Miaka 50 Oyee: Tutaimbaje wimbo huu?


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 19 October 2011

Printer-friendly version
Uchambuzi

MIAKA 50, Oyeee!

Ni mingi
Ni nusu karne
Wengi wamezaliwa
Wengi wamekufa;
Lakini taifa bado;
Bado laitwa changa
Na mbele twasonga.

Shule zimeongezeka
Vyuo vimemea
Walimu wamechongwa
Hata wa wiki mbili
Wanafunzi wamesoma
Hata waliokosa –
Memkwa hao waitwa;
Oyeee! Miaka 50.

Usichanganye mambo
Ukweli na hizo tambo
Usichanganye hisia
Hata huo ushabiki
Usiingize dharau
Hata chuki binafsi
Kipo kilotendeka;
Miaka 50, Oyeee!

Kama hukwenda mbele
Basi umerudi nyuma
Kama hukufurahi
Basi umenuna
Kama hukukua
Utakuwa umedumaa
Miaka 50 ni hii
Nawe itika, Oyeee!

Kila mmoja alipo
Asifu au asute
Kila mmoja aone
Jema hata lilobaya
Kila mmoja aseme
Jichole laona nini
Kila mtima uujue
Miaka 50, Oyeee!

Ukitaja yaloota tu
Wenzi watakusuta
Yapo hayakumea
Hewa yamekinzanwa
Wapo walotoka kapa
Shuleni na biashara
Jino wauma sana
Bali waitika Oyeee!

Tarakimu zadanganya
Bali mtindo wa usomi
Kuhesabu na kuhesabu
Wingi ndo mafanikio
Hata kama hujala
Wakinena usigune
Mkumbo siyo muhali
Itikia tu Oyeee!

Itikia Oyeee
Usitake kukemewa
Hata kama huyaoni
Yaletayo majigambo
Ndweo za watawalao
Nazo pongeza kikiri
Ni mtindo, ni kisasa
Miaka 50, Oyeee!

Kibarua hukioni
Wewe itika, Oyeee!

Matibabu huyagusi
Hata roho ikatike
Wanao shule kukwama
Wa wenzi Ulayani
Kubali wimbo uimbe
Miaka 50, Oyeee!

Miaka 50, Oyeee!

Liko wapi trekta letu
La kuinua migongo?

Liko wapi gari letu
Kutukimbiza twendako?

Iko wapi hospitali
Kutibu yasotibika
Tukaimba na kusifu.

Iko wapi misitu yetu
Utajiri tulorithishwa
Iko wapi dhahabu yetu
Almasi, Tanzanite
Na madini mengimengi
Ziko wapi mbuga zetu
Urithi uliotukuka:
Leo, miaka 50!

Tunalia na mbu
Wazungu wachota
Wacheka, wahama
Na madini na mbao.

Tunalia na njaa
Miaka 50
Ardhi wamega wakuja
Bali tuimbe, Oyeee!

Ujasiriamali!

Wimbo usio mabeti
Siasa za njiapanda
Vijana kukamatia
Asolima mvivu, mlevi
Kwa meno
Ardhi akakatue
Leo aimbe, Oyeee!

Biashara ushindani
Hata wewe ufanye:
Wito wa walasiasa
Mjerumani, Mhindi
Mchina na Mwingereza
Ukishindwa tokomea
Hizo ni fursa sawa
Bali leo uimbe, Oyeee!

Machinga analia
Ashindane na nani
Alikofukuzwa
Kachukua Mchina
Na wengi wenzake
Bidhaa ni chupi
Vichokonoa meno
Pamoja tuimbe, Oyeee!

Njiti za mdomoni
Miaka 50 ya uhuru
Bado nje zatoka
Kwa marafiki wa China
Pilipili na maepo
Cape Town nyumbani
Twala na kujigamba
Na kuimba, Oyeee!

Kelele ni nyingi leo
Kutukusanya kuimba
Lipalamba na Mitomoni
Viongozi hawajafika
Tangu uhuru kuumbwa
Wasichana wa Korogwe
Kama njugu wauzwa
Nasi tuimbe, Oyeee!

Tusipuuze kuimba
Labda mwanzo ndo huu
Kuimba kwaleta faraja
Mitima kutokunjamana
Tukisubiri kuche
Kusikokucha tufungue
Tufanyenye – leo au kesho?

Twendelee kuimba, Oyeee!

Kuna mambo twayaona
Vyovyote yangefanyika
Kuna mambo hayaitwi
Kwetu yaja kiana
Kuna yajayo kwa jasho
Yale yainuayo taifa
Yale tuimbe, tusifu
Kwa 50, Oyeee!

Kwa wizi na ulozi
Hatuimbi haslani
Ukwapuaji mabilioni
Ya shilingi kodi zetu
Taifa kunyong’onyeza
Hatuafiki hakika
Kama kusindikiza,
Basi tuseme tu, Oyeee!

Wanoiba wanajua
Pembeni wanatucheka
Walowasaidia hawa
Wanachekea kiganjani
Sote eti kalagabao
Kaseme ulile konzi
Hata hili la kuimba
Oyeee, sasa ni soo!

Koo zao zimepanuka
Wanameza kama mioto
Vifua vimetanuka
Wanavaa mita kumi
Wanatembea kwa shida
Hawali wakafurahi
Wanatupumulia sisi
Tuimbe, 50 Oyeee!

Hapa 50, pale 50
Kila wizara 50
Kila mkoa 50
Kila wilaya 50
Kila chuo 50
Hamsini na hamsini
Kila kukicha hamsini
Eti tuimbe, Oyeee!

Ninatamani kuimba
Oyeee! ya kweli moyoni
Mwongozaji havutii
Hata ukweli hapendi
Namwona mwigizaji
Atafuta kifuta machozi
Kapule kujalizia
Nasi tumwimbia, Oyeee!

Basi iwe ya kweli
Ile 50 ijayo
Viwanda viteme bidhaa
Tuonyeshe kujitawala,
Elimu na biashara
Vionyeshe uhuru wetu
Nasi tuweze kuimba
Miaka 50, Oyeee!

Tukishika kijiko
“Madeni” ya Tanzania
Tukishika jembe
Madeni ya Tanzania
Tukishika trekta
Madeni ya Tanzania
Hata sindano na njiti
Ndipo tuimbe, Oyeee!

Tukiiita kandarasi
Awe mwana wa jirani
Hawa wachimba madini
Wawe hao wanawetu
Mikataba ilo wazi
Uwe wetu utamaduni
Ndipo tutaimba sote,
Miaka 50, Oyeee!

Katika zetu tawala
Tukiongozwa na katiba
Lile tunda la jamii
Lielezalo mipaka
Kila mmoja kuthamini
Haki tupu kuzingatia
Pamoja tuje kuimba
Miaka 50, Oyeee!

Katika uandishi wetu
Ukweli kuzingatia
Kukataa minyororo
Ile ya hongo shingoni
Kukana utumwa wa fedha
Za wezi na mafisadi
Ndipo tushiriki kikweli
Kuimba 50, Oyeee!

0713 614872, ndimara@yahoo.com, www.ndimara.blogspot.com
0
Your rating: None Average: 3 (1 vote)