Mikopo Elimu ya Juu: Kama tunachangia, basi hatuna deni


Owawa Stephen's picture

Na Owawa Stephen - Imechapwa 21 April 2009

Printer-friendly version

BODI ya Mikopo ya Elimu ya Juu imekuwa chanzo cha malalamiko na migomo isiyokwisha kati ya wanafunzi na serikali.

Yamekuwepo malalakiko kuwa Bodi haina uwezo wa kutambua hali ya kiuchumi ya Watanzania. Bodi haifanyi tathmini ya kuweza kutambua kila Mtanzania mahali alipo.

Bodi haijatambua mwananchi anafanya nini na kipato chake kikoje?  Ni halali kisheria? Vigezo vinavyotumika kutoa mikopo vimefanyiwa tafiti kulingana na hali halisi ya maisha ya wananchi?

Mambo ni tofauti katika utendaji wa Bodi ya Mikopo. Kuna mkanganyiko kuanzia uanzishwaji, jina lake na matokeo ya kazi yake. Taasisi hii haijaleta tija. Badala ya kushughulikia mikopo, imesababisha migogoro na minyukano kati ya wanafunzi na serikali.

Hii ni kwa sababu taasisi imefanya isichojua na kuleta majibu yasiyohitajika kwa wahusika.

Kwanza, sera ya uchangiaji nchini iliazishwa bila ridhaa ya Watanzania. Wananchi hawakushirikishwa katika maandalizi ya awali ya kuazisha sera ya uchangiaji.

Matokeo yake imekuwa mapokeo yanayoletwa kwa nguvu ya vyombo vya dola bila kujali kama wanaolazimishwa kuipokea wana uwezo wa kutekeleza matakwa ya sera ya uchangiaji.

Kuna jina la chombo chenyewe. Ni bodi ya mikopo inayoshughulika na sera ya uchangiaji? Hapa kuna kudanganya watu.

Hii ni bodi ya mikopo na inatekeleza sera ya ukopeshaji katika elimu ya juu. Sasa swali ni hili: Kama hivyo ndivyo, inakuwaje bodi itoe mikopo na wakati huohuo ishughulikie sera ya uchangiaji?

Uchangiaji ni kupeana michango. Serikali inayokusanya kodi ya wananchi inatakiwa itumie kodi hiyo katika kuwapa elimu iliyo bora na isiyo ya kibaguzi.

Kama ni kuchangia serikali inatakiwa kutamka wazi kisheria kiwango inachochangia kwa wanafunzi, na mwanafunzi au mzazi wake wachangie kiwango kinachosalia kulingana na uwezo wa aliyechangiwa.

Kutokana na serikali kutoza kodi na kuwajibika kutoa elimu, mwanafunzi hatakiwi kurudisha kiasi alichochangiwa na serikali. Hapo ndipo tutakuwa tunatekeleza sera ya uchangiaji.

Tunachoshuhudia hivi sasa ni udanganyifu kwa wanafunzi na jamii ya Watanzania kwa ujumla. Hakuna sera ya uchangiaji, ni sera ya ukopeshaji usiokuwa na utaratibu maalum.

Kasoro nyingine ipo kwenye utendaji na uwezo wa bodi yenyewe kuweza kufanya kazi ya kutambua hali ya kiuchumi ya waombaji mikopo.

Kwa sasa Bodi haina uwezo wa kuwatambua wenye uwezo. Inafanya kazi ya kutabiri, kubahatisha na wakati mwingine inachezesha majina ya wanafuzi kama karata ili kuweza kutoa viwango vya kuwakopesha wanafunzi visivyojali uwezo wa mwombaji.

Hii inadhihirishwa na barua ya Mkurungezi wa Bodi ya 5 Januari 2009 yenye Kumb. Na. CB/89/92, kwenda kwa marais wa vyuo vya elimu ya juu Tanzania, ikiomba msaada wa serikali za wanafunzi.

Mkurugenzi alitaka serilai za wanafunzi kuisaidia bodi kujua kama kweli wanafunzi wanaolipiwa asilimia miamoja, wanastahili kupewa kiwango hicho.

Hii inadhihirisha madai ya siku nyingi ya wanafunzi kwamba bodi ya mikopo haina uwezo wa kutambua nani ana uwezo na nani hana.

