Miaka 40 ya 'kupanga ni kuchagua'


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 09 June 2009

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

TUNAOGOPA kuangalia nyuma. Hatupendi kukumbuka au kukumbushwa. Tumekuwa kama mtu mlevi ambaye akiamka asubuhi na kumbukumbu ya usiku uliopita inamjia, anajikuta hataki kukubaliana na ukweli wa usiku uliopita.

Naomba leo niwe mkumbushaji. Nikumbushe historia ambayo wazee kama mimi wanaifahamu vizuri na vijana wetu wengine hawajawahi hata kuisikia japo mtu akiamua kwenda maktaba ataipata kwa urahisi.

Nikumbushe juu ya kilichotokea miaka 40 iliyopita na kilishuhudiwa hadharani na leo hii, japo kilikuwa ni kikubwa mno. Sijamsikia hata mwana-CCM mmoja (wengine walikuwepo pale), ambaye amekumbuka kuwa kilitokea na umuhimu wake katika historia ya Taifa na hasa juu ya mwelekeo wa taifa letu katika karne hii mpya.

Ilikuwa tarehe 28 Mei 1969 katika Mkutano Mkuu wa TANU Jijini Dar es Salaam ambapo Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano ulijadiliwa na kupitishwa kufuatia mpango wa kwanza wa 1964. Hilo lilifanyika kabla ya mpango huo hatimaye kupitishwa na Bunge.

Baba wa Taifa alitoa hotuba kwenye mkutano huo ambayo inajulikana kama “Kupanga ni kuchagua.” Hotuba hii ninaamini, kama ningekuwa na uwezo, ningehakikisha mawaziri wote na manaibu wao, kabla hawajaanza kazi zao, wanaisoma na kuelewa ujumbe uliomo ndani yake.

Msingi wa hotuba yake ile ilikuwa ni kufafanua kwa wajumbe wa mkutano wa TANU juu ya hali ya taifa ilipo na wapi taifa linataka kwenda.

Kiongozi mzuri ni yule ambaye haogopi kuangalia historia yake jinsi anavyoongoza na hata baada ya kutoka madarakani.

Pia alifanya hilohilo miezi michache kabla katika hotuba yake ya Uhuru ambapo alitoa ile hotuba maarufu ya “Tujisahihishe.”

Siyo Mwinyi, Mkapa wala Kikwete leo hii ambao wameweza kuangalia uongozi wao na kusema tumefanya makosa na tubadilike. Nyerere bado anabakia kuwa mfano.

Lengo la Mwalimu lilikuwa kutoa mwelekezo mpya wa kitaifa wa wapi nchi inataka kwenda baada ya kupima na kusahihisha makosa ya mpango wa kwanza wa miaka mitano wa 1964.

Kwa mfano akiangalia mpango ule wa kwanza, Nyerere kwa kujiamini alikiri makosa ambayo yalitokea ambayo aliamini yalisababisha baadhi ya malengo kutofikiwa. Alikiri tatizo la mabadiliko yaliyo nje ya uwezo wa serikali na tatizo la kutokuwa na takwimu za kutosha na sahihi.

Nyerere hata hivyo, anakiri kuwa haiwezekani serikali kumridhisha kila mtu hata kama ingependa; na kwa hakika haiwezi kutumia raslimali zake zote kwa wakati mmoja kushughulikia mambo yote.

Kwa maneno ya Mwalimu, “Kwa kiasi fulani, kila nchi duniani ina kiasi fulani cha raslimali zake na hivyo inapotumia kiasi kwenye jambo moja ina maana haitumii kiasi fulani kwenye jambo jingine.”

Hivyo basi, naweza kusema kuwa ukiisoma vizuri hotuba ile utaona kuwa alichokuwa anakisema Nyerere miaka 40 iliyopita ni kuwa, kama taifa, lazima tuwe na vipaumbele.

