Milioni 3.8 waikataa Sudan Kaskazini


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 09 February 2011

Printer-friendly version

HAYAWI hayawi yamekuwa. Tume iliyoundwa kwa ajili ya kuosimamia Kura ya Maoni kuhusu uamuzi wa Sudan Kusini kuamua mustakabali wake imetangaza kwamba asilimia 98.83 ya waliopiga kura wameamua kujitenga.

Kwa matokeo hayo ya Kura ya Maoni yaliyotangazwa juzi mjini Khartoum na mkuu wa tume hiyo Mohamed Ibrahim Khalil, Sudan Kusini ni nchi huru na yenye mipaka yake tofauti na Kaskazini.

Upigaji wa kura ya maoni ni sehemu ya makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwaka 2005 ya kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa zaidi ya miongo miwili kati ya kusini na kaskazini.

Taarifa zilisema kwamba karibu asilimia 99 ya watu waliopaswa kushiriki katika upigaji wa kura ya maoni mwezi uliopita walishiriki.

Juba

Baada ya Tume ya Maoni kutangaza matokeo hayo, wakazi wa mjini hapa ambako yatakuwa makao makuu ya Sudan Kusini walishangilia kwa vifijo.

Watu wapatao 1,000 walikusanyika usiku katika kaburi la kiongozi wa zamani hayati John Garang, kusikiliza matangazo hayo kupitia skrini kubwa ya televisheni.

Watu walikuwa wakipeperusha bendera za Sudan ya Kusini na wakishangilia kila hatua ya matangazo hayo.

"Tutaandamana mitaani kushangilia mpaka asubuhi,” alisema Peter Deng, ambaye ni kiongozi wa vijana. “Sote unaotuona tumekua kipindi cha vita, kwa hiyo tunafuraha kupita kiasi kushangilia uhuru tuliopata.”

Hata kabla ya matokeo yote kutangazwa juzi usiku, tayari baadhi ya wakazi walishaanza kushangilia baada ya taarifa kuvuja kwamba wengi walipiga kura kuunga mkono hoja ya Sudan Kusini kujitenga.

"Hiki ndicho kinachotokea serikali ikikandamiza haki za watu na kuwapuuza kwa kipindi cha zaidi ya miaka 50,” alisema Puok Dieu aliyeshiriki katika vita ya wenyewe kwa wenyewe. "Siku moja watu walionyanyaswa kiasi hicho watasimama na kusema: Imetosha.'"

"Matokeo ya Kura ya Maoni yanamaanisha kwamba niko huru leo," alisema Abiong Nyok, mwana mama wa nyumbani. "Kwa sasa ni raia wa Sudan Kusini daraja la kwanza."

Matokeo rasmi

"Wale waliopiga kura kutaka Sudan iendelee kuwa moja walikuwa 44,888, sawa na asilimia 1.17. Waliopiga kura kuunga mkono Sudan Kusini kujitenga walikuwa 3,792,518, sawa na asilimia, 98.83," alisema Khalil.

Katika makao makuu ya Sudan Kusini, Juba wananchi walishangilia kwa furaha mchana kubwa wakisubiri matokeo
Lakini, mwanamke mmoja anayetoka Kaskazini, alilia baada ya tangazo hilo akisema ana ndugu wanaoishi kusini.

Mapema Jumatatu, Rais Omar al-Bashir alisisitiza kwamba ataheshimu matokeo ya kura hiyo. Hata hivyo wasiwasi wake ni kwamba kutengana huko kunaweza kusababisha mgogoro juu ya udhibiti wa hazina ya mafuta iliyoko kusini.

"Tunayapokea na tunakaribisha kwa mkono miwili matokeo haya kwa sababu yanawakilisha matakwa ya wakazi wa kusini,” alisema Bashir kupitia televisheni ya taifa.

Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa Rais Bashir kutoa msimamo huo. Lakini msimamo wa sasa ulilenga kuwatoa wasiwasi wakazi wa Kusini kwamba serikali yake haitarudi nyuma.

Rais alisema anawahakikishia Sudan Kusini kwamba ataendeleza uhusiano mzuri na serikali ya baadaye ya kusini.

Kufuatia kura hiyo ya maoni, Marekani imetangaza kwamba itaiondoa Sudan kutoka kwenye orodha ya nchi inazozishutumu kwa kufadhili ugaidi.

Kiongozi wa Sudan Kusini, Salva Kiir ameahidi pia ushirikiano mzuri na serikali ya Khartoum kwa siku za baadaye akisema “kuna mambo mengi yanayohusisha kaskazini na kusini ".

"Uhuru huu wa kusini si mwisho wa njia, kwa sababu hatuwezi kuwa maadui. Lazima tujenge ushirikiano madhubuti," alisema Kiir, ambaye ni makamu wa rais wa Sudan. Kiir anatarajiwa kuwa rais wa Sudan Kusini.

Washington

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton alisema: "Tunawapongeza viongozi wa kaskazini na kusini kwa kusaidia mazingira ya upigaji kura kwa amani na mpangilio na kwamba sasa watu wa Sudan Kusini wamezungumza kwa kauli moja, tunaishauri serikali ya Sudan kupokea matokeo."

Hillary ambaye ni mke wa rais wa zamani wa Marekani alisema, Marekani kwa sasa “imeanzisha mchakato wa kuiondoa Sudan katika orodha ya nchi  zinazofadhili ugaidi duniani. Hatua ya kwanza ni ya kupitia mchakato huo ".

Naye Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa “kuisaidia Sudan kufikia uimara na ufanisi wa maendeleo” na kwamba UN itasaidia pande zote mbili.

Historia

Japokuwa upigaji kura ulifanyika kwa amani, kulikuwa na kiwango cha hali ya juu cha hofu katika maeneo yenye utajiri mkubwa wa mafuta.

Takriban watu 50 waliuawa mwishoni mwa wiki iliyopita katika mapigano yaliyohusisha wanajeshi katika jimbo la Upper Nile.

Katika kipindi cha nusu karne, wakazi wa Sudan Kusini walipigana vita vikali mara mbili na serikali ya Sudan Kaskazini. Katika vita hivyo, inakadiriwa zaidi ya watu milioni mbili waliuawa.

Wakazi wa kusini wanajiona kwamba wako tofauti kidini, kiutamaduni na asili ikilinganishwa na wenzao wa klaskazini ambao ni Waarabu. Kusini wanaamini wameuamia sana kutokana na kutengwa na serikali yao.

Masuala mazito kama kuhusu mpaka wa eneo la Abyei, uraia na masuala ya kisheria kuhusu raslimali ya mafuta bado yatahitaji majadiliano.

Japokuwa Sudan Kusini ni tajiri kwa mafuta, ni moja ya maeneo maskini duniani na kwamba misuguano ya kiasili na uhusiano mgumu na kaskazini vitabaki kuwa changamoto za muda mrefu kiusalama.

Tangazo rasmi juu ya uhuru wa Sudan Kusini litatolewa 9 Julai 2011 ikiwa miaka sita tangu utiwe saini mkataba wa amani uliowezesha kufanyika Kura ya Maoni.

0
No votes yet