Mikoa mipya aina nyingine ya kupeana ulaji


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 23 June 2010

Printer-friendly version
Tafakuri

MIONGONI mwa mambo ambayo serikali ya Awamu ya Nne inasifiwa kwayo ni ukubwa wa serikali kwa maana ya baraza la mawaziri.

Alipoingia madarakani Desemba 2005, Rais Jakaya Kikwete aliteua baraza kubwa la mawaziri kuliko ambalo limewahi kuundwa na watangulizi wake wengine watatu.

Hata pale alipolipunguza mwaka 2008 kufuatia kashfa ya Richmond ambayo ilisababisha baraza hilo livunjike baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, bado lilikuwa kubwa zaidi kuliko ya watangulizi wake.

Katika baraza la kwanza, kulikuwa na mawaziri 30 na manaibu 31, ambao kwa mwaka mmoja yaani lilipoundwa mwaka 2006, lilikuwa linalipwa jumla ya Sh. 1,012,764 kama mshahara.

Kiasi hicho ni cha juu mno. Kwa mfano, baraza la mawaziri la mwisho la Rais Benjamin Mkapa, lilikuwa likilipwa kiasi cha Sh. 777,492,000. Mkapa alikuwa na baraza la mawaziri lenye wajumbe 28.

Gharama za ununuzi wa magari ya mawaziri wa baraza la kwanza la Kikwete ilikuwa mawaziri Sh. 3.15 bilioni na naibu mawaziri 31 ni Sh. 3.255 bilioni.

Kiasi hicho kikilinganishwa na baraza la mwisho wa Mkapa la mawaziri 28, gharama ya magari yao ilikuwa Sh. 2.94 bilioni na kwa naibu mawaziri Sh. 1.89 bilioni.

Ingawa baraza la mawaziri lilipunguzwa sana baada ya kuvunjika mwanzoni mwa 2008, bado katika macho ya wengi liliendelea kuonekana kubwa. Lilibaki na mawaziri 48; mawaziri kamili wakiwa ni 27 na manaibu 21.

Wakati wananchi wakiendelea kubeba mzigo wa baraza kubwa la mawaziri, juzi ametangaziwa kwamba sasa mikoa inaongezeka hadi kufikia 30.

Mikoa mipya minne imekwisha kuundwa ambayo ni Njeruma unaunganisha wilaya za Ludewa na Njombe kutoka mkoa wa sasa wa Iringa; mkoa wa Geita unaomega eneo la mkoa wa Mwanza wa sasa; mkoa wa Simiyu unaotengwa kutoka mkoa wa Shinyanga; na mkoa wa nne uko kwenye mchakato ambao utaitwa Mpanda.

Kwa mtazamo wa haraka, uundwaji wa mkoa unaweza kuelezwa kwamba ni kupeleka madaraka zaidi kwa wananchi, kwa maana hiyo ni kitu kizuri. Kwamba wananchi sasa watafikiwa na huduma muhimu.

Mbali na mikoa hii pia kuna orodha ndefu ya wilaya zilizoundwa zikifikia 16 hivi.

Hata hivyo, mikoa na wilaya havijawahi kuwa maeneo ya uwakilishi wa wananchi, ni mwendelezo wa serikali kuu.

Mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya wote hawa ni sehemu ya serikali kuu, kwa maana hiyo kuzidi kuvunja nchi katika vipande vya mikoa na wilaya si jambo lolote la maana kwa wananchi mbali ya kuongeza matumizi ya serikali.

Si mkuu wa wilaya au mkuu wa mkoa anayeweza kusema kwamba yu katika eneo lake la utawala kwa sababu ya kusaidia maendeleo ya eneo husika yaani mwakilishi wa wananchi!

Nitatoa mifano michache. Kwa utamaduni wa hivi karibuni nafasi za wakuu wa mkoa na wilaya zimethibitika kuwa ni nafasi za kutafutia “washikaji” kazi.

Mosi, wale waliokosa nafasi za ubunge na hivyo kushindwa kuwa mawaziri; lakini pia wale ambao walipata ubunge lakini kwa sababu ya uchache wa nafasi za uwaziri wanatafutiwa sehemu ya kuchomekwa.