Chukua mfano mwingine wa barua  ya mkurugenzi mkuu wa Bodi yenye Kumb. Na. CB/89/92/049, kwenda kwa rais wa serikali ya wanafunzi Chuo cha Muhimbili.

Mkurugenzi anamwomba rais wa serikali ya wanafunzi na uongozi wake kwa ujumla, kumsaidia kutambua kama wanafunzi 16 wa mwaka wa kwanza na 26 wa mwaka wa pili, waliolipiwa asilimia miamoja wanastahili kufanyiwa  hivyo.

Majina yao, kozi wanazosoma na viwango walivyokopeshwa viliambatanishwa kwenye barua hiyo.

Kwa maana nyingine ni kuwa, serikali za wanafunzi zina uwezo wa kutenda kazi kuliko bodi ya mikopo, na hapa bodi inakiri kushindwa kwake kufanya kazi na kudhihirisha kuwa madai ya siku nyingi ya wanafunzi ni ya kweli na wanafunzi wengi walioko vyuoni wamepewa viwango wasivyostahili.

Hapa jambo la kusikitisha na kukatisha tamaa ni  lile la kuzipa serikali za wanafunzi vyuoni  kazi isiyo yao; ya kufanya kazi ya kuwa wana-usalama wa bodi hiyo, bila kujali kuwa viongozi wa wanafunzi nao ni wanafunzi kama wanafunzi wengine.

Ukisoma sehemu ya barua ya Mkurungenzi wa Bodi ya Mikopo ya 5 Januari 2009, ambayo nakala yake imepelekwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kuna sehemu inasomeka hivi:

“Ni matumaini yangu kuwa uchunguzi utakaofanyika, utafanyika kwa siri. Tunachohitaji ni jina lake, majina halisi ya wazazi wake, mahali wanapofanya kazi/biashara au cheo chake.”

Kwamba serikali ya wanafunzi inageuka kuwa taasisi ya uchunguzi na ifanye kazi ya kubaini majina halali ya mwanafunzi, wazazi wake, makazi yao na kazi/bishara au vyeo vyao.

Elimu ya nchi hii ipo rehani; imewekwa mikononi mwa wasiojua waifanyie nini Tanzania. Matokeo yake ndiyo haya ya Mkurungezi wa Bodi kuomba msaada kwa wanafunzi. Serikali za wanafunzi zina utaalam gani wa kutambua watu kuliko waajiriwa wanaolipwa na wananchi kufanya kazi hii?

Novemba 2008, serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO) iliunda timu ya wanafunzi viongozi kwenda Bodi ya Mikopo. Nilikuwa mwenyekiti wa timu hiyo; kwenda kuangalia ni kwanini wanafunzi wamebadilishiwa viwango vyao vya mikopo.

Kiutaratibu ni kwamba kila mwanafunzi anapewa kiwango cha mkopo mara moja kwa miaka yote atakayokuwa chuoni. Kwa mfano akipewa kiwango cha “C” akiwa mwaka wa kwanza, ina maana  atapewa mkopo wa asilimia sitini kwa kila mwaka kwa miaka yake yote ya masomo, bila mabadiliko kwenye asilimia anayokopeshwa.

Lakini kilichotokea mwaka jana ilikuwa kinyume na inavyotakiwa. Wanafunzi wengi walijikuta wakiwa na viwango tofauti na vya awali walivyopewa, tena bila taarifa yoyote ya mabadiliko hayo.

Kwa mfano, kuna wanafunzi ambao viwango vya mikopo wanavyopewa vilishuka kutoka asilimia sitini kwenda arobaini na wengine kupanda kutoka kiwango kimoja kwenda kingine. Tunaambiwa  wanafunzi hawatakiwi kuhoji. Hii ndiyo njia ya kuasisi migomo.

Jiulize, ni kwa nini barua iliyoandikwa na Mkurugenzi wa Bodi ya 5 Januari 2009 kwenda kwa marais wa serikali za wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu, haikujumuisha watu wanaokopeshwa asilimia 30, 30, 40,60 na 80? Kwa nini iwe kwa wanaolipiwa asilimia miamoja pekee?

Mbona bodi haijaomba kusaidiwa kuhusu  walionyimwa mikopo ili kuona kama wanastahili kupewa? Huu ni ubabahishaji.

Bodi inapaswa kufanya kazi yake na kuacha kufanya utabiri katika elimu.

0
No votes yet