Bajeti mpya inakuja na sitoshangaa iwapo itakuwa ni bajeti ya kujaribu kufanya mambo yote kwa wakati mmoja; bajeti ambayo itajaribu kuridhisha makundi mbalimbali, na kwa vile tunaelekea uchaguzi mkuu mwakani, inaweza kuwa bajeti ya kisiasa zaidi kuliko bajeti yenye kipaumbele kwa taifa.

Lakini tatizo jingine ambalo inaonekana watawala wetu bado hawajifunza kutoka kwenye hotuba ile ya “Kupanga ni Kuchagua,” ni kuishi kwa kutoa visingizio vya matatizo yetu badala ya kuyaita kwa jina lake.

Leo hii ulimwengu unakabiriwa na hali mbaya ya kiuchumi. Matatizo ambayo watawala wetu nao watayadandia na kudai kuwa na sisi tuna matatizo kama hayo ya nchi za Magharibi kiasi kwamba wanataka “stimulus package” ili kuchochea uchumi wetu.

Tena wanataka kutoa mapendekezo kama yale ya nchi kubwa zilizoendelea ambazo sekta yao kubwa ya fedha ndiyo imeathirika sana. Hivyo, na sisi kama kasuku, tunataka kujaza mabilioni ya fedha kwenye mabenki yetu. Huku ni kutokuelewa kupanga ni kuchagua.

Ukweli hata hivyo ni kuwa watawala waliacha zamani kulijenga taifa. Wanataka tuamini kuwa Tanzania ni taifa lililojengwa tayari na linafurahia mambo yaleyale kama ya nchi za Magharibi.

Ni kwa sababu hiyo mimi si muamini wa mpango wa kujaza mapesa kwenye mabenki na kuja na haya ya “stimulus package” yanayofanywa na Marekani.

Mimi ni muamini wa nadharia kuwa kuna haja ya kupanga na kuchagua vizuri, nini tukifanye kama taifa wakati huu ambapo bei ya vitu inashuka na mikataba mizuri zaidi na yenye manufaa kwa taifa inaweza kuingiwa.

Badala ya haya ya kuandaa mpango wa kuchochea uchumi kama wanavyofanya Wamarekani, Wajerumaini na wengine, kwanini sisi tusifanye kitu ambacho tunajua kinahitajika? Kwanini tusifikiri nje ya sanduku la wazungu na kupanga kile tunachofahamu ndicho tunahitaji?

Hoja yangu ni kuwa turudi kwenye “kulijenga taifa”. Yaani, tukae chini kama taifa na kupima tulikotoka, tujue ni wapi tumefanya makosa, na kutoka hapo tuchonge njia yetu upya ya wapi tunataka kwenda na jinsi gani tutafika huko.

Badala ya kuharakisha haya ya “stimulus package” kwanini tusiandae “Nation Building Package” – mpango wa “ujenzi mpya wa taifa?”

Hadi hivi sasa sijaona ushahidi wowote ambao unaweza kuelezea matatizo yetu ya uchumi kuwa yametokana na matatizo haya ya nchi za Magharibi.

Kwa mtu yeyote anayefuatilia siasa za ndani anajua kabisa kuwa matatizo yetu ya kiuchumi, kwanza kabisa yamesababishwa na sera mbovu na siasa mbovu za CCM. 

Ni sera mbovu na siasa mbovu kwa sababu hazigusi matatizo hasa ya nchi yetu na badala yake zinalenga kutibu dalili tu za matatizo hayo.

Pendekezo langu ni kuwa badala ya kukumbatia dhana ya fedha za kichocheo cha uchumi, tufikirie mpango mpya wa maendeleo ambao utalenga katika ujenzi mpya wa taifa la kisasa.

Kwani pale tulipoacha kama nilivyosema, karibu mwaka mmoja uliopita, ndipo pale tulipoanza kulibomoa taifa na kujenga majengo.

Tunahitaji kurudi kwenye misingi ya “kupanga ni kuchagua” iliyotolewa na Baba wa Taifa miaka 40 iliyopita. Vinginevyo tutaendelea kuburuzana tu.

0
No votes yet