Hakuna maelezo yoyote kwa mfano ya kumchukua mbunge wa jimbo fulani kwenda kuwa mkuu wa mkoa katika mkoa mwingine.

Ipo mifano, akina Dk. James Nsekela (Tabora Kaskazini), mkuu wa Mkoa wa Dodoma ; William Lukuvi (Isimani), anayeongoza Mkoa wa Dar es Salaam), Monica Mbega (Iringa Mjini), Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na Abdul Azizi (Lindi Mjini), Mkuu wa Mkoa wa Iringa.

Ukiacha hawa waliopata ubunge lakini kwa kuwa nafasi za uwaziri hazitoshi, bado wapo wanaotafutiwa mahali pa kipachukwa kwa kuwa hata ubunge uligoma; kwa hali hiyo wanapewa mkoa.

Hawa nni kama Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile, ambaye tangu ashindwe kwenye kura ya maoni na mbunge wa sasa wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, kazi yake imekuwa ni moja tu, kumuhujumu na kumsakama mbunge huyo. Kinyongo cha kushindwa.

Kimafao na nafasi wakuu wa mikoa ni sawa kabisa na mawaziri kwa maslahi na pengine wanawazidi kulingana na rasilimali ambazo zipo katika mkoani ambazo anaweza kutumia mbinu zake, halali na chafu, kujinufaisha.

Ukitafakari nafasi za wakuu wa wilaya, sura inayojengeka ni ile ile. Wana kazi gani? Je, wanaweza kuwa na kazi wakati kuna halmashauri ama za wilaya, miji, manispaa au majiji? Kazi gani wanafanya?

Mbona hawaonekani wakifurukuta kuleta mabadiliko yoyote ya maana kwa maisha ya wananchi?

Uzoefu wa uongozi wa mikoa na wilaya umethibitisha pasi na shaka yoyote kwamba viongozi wake ni wawakilishi wa serikali kuu, wapo ili kuhakikisha kwamba madaraka ya serikali kuu yanafika kwa wananchi.

Hawatendi kwa maana ya kuwapa nafasi zaidi wananchi kuamua kuhusu maisha yao, bali kuongeza nguvu za dola kila kona ya nchi.

Kama nia ya kugawa mikoa ni kuwapelekea wananchi madaraka zaidi, mikakati hiyo ingeelekezwa kwenye halmashauri, kuzisaidia wataalam bora zaidi, kuziwesha na kuzipa nguvu ya mapato na kuongeza ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kulingana na fedha zilizotengwa.

Ingekuwa na maana zaidi kama nguzu za Mkaguzi na Madhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, moto wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) vingejielekeza kusaidia halmashauri ziwajibike, kwa kufanya hivyo wananchi wangeona mabadiliko katika matumizi ya kodi zao.

Kwa hiyo hali hii inapotazamwa katika tathmini ya kuongeza idadi ya mikoa au wilaya haina maana yoyote ya kusukuma maendeleo zaidi kwa wananchi.

Hapa Kikwete amelenga kuwatafutia ‘washikaji’ nafasi za ulaji kwa kuwa kule juu kumejaa na kuendelea kupaunua si busara walau kwa sasa.

Lakini mbali na hili, tukijiuliza ni kwa kiwango gani kwa mfano mkoa mpya kama wa Manyara au wilaya mpya kama za Siha, Rorya na nyinginezo zimewahakikishia wananchi maendeleo zaidi?

Au ni kwa jinsi gani zimewaongezea uhuru wa ushiriki wao katika kuamua juu ya mustakabali wao? Jibu ni moja tu: Hizi ni taasisi za serikali kuu, zenye lengo la kudhibiti na kukamua wananchi.

Kama nia ni kuongeza nguvu kwa wananchi njia sahihi kwa nyakati zilizopo ni kutafuta jinsi ya kuimarisha halmashauri kwa maana ya kuwapa watendaji bora na kuongeza ufuatiliaji wa uwajibikaji.

Kufanya hivyo kutaongeza madaraka kwa wananchi, vinginevyo ugawaji wa mikoa hii ni aina nyingine ya kupeana ulaji.

0
No votes yet