Mifugo haistahili kuawa


editor's picture

Na editor - Imechapwa 01 September 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

WAANDISHI wa habari waliotembelea vijiji vinavyopakana na hifadhi ya wanyamapori, upande wa Kilosa, mkoani Morogoro hivi karibuni walishuhudia ukatili mkubwa dhidi ya wanyama.

Wakiwa ni wenyeji wa wananchi wanaoishi maeneo jirani na hifadhi hiyo, waandishi hao walielezwa kushamiri kwa mauaji ya mifugo kwa kupigwa risasi na walinzi wa hifadhi hiyo.

Wanavijiji wanasema wanavamiwa na walinzi wa hifadhi na kufurushwa kwenye maeneo wanayotumia kuchungia mifugo yao kwa kudaiwa kuwa wamevamia maeneo hayo.

Hapo ndipo walinzi wanapowaua ng’ombe, mbuzi na kondoo kwa risasi bila ya kujali kuwa ufugaji ndio shughuli muhimu ya kiuchumi kwa wananchi hao.

Wananchi wa vijiji vya Luhoza na Kiduwi walionyesha waandishi wa habari mabaki ya mifupa ya mifugo iliyouliwa pamoja na maganda ya risasi zilizotumika kuwaua.

Viongozi wa vijiji wanasema inashangaza serikali haijachukua hatua yoyote kuzuia ukatili huo dhidi ya wanyama licha ya kuwatumia taarifa mara kwa mara.

Kuanzia Juni mwaka huu hadi hivi karibuni, mifugo iliyouliwa kwa mtindo huo imefikia 150 hali inayoashiria kuwepo tatizo kubwa la uhusiano mbaya kati ya uongozi wa hifadhi na wananchi. Wananchi wanalalamika matukio hayo yamewasababishia hasara ya zaidi ya Sh. 200 milioni.

Hatuoni ni kwanini menejimenti ya hifadhi imeshindwa kujenga uhusiano mwema na wananchi wanaoishi jirani na hifadhi, lakini wakaamini ni sahihi kuendelea kutumia nguvu nyingi kama suluhisho la tatizo.

Kujenga maelewano na wananchi ni kazi ngumu lakini kugharamika kununua risasi na kulipa walinzi wa kufukuzana na mifugo na hatimaye kuwaua inawezekana. Ajabu!

Kwa kuwa ufugaji ni kazi halali nchini petu, wanaojishughulisha nayo wanapaswa kuthaminiwa kwani huo ndio mchango wao katika maendeleo ya nchi.

Iwapo wafugaji hawana mahali pa kuchungia mifugo yao, basi ni jukumu la serikali kuwasaidia kupata maeneo ya kufanyia shughuli zao badala ya kuwanyanyasa.

Tunapata hofu kwamba ipo siku wananchi wanaoonewa, kunyanyaswa na kudhalilishwa watachoka kuvumilia matendo hayo na watataka kuchukua hatua za kujitetea.

Nani yupo tayari kuachia mali zake na kwa wananchi wa Kilosa kuachia mifugo yao iteketezwe ovyo kwa risasi za moto? Wakifikia hatua hiyo hali inaweza kuwa mbaya kuliko ilivyo sasa.

0
No votes yet