaka yote ili kampuni ya uwindaji kutoka nchi za kiarabu, Oterllo Business Corporation (OBC), ijitanue kibiashara katika eneo lao.

Miaka miwili iliyopita, askari wa FFU, wakiwa na silaha, waliingia katika vijiji vya Ololosokwan, Soitsambu, Arash na Lorien Magaiduru na kuchoma nyumba na maboma ya mifugo; kutishia wananchi kwa bunduki na kuwaamuru waondoke kwao.

Historia ndiyo shahidi mkuu katika hali na mazingira haya ambamo, watawala wakishirikiana na mwekezaji, wamefanya mnyama kuwa na thamani kuliko binadamu.

OBC ilingia Loliondo mwaka 1992 baada ya kupewa leseni ya uwindaji. Mkataba ulisainiwa na serikali chini ya uongozi wa rais wa pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi.

Mkataba ulisainiwa tarehe 20/11/1992; bila kushirikisha, kwa namna yoyote ile, wanavijiji au viongozi wao.

Taarifa zilizopo zinaonyesha mkataba ulisainiwa na mbunge wa wakati huo, Richard Koilah (marehemu), mkuu wa wilaya wakati huo, Luteni mstaafu Laban Makunenge, kwa niaba ya serikali kuu na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya.

Ni wazi basi kwamba mkataba huo ulisainiwa kinyume cha sheria ya ardhi ya mwaka
1923.

Kimsingi, kampuni ilipaswa kuingia mkataba na vijiji sita ambavyo ndio wamiliki halali wa ardhi hiyo. Vijiji hivyo ni Soitsambu, Arash, Ololosokwan, Olorien, Oloipiri na Oloosoito; lakini haikufanya hivyo. Serikali haikufanya hivyo pia.

Tangu wakati huo, wananchi wamekuwa wakipinga kuingiliwa katika ardhi yao;

kubughudhiwa, kutishiwa na kutendewa unyama wa kila aina ikiwa ni pamoja na kuchomewa nyumba na mifugo yao kusambaa na mingine kupotea.

Kampuni hii, tangu kuanza shughuli zake eneo la Loliondo mwaka 1992 hadi 2004, iliongozwa na Bw. Ahmed Seed Abdulrahaman Alkhateeb, ambaye ni raia wa Kenya.

Huyu alijitahidi kuimarisha uhusiano mzuri na wadau mbalimbali; kwa mfano kati ya vijiji na kampuni; serikali na vijiji na kampuni na serikali.

Mwaka 2004 hadi 2007 kampuni iliongozwa na Juma Akida (marehemu), ambaye naye alijitahidi kuendeleza mahusiano yaliyokuwepo baina ya wadau.

Bali Akida naye alikuja kugeuka. Akaanza kutoshirikisha jamii katika shughuli zinazoendelea katika maeneo yao; akaibua migogoro isiyoisha na kuondoa wananchi kwenye hoja kuu ya kupigania ardhi yao iliyoporwa.

Kuanzia mwaka 2007 hadi sasa, kampuni hii inaongozwa na Bw. Isaack Mollel ambaye chini ya uongozi wake, mahusiano yaliyokuwepo yamezorota na hatimaye kuisha kabisa.

Mkurugenzi huyu sio tu kwamba hajajenga; bali pia ameharibu hata mahusiano yale yaliyokuwepo awali chini ya waliomtangulia.

Ni chini ya uongozi wa Mollel ambapo makazi ya wafugaji yalichomwa moto mwaka 2009; mali nyingi za wakulima ziliteketezwa, mifugo kufa, vyakula kuteketea na mateso mengi na makubwa kuwakumba wananchi Loliondo.

Yote haya yalifanyika kupitia operesheni ya FFU inayodaiwa kugharimiwa na OBC.  Juu ya adha hizi, Mollel akaja na mbinu nyingine na yenye lengo la kupora ardhi ya vijiji kwa kufadhili kile kinachoitwa “Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi ya
Wilaya.”

Kwa mujibu wa ripoti ya ardhi ya mkoa wa Manyara ya 2009, mpango huo wa kupokonya ardhi ya wakazi na wafugaji uligharimu jumla ya Sh. 157 millioni.

Cha kushangaza, kwa mujibu wa taarifa hiyo, ni kwamba fedha hizo zilitolewa na OBC – adui mkubwa wa fursa na maendeleo ya wafugaji Loliondo.

Haishangazi basi, kwamba matokeo ya mpango ulioandaliwa kwa kutumua fedha za anayejiita “mwekezaji,” yamekuwa kupora zaidi eneo la wale ambao wamekuwa wakibughudhiwa – wakazi halali wa Loliondo.

Aidha, kinachoitwa mpango wa matumizi bora ya ardhi unaopigiwa chapuo, kilifanyika bila kushirikisha wananchi ambao ndio wenye ardhi na hivyo hakina baraka zao.

Mpango huo, hata hivyo, umekiuka sheria ya ardhi ya vijiji ya 1999 na sheria ya matumizi bora ya ardhi ya mwaka 2007 zinazoelekeza ushirikishwaji wananchi katika kuandaa na kutekeleza mpango wa aina hii.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, mkutano mkuu wa kijiji ndio wamiliki wakuu wa ardhi yote ya kijiji huku halmashauri ya wilaya ikiwa na uwezo wa kushauri tu; na hii ni kama kijiji kitahitaji ushauri wake.

Mpango huu una hitilafu nyingi. Unaingiza ushoroba – mapitio na mazalia ya wanyama – suala ambalo linaendelea kupunguza ardhi ya kijiji.

Unaonyesha eneo lote la tarafa ya Loliondo kuwa limetengwa kama “game controlled area” na kuacha eneo dogo sana kwa ajili ya makazi ya watu. Hakuna hata eneo dogo la kilimo.

Katika tarafa ya Sale, eneo lake kubwa limetengwa kama “Wildlife management area” – eneo la menejimenti ya wanyamapori.

Kwa hiyo, kinachoitwa mpango wa matumizi bora ya ardhi, licha ya kutofuata sheria, hakikuzingatia kabisa mfumo wa maisha ya wananchi katika eneo hili – wafugaji wanaohitaji nafasi kubwa ya kutandawaa na mifugo yao.

Hii ina maana kuwa mpango huo ni batili na haramu, kwani asilimia 95 ya wakazi wa tarafa za Sale na Loliondo ni wafugaji ambao sasa wamenyag’anywa maeneo ya kuishi na maeneo ya kuendeshea ufugaji.

Kwa msingi huo, mpango huu unakuza mgogoro uliopo. Huu ndio mwanzo hasa wa maisha magumu na ukaribishaji umasikini wa kiwango cha juu kwa wananchi wa Loliondo.

Wakazi wa Sale na Loliondo wanahitaji kubaki na maeneo yao na mifugo yao. Ng’ombe na maeneo ya kuchungia, ni  sehemu muhimu katika maisha ya kila siku ya mfugaji.

Ili kuondokana na migogoro; na kwa shabaha ya kuendeleza ustawi wa wananchi; ardhi ya Sale na Loliondo inabidi ibaki kama ilivyokuwa kwa matumizi ya vijiji vyenyewe.

Hivyo ndivyo wananchi wanavyotaka. Ndivyo viongozi wao wa kweli wanavyotamani. Ndivyo haki inavyotaka.

Unyang’anyi wa aina yoyote ile, kwa njia ya “mpango” au kanuni – vinavyotokana na kazi iliyogharimiwa na mporaji – hauwezi kupata baraka za wananchi.

0
Your rating: None Average: 5 (2 votes)