MIAKA 50: Serikali wanasherehekea, wananchi wanalia


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 21 September 2011

Printer-friendly version

TAIFA, kwa maana iliyotafsiriwa katika kamusi ya Oxford toleo la pili ni jamii ya watu wanaoishi katika nchi moja na wanaounganika kutokana na matukio ya kihistoria, mfumo wa uchumi na utamaduni chini ya serikali moja!

Kwa tafsiri hii Tanganyika, kama taifa, ilizaliwa mwaka 1961 na kukoma mwaka 1964 lilipozaliwa taifa la Tanzania. Tanganyika haikupata bahati ya kutimiza miaka 50. Lakini Tanzania, kama taifa, panapo majawaliwa itatimiza miaka 50 mwaka 2014.

Nchi kama ilivyotafsiriwa katika kamusi ya Oxford toleo la pili ni ‘sehemu ya ardhi katika ulimwengu iliyogawanyika kisiasa kwa mipaka na kutambulika kwa taifa lake’. Kwa tafsiri hii, Tanzania kama nchi, ilizaliwa mwaka 1964 pale nchi ya Tanganyika na nchi ya Zanzibar zilipoungana na kuwa nchi moja. Tanzania sasa ina umri wa miaka 47.

Tukizingatia tafsiri hizi lazima tujiulize tunasherehekea miaka 50 ya nchi ipi au taifa lipi? Tumejichanganya. Tumechanganywa. Tumechanganyikiwa. Au tuko katika hali zote tatu?

Mabilioni ya shilingi kutoka katika kodi iliyokusanywa kutoka kwa wananchi yametengwa kwa ajili ya wateule kula, kunywa na kufanya starehe za kila aina hata za kukufuru. Wanasema wanasherehekea miaka 50.

Kufuja mabilioni ya fedha kwa ajili ya kula na kunywa kwa kitu kisichojulikana vizuri huku tukielewa fika hali ngumu sana ya maisha ya watu wetu, ni sawa na kumkufuru Mwenyezi Mungu.

Watoto wa maskini shuleni wanakaa chini kwenye mavumbi. Shule ya Msingi Mhugu iliyoko mkoani Iringa watoto wanasomea nje; jua linapokuwa kali zaidi hulazimika kujificha katika vivuli vya vichaka. Hawa wana uhuru gani wa kuufanyia sherehe!

Tunaambiwa uchumi wa nchi umeshuka kutokana na tatizo kubwa la uhaba wa umeme, badala ya kuelekeza nguvu kutatua tatizo hili tunataka kushereheka. Kama siyo ulevi ni nini?

Mama zetu na dada zetu wanaendelea kufa kwa kukosa huduma wakati wa kujifungua. Zahanati na hospitali zimekuwa sawa na machinjioni kwa kukosa dawa na vifaa. Wafanyakazi wamenyong’onyea kwa malipo duni na hakuna anayeonesha kuwajali. ‘Mabosi’ wao wako ‘bize’ kujiundia vijisafari na mikutano ya uongo na kweli ili kuziba wanachodhani ni mapengo katika mifuko yao.

Wakati nchi inaelekea kusimama, huku bei za bidhaa zikipaa na kufanya hali ngumu ya maisha kuwa ngumu zaidi, unawaita viongozi wa mataifa mbalimbali kutoka kwao kwenye neema, waje kutanua kwa kufuja mabilioni ya fedha ambayo kwa kiasi fulani yangetumika kuwapunguzia wananchi ukali wa maisha. Timamu hawasherekei umri wa ndoa yao yenye matatizo lukuki.

Wakati watoto wa maskini wakinyimwa hata mikopo kwa ajili ya elimu yao ya juu, baadhi ya watoto wa viongozi wanahemea kwa juu. Wamezama katika dimbwi la tuhuma nzito za utajiri wa kukufuru. Wamepora kuanzia ardhi hadi mashirika ya umma yaliyokuwa yamebakia. Wanajikusanyia chochote hata vyeo katika ofisi za umma.

Vijana wako wengi ambao au kwa jasho la damu yao na ya wazazi wao au kwa mikopo hii nyanyasika wamepata digrii zao na sasa wanatembea nazo barabarani kwa kuwa ajira zipo lakini kwao hamna.

Injinia aliyejiajiri mwenyewe na kuajiri wengine inapotokea ajira ya viti maalum anaajiriwa yeye. Kufuru inakuja pale ambapo hata ikitokea ajira nyingine kama ya ukuu wa mkoa anaajiriwa  yeye. Ajira kwa ajiri ya hawa ambao au wazazi wao hawana majina au hawajahusishwa katika kuficha ufisadi wa wakubwa zitakuja kupatikana vipi?

Jumatatu, nikiwa mtaa wa Ohio, nilikutana na kundi kubwa la mgambo wa ‘site’ huku kila mmoja akiwa amejisheheni mizigo waliyopora kwa wamachinga. Walitembea kwa nguvu huku wakiwa na nyuso za furaha kama wanazokuwa  nazo wawindaji wakishapata mawindo yao .

Wamachinga wenye mali zao sikuwaona. Kunyang’anya mali ya mtu kwa nguvu ni kupora. Ni serikali ya kidhalimu peke yake duniani inayoweza kuhalalisha uporaji wa kinyama kama huu dhidi ya raia wake wema ambao hawataki kujihusisha katika uhalifu kama wizi bali wanataka kupata riziki zao kwa kufanya kazi halali..

Serikali imeshindwa kuwapatia hawa vijana ajira. Ili waione kesho yao wanajitafutia ajira ambazo si haramu. Serikali hiyo hiyo inageuka jambazi na kuwapora vijana wake wenyewe. Inataka hawa waishije?

Wanachofanya mgambo wa site ni ujambazi sawa na ujambazi mwingine. Wanaweza wakasherehekea miaka 50 ya ujambazi huo, hawa wanaoporwa wanafurahiaje miaka 50?

Mwenyezi Mungu aliwapa wanawema wa nchi hii, nchi tajiri mfano wake duniani hakuna. Aliwajazia madini ya thamani kubwa katika ardhi yake na juu yake akajaza milima ya kuvutia, mito inayotiririsha maji yaliyojaa viumbe wa kila aina waishio majini, misitu ya kijani iotayo mimea yote, mbuga za wanyama na wanyama wa aina zote wengine duniani kote hakuna.

Baadhi ya viongozi walafi wamewakaribisha wageni wezi nao kwa pamoja wamekuwa wakipora raslimali za nchi hii kwa miaka 50. Sasa wanasherehekea! “Mawe!” tunalia, tutasikiwa na nani?

 Nayakumbuka maandiko katika vitabu vitakatifu. Alikuwapo mwanamke akiitwa Raheli mkazi wa Ramal. Aliporwa watoto wake wote na majahili kama hawa, wakapelekwa nchi ya mbali kama twiga na wanyama wengine na ndege wetu walivyopelekwa nchi za mbali.

Alijiwa na fahamu kuwa maombi ya mwenye haki Mungu huwa anasikia. Akaenda akamlilia Mungu wake. Ndipo Bwana akamjibu akasema, “Zuia sauti yako. Usilie ee Raheli. Nimesikia sauti yako. Watoto wako wote sasa wanakuja tena wanarudi”.

Ndugu zetu wamachinga, wapondakokoto, wakulima wanuka jasho, walionyimwa elimu ya juu na wanaosomea mavumbini, Mwenyezi Mungu bado anawapenda. Unganeni, unganisheni sauti zenu, lieni, pazeni sauti zenu, ombolezeni kwa siri kwa maana Mungu wetu anasikia. Wapandao kwa machozi watavuna kwa shangwe!

Jipangane katika safu, lieni  mkisema nchi yetu kwanza. Mwenye kukaa ikulu ndiye baba yenu, naye ni mwema. Msililie vichochoroni, mlilieni naye atawasikia katika miaka hii 50 ya machungu yenu.

0713334239, ngowe2006@yahoo.com
0
No votes yet