Mikataba ya gesi, mafuta ipitiwe upya


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 25 July 2012

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

IMEZUKA staili moja siku hizi nchini ya kufikiri kwa kutumia kiungo fulani cha mwili badala ya kichwa. Aliyegundua kuwepo staili hii ingawa hajatangazwa kupewa Tuzo ya Nobeli ni meya wa jiji la Dar es Salaam, Didas Masaburi.

Kwa wasiomfahamu Masaburi, ni yule bwana mnene, mzito, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Dar es Salaam na mmiliki wa chuo cha manunuzi, mauzo na upangaji bei kilichopo Chanika nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Kwa hiyo, mtu mwenye sifa kubwa na nyingi kama Masaburi ni muhimu na anayeijua sana serikali na chama tawala kwa vile yeye mwenyewe ni mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na katika serikali, hivyo anaposema staili ya kufikiri imebadilika lazima tukubali.

Akizungumzia matatizo ya utapeli, ufisadi na hujuma miongoni mwa watu fulani fulani kuingilia utaratibu wa ubinafsishaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), Masaburi alisema tatizo la watu wengine ni kwamba wanatumia “nanihii” kufikiri!

Baada ya kutafakari sana hoja, mantiki na uzito wa maneno ya “poti” wangu Masaburi, nimekubali kuwa Watanzania wengi na hasa waliopo mjengoni wanafikiri kwa staili hii mpya ya “kimasaburisaburi”.

Hebu fikiria kwa mfano, fedha nyingi zilizogunduliwa kufichwa Ughaibuni huko Uswisi; nimesikia kwamba fedha hizo zimefichwa kwenye mabenki ya mji mkuu Berne, mji mashuhuri kibiashara wa Zurick na mji wa utalii na starehe wa Geneva !

Taarifa ya kugundulika fedha hizo kufichwa nje ya nchi, tena wahusika wa kuficha pesa hizo wakitajwa kuwa maofisa sita, waliohusika kwa namna moja au nyingine na utoaji vibali vya kutafuta mafuta na gesi katika pwani ya Tanganyika , ziliibuliwa na Wakenya.

Magazeti ya Kenya – Daily Nation na The East African – ndiyo yaliyotoa taarifa za awali kabisa kuwa mabilioni ya dola yalikuwa yamefichwa katika mabenki ya Uswisi.

Japokuwa hata fedha za Kenya , Uganda , Rwanda na Burundi zimefichwa nchini Uswisi, hizi za Tanganyika ndizo zinatia uchungu zaidi kwa sababu matatizo yetu ni mengi kuliko ya wengine.

Magazeti ya Kenya yalieleza kuwa akaunti hizo sita zilifunguliwa na maofisa waliopo kwenye sekta ya gesi na mafuta na kwamba tangu walipofungua akaunti hizo mabwana hao hawakurudi tena kuongeza au kuweka senti yoyote.

Kilichowashangaza wachunguzi wa mambo ni kwamba akaunti hizo baada ya kufunguliwa na maofisa wa sekta ya nishati na madini wanaosimamia utafutaji gesi na mafuta nchini, ziliongezewa pesa na wageni tu hadi zikanenepa ‘kishenzi’.

Taarifa zilizopo zinasema waliokwenda kuzinenepesha akaunti hizo za maofisa wa Tanzania wa sekta ya gesi na mafuta ni maofisa wa kampuni za kigeni za mafuta na gesi!

Swali la kujiuliza ni kwa nini kampuni za mafuta na gesi ziliona haja ya kuwawekea wakubwa hawa mapesa kwenye akaunti zao? Wote tunajua hakuna cha bure duniani, sasa hawa wakubwa wa gesi na mafuta walifanya kazi gani kustahili pesa hizo?

Pia inaeleweka kwamba maofisa wa kampuni za mafuta wasingeweza kujua akaunti za wakubwa wetu hawa wa mafuta na gesi bila kukutana nao na kupeana akaunti hizo! Hii inaashiria yalikuwepo makubaliano kuwa “nyie kafungueni akaunti halafu tuwawekee…”

Ukifika hapo ndipo unakumbuka mchango wa mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zito Kabwe alipolalamikia mikataba ya mgawanyo wa mapato baada ya mafuta au gesi kupatikana (Profit Sharing Agreement) inayoingiwa na maofisa wa Tanzania .

Zito alilalamika kwamba kampuni moja ya ya utafutaji mafuta na gesi imeingia mikataba na nchi mbili – Tanzania na Msumbiji, kwamba upande wa Msumbiji mkataba unataka nchi hiyo ipate asilimia 40 ya faida.

Lakini cha ajabu Zito anasema upande wa Tanzania mkataba unataka nchi kupata asilimia 10 tu ya faida! Kwamba kampuni hiyo hiyo moja, upande wa Tanzania tupate asilimia 10 lakini upande wa Msumbiji wao wapate asilimia 40!

Baada ya siri hii ya maofisa wa mafuta kuwekewa pesa kwenye akaunti zao za Ughaibuni ndipo tumeelewa kwa nini Tanzania ina mkataba mbovu wa kupata asilimia 10 tu wakati nchi nyingine zinapata asilimia 40 – rushwa, hongo, posho, zawadi walizopewa hawa.

Sasa hapa hatuna ujanja tena, dawa pekee ni kuvunjwa mikataba hii ya kitapeli na wakubwa hawa warejeshewe pesa yao waliyowawekea maofisa wetu wanaohusika na usimamizi wa sekta ya mafuta na gesi.

Yaani wao wawekewe mabilioni halafu kampuni za mafuta zichote hazina yote ya mafuta na gesi kwa miaka dahari hadi yatakapokauka? Mimi nasema mtu pekee anayetaka turejeshewe fedha hizi ni yule anayefikiri kimasaburi tu.

Yaani turejeshewe pesa hizo bilioni sijui ngapi halafu watoaji rushwa (kampuni ya mfuta na gesi) ziendelee kuchota mafuta na gesi asilimia 90 na kutuachia kiduchu cha asilimia 10! Hapana, siyo wote tunaofikiri kimasaburi nasi wengine tuna vichwa na tunavitumia.

Mkataba haukufikiwa in good faith tunayo haki kuuvunja. Ushahidi wa bad faith upo. Ni hiyo rushwa iliyowekezwa Uswisi, tunaogopa nini? Kama kweli kampuni hizi zilijadili mikataba kwa nia njema, rushwa ya Uswisi ya nini?

Vijisenti vilivyokutwa Ughaibuni havikurudishwa na mhusika hakuchukuliwa hatua yoyote badala yake alipandishwa cheo kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu huko CCM makao makuu.

Safari hii hatutaki wala hatuombi CCM wachukue hatua. Tunachokiomba seriously ni kwamba mikataba ya gesi na mafuta irejewe kujadiliwa ili tupate haki kama inavyofanyika katika nchi nyingine kama vile Nigeria , Gabon , Cameroon , Congo ya Brazaville, Angola na hata Msumbiji.

Kwa nini sisi tu ndio tupate asilimia 10 wakati nchi nyingine zote nilizozitaja zinapata asilimi 40? Kwa hili naomba wote tuungane, tunaofikiri kikawaida na wale wanaofikiri kimasaburi, tuungane kudai haki yetu ya kupata asilimia 40 na siyo kudai eti kurudishwa pesa zilizofichwa nje ya nchi!

0
Your rating: None Average: 5 (4 votes)