Midahalo ya wazi itaiumbua CCM


Nkwazi Mhango's picture

Na Nkwazi Mhango - Imechapwa 15 September 2010

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi

INGAWA midahalo baina ya wagombea ni jambo jema, kwa wengine, hasa wasio na kitu cha kuonyesha wapiga kura, ni jambo la hatari.

Kupitia midahalo, chama hata mgombea huweza kuwashawishi wapigakura kwa kujibu maswali yao makuu. Kupitia midahalo, mipango, vipaji, sera, historia, weledi, uoza na hata umahiri wa wagombea na vyama vyao, huwekwa wazi mbele ya wapiga kura.

Kwa mgombea au chama ambalo kiliishachafuka au kutopea kwenye shutuma lukuki, tena za kutisha na kuchusha, midahalo ni sawa na moto, huku wao wakiwa wamejipaka petroli.

Kwa kutambua hatari na hali hii, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimewapiga marufuku wagombea wao kushiriki midahalo.

Hata hivyo, hii ni dhuluma na hujuma kwa demokrasia. Kwani kufanya hivyo ni kujiangalia binafsi na kuupuuzia umma ambao chama hicho kinadai kuupigania na kutaka kuuongoza.

Midahalo haijaanzia Tanzania. Hata nchi zinazotufadhili hutumia midahalo kuonyesha kufaa au kutofaa kwa wagombea wa nafasi za uongozi.

Hivyo kutoshiriki ni sawa na kuturejesha kwenye zama za kiza za chama kimoja. Ni aina fulani ya ubabaishaji na kushindwa kwa wazi.

Zuio hili lilianza baada ya mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete kuonyesha wazi kukacha midahalo kwa sababu anazozijua mwenyewe na chama chake.

Wengi hawakushangaa hili kutokana na kujua hali ambayo CCM na mgombea wake wanakabiliana nayo katika uchaguzi huu. Wameamua kufunika kombe mwanaharamu apite.

Hata hivyo tukirejea historia ya ugombea wa Kikwete, hatutashangaa kukacha midahalo hadi sasa kuingiza hata wagombea wengine wa chama chake.

Alianza mchezo huu mwaka 2005 alipopitishwa kwa kishindo na ushabiki baada ya wengi waliompinga kuchafuliwa vibaya.

Kwa wanaojua uwezo wa Kikwete na hali inayokikabili chama chake, hasa tuhuma za ufisadi, ingekuwa sawa na kujinyonga kama wangeridhia kushiriki midahalo.

Wangeshiriki na lipi la maana ambalo CCM wangewasilisha kwa wapigakura? Je, ingetokea wakaulizwa maswali muhimu na chokonozi, wangejibu nini?

Kwa mfano, kama wananchi wangemuuliza juu ya yeye na chama chake kunufaika na fedha za umma zilizoibwa na kampuni ya Kagoda, Kikwete angejibu nini?

Au, kama baadhi ya vyama vingekuja katika mdahaho huo na nyaraka zinazoonyesha majina halisi ya wakwapuaji wakiwamo vigogo wa serikali, Kikwete na chama chake wangesemaje?

Angeelezwa kwamba fedha hizo zilizoibwa katika fuko la madeni ya nje (EPA) zilitumika kumuwezesha kuingia madarakani chini ya jinai ya takrima, angeeleza nini?

Hivi Kikwete angejibu nini kama angeulizwa chanzo cha fedha zinazomwezesha mke wake kumpigia kampeni, ukiachia mbali madai ya matumizi ya mali na fedha za umma katika kufanya hivyo?

Bila shaka Kikwete angeulizwa mantiki ya mkewe, kwa mfano, kuanzisha NGO baada ya yeye kuingia madarakani. Angeulizwa kwa nini mke wake anayelindwa na fedha za umma anatumikia chama kimoja?

Swali jingine ambalo lingempiga chini na kumuacha uchi bila shaka lingekuwa juu ya ahadi zake za kuwapeleka Watanzania Kanani ambazo alitoa mwaka 2005 asitekeleze hata moja.

Pia swali juu ya ni vipi atatekeleza ahadi nyingine mpya lukuki anazozidi kutoa lingemuacha hoi mbele ya wapigakura kiasi cha kupunguza kura zake.

Hapa halijaulizwa swali moto kabisa kutokana na tukio la hivi karibuni la Shehe Yahya Hussein kuahidi kumpa ulinzi wa majini, tena katika karne ya 21 ya sayansi na teknolojia, ilhali anao walinzi wanaolipwa mabilioni ya shilingi.

Pia wengi wangetaka aeleze ni vipi alichezewa hadi kuanguka kama alivyodai Hussein bila kusahau kumbana aeleze ni kwanini Hussein amegeuka msemaji wake.
Angeulizwa kwa nini Yahya anaingilia mambo yanayopaswa kutolewa maelezo na yeye Kikwete au daktari wake na asimkemee, kama kweli hajamtuma kujenga hofu kwa Watanzania?

Hivyo basi, CCM imekataa kuweka shingo lake kitanzini na kufa ikijiona, ingawa hili si jibu mujarabu. Kwani wengi wamefanikiwa kuona woga wa chama hiki kiasi cha kushindwa kuiamini CCM-mwoga kuendesha taifa lao.

Kuna maswali mengine ambayo yangemsumbua hata kumuumbua Kikwete.

Kwa mfano, kama angeulizwa mantiki ya mwanae Ridhiwan kuwa na nguvu katika chama; unadhani angejibu nini?

Najua wanaohoji wasingekuwa na ubavu wa kumuuliza maswali makali kama haya. Bali wagombea wenzake hasa Dk. Willibrod Slaa angeyachomeka ili yapate majibu kwenye kadamnasi.

Kwa vile kugoma kushiriki midahalo kwa CCM kumewanyima wananchi haki yao ya kuchambua sera na mipango yao, kuna haja ya kuiogopa CCM kama ukoma.

Hakika kama chama hicho kimekosa hata mawazo ya kuwaeleza wananchi, kitapata wapi msuli wa kuwa na matendo ya kuwafikisha watakako?

Leo, Kikwete anajitahidi kuwaaminisha Watanzania kuwa atawavusha wakati pesa ya umma, licha ya kutumika vibaya, inaibiwa kila uchao?

Rejea kugundulika kwa wizi wa Sh.1,700,000,000 (trilioni moja na milioni mia saba) uliofichuliwa na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) kuwa ulifanyika ndani ya mwaka jana tu.

Fedha hizi ni sawa na takriban moja ya tano ya bajeti ya Tanzania ambayo ni trilioni 11.

Kupitia midahalo, wengi wangetaka kusikia majibu ya Kikwete, hata wagombea wengine, juu ya mantiki, kwa mfano, ya kupitisha wagombea wanaotuhumiwa kwa kashfa mbalimbali, kama vile ufisadi na kughushi vyeti ukiachia kutoa rushwa ambayo inasemekana imetolewa na wagombea wengi, kama sio wote, wa CCM.

Aidha, wengi wangetaka kumsikia Kikwete akielezea mipango yake ya kuvunja urafiki na watuhumiwa wa ufisadi ambao wamekuwa wakijisifu kuwa urafiki wao hauwezi kuvunjwa na vyombo vya habari.

Wengi wangetaka kusikia tathmini binafsi ya Kikwete ya utawala wake ulioonyesha wazi kulegalega na kufumbia macho ufisadi kiasi cha imani kuanza kujengeka kuwa CCM inaendeshwa na mafisadi.

Kwa jumla, maswali ambayo yangemuweka Kikwete msalabani kama angeridhia kushiriki midahalo, ni gunia.

Hapa CCM imekiri wazi udhaifu na utupu wake. Hakika, imedhihirisha kuwa imeisha na kuishiwa, ukiachia mbali kuwa mshiriki wa jinai na kuendeshwa kwa mawazo mgando yanayopingana na mambo ya kisasa kama midahalo.

Je, kwa hili, hukumu ya wapiga kura itakuwa kali kiasi gani? Tungoje tushuhudie ambacho hatukutegemea. Kuna uwezekano watu wasiamini masikio na macho yao huko tuendako.